UCHAMBUZI -TAMTHILIYA YA KIVULI KINAISHI
JINA LA KITABU: KIVULI KINAISHI
MWANDISHI: SAID A. MOHAMED
WACHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS
MWAKA: 1990
UTANGULIZI
Kivuli Kinaishi ni tamthiliya inayojadili na kuchambua matatizo mbalimbali yanayozikabili jamii zetu. Matatizo hayo ni kama vile uongozi mbaya,rushwa,kukosekana kwa haki,kuwepo kwa matabaka katika jamii,Ushirika na uzembe kazini.Kwa kutumia dhana ya Giningi mwandishi amefaulu sana katika kujadili matatizo yao.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU: UJENZI WA JAMII MPYA
Mwandishi ameonesha jinsi jamii ya Giningi ilivyooza.Ni jamii yenye matabaka,tabaka tawala la watu wachache wenye navyo na wanaopenda kila kitu kiwe chao.Pili kuna tabaka la chini,hili ni tabaka la walio wengi ambao hawana chochote,hata kile kidogo walichonacho hunyang’anywa.(uk 18) mazungumzo kati ya Bawabu II na mkulima.
Mfano:‘’Unadhani mpunga huu unatosha hazina ya Giningi?’’
Ili kuonyesha kuwa tabaka tawala linapenda kupata Zaidi kuliko kutoa;mkulima huyo ambaye alipata mpunga kidogo kutokana na kukosekana kwa matrekta,mbolea waliyohaidiwa,hakusikilizwa alipojitetea.Alihukumiwa adhabu kali.
Rushwa imeshamiri katika jamii ya Giningi.Wafanya biashara ndio wanaotendewa haki ya upendeleo kwa sababu ya rushwa.Bawabu II alishindwa kuwatetea walimu,wakulima na tabibu kwa sababu hawakutoa rushwa.Katika (uk 24-25) mwandishi anaonesha jinsi kukithiri kwa rushwa kunavyosababisha kupotea kwa haki katika jamii ya Giningi.
Kutokana na hali hii,mwandishi anaonesha kuwa hata kuingia katika utawala wa Giningi ni lazima mtu atoe rushwa ndipo akubalike.Kwa mfano,Mtolewa alitoa shs. 5000/- (uk 28-29) ndipo aliruhusiwa kupita langoni.
Katika jamii ya Giningi,viongozi wamejigeuza miungu wadogo wenye kuishi milele.Wao ndio wenye sauti ya kusema na kutoa mawazo.Viongozi hao hawaangalii matatizo ya nchi kama vile shule kukosa huduma bora za kuboresha elimu,hospitali kukosa dawa,n.k. Badala yake wamepoteza muda mwingi katika sherehe za pombe na ngoma badala ya kutatua matatizo yanayowakera wananchi.
Uozo mwingine unajitokeza katika jamii ya Giningi ni ule wa watu kulazimishwa kusema uongo badala ya ukweli,yaani uongo ni ukweli na ukweli uongo.Mfano tabaka tawala hudanganya wananchi kuwa matatizo ya nchi husababishwa na vita,ukame,kupanda kwa mafuta, n.k. (uk 98).
Pia,mwandishi ameonesha kuwa,jamii ya Giningi maisha yake yamejaa chuki,kisasi,fujo na woga unaowaandama wananchi wa kawaida.
Hivyo mwandishi ameonesha kuwa ili tujenge jamii mpya yenye kuondokana na matatizo haya, lazima wananchi wasimame imara kupingana na aina zote za dhuluma,uonevu,kupiga vita rushwa na kuondoa matabaka katika jamii.Vilevile ameonesha kuwa,ili tujenge jamii mpya lazima tufanye mapinduzi ambayo yatawaangamiza wagandamizaji kama vile Bi Kirembwe.
MBINU ZA UJENZI WA JAMII MPYA
UONGOZI MBAYA
Suala la uongozi mbaya limewashughulisha sana waandishi wengi wa Afrika wakiwemo waandishi wa Fasihi ya Kiswahili.Viongozi wa Afrika waliotwaa madaraka kutoka kwa wakoloni,wengi wao wana sifa zinazofanana na Bi Kirembwe wa serikali ya Giningi.Wao walijigeuza na kuwa viongozi wa kudumu milele na milele na hali hii imekwamisha ufanisi wa ujenzi wa jamii mpya katika nchi za Afrika.
Nyerere aliainisha vigezo vine vya kuleta maendeleo katika nchi changa kama Tanzania kuwa ni Ardhi,Watu,Siasa safi na Uongozi bora, lakini jamii ya Giningi imekosa maendeleo kwa sababu imekosa siasa safi.Imekosa siasa safi kutokana na kukosekana kwa uongozi bora.Hivyo maendeleo ya Giningi yamekwamishwa na uongozi mbaya wa Bi Kirembwe na wazee wenzake.
Bi Kirembwe ana hali zote za udikteta, anasema kwa niaba ya watu,anaua watu ovyo pale wanapotaka kumpinga,anawanyima watu uhuru wa kuabudu na badala yake wanamuabudu yeye kama Mungu.Hapendi mabadiliko – anakatalia kwenye madaraka,ana ukatili na vitisho visivyo kifani pamoja na uchawi uliokithiri.Kutokana na hali hiyo,amefanya kila hila na amefanikiwa kujifanya Mungu,mchawi wa wachawi,Bwana wa Mabwana,n.k. (uk 33-36) na (uk 56-60).
Utawala wa Bi Kirembwe umeleta hofu na vitisho kwa Wanaginingi.Bi Kirembwe hapokei ushauri wowote ule hata ukiwa mzuri.Anayetoa ushauri anauwa (uk 65-68) na (uk 73-75).Kama hiyo haitoshi, Bi Kirembwe anajistarehesha kwa vileo na ngoma wakati raia wengine wanaathirika na hali ngumu ya maisha.
Vilevile Bi Kirembwe amejilimbikizia madaraka yote.Ni mama wa wote,ni malkia,ni mfalme,ni hakimu, n.k.
Pia Bi Kirembwe ameshindwa kukemea maovu yanayotendeka nchini mwake kama vile rushwa na kukosekana kwa haki, kutokuwepo kwa demokrasia,n.k.Nchi za dunia ya tatu hususani nchi za Afrika zimeshindwa kujenga jamii mpya kwa sababu ya kuwa na viongozi wabinafsi na wasioshaurika kama Bi Kirembwe.Baadhi ya viongozi waliopewa madaraka na wananchi,waliwageuka wananchi hao na baadhi yao walijitangaza kama Maraisi wa maisha.Hali hii inasababisha bara la Afrika kushuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe mfano Sudan,Burundi, Rwanda, Kongo, Algeria,Sierra Leone, Angola, n.k.
Hivyo mwandishi anapendekeza kuwa,ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi mzuri.Uongozi mbaya ni kikwazo kikuu cha ujenzi wa jamii mpya katika nchi zinazoendelea.
KUFANYA MAPINDUZI (MAGEUZI)
Kuanzia onyesho la saba na kuendelea tumeoneshwa jinsi Mtolewa alivyoshirikiana na Wari kuleta mapinduzi katika jamii ya Giningi.Lengo kuu lilikuwa ni kuanganisha utawala mbovu wa Bi Kirembwe.
Katika harakati za ukombozi (kufanya mageuzi) Mtolewa aliwaunganisha Wari na kuwakomboa kifikra kwa kuwalisha unga wa rutuba. Katika harakati hizo Mtolewa na wale Wari walikamatwa na kuuawa lakini vuguvugu la mapinduzi walilokuwa wamekwisha pandikiza kwa kizazi kile lilisaidia sana kuutokomeza utawala mbovu wa Bi Kirembwe.(uk 118-119) mwandishi anasema;
‘’Tunaishi Bi Kirembwe,sote tunaishi,sote tulioangamia,………Sura zetu zimo ndani ya viwiliwili vya watoto wetu.Mawazo yetu yamo ndani ya bongo zao.Imani na itikadi imo ndani ya maisha yao…….tunaishi,ni vivuli vinavyoishi visivyoweza kufa,ni sauti zinazosema kimya kimya nahata kwa matamko ya wazi……’’.
Vivuli viliendelea kumsumbua Bi Kirembwe hadi anauona mwisho wake, kwani hata viungo vyake vya mwili vilimsaliti (uk 128).
Mfano: Macho ya Bi Kirembwe – Mimi ni shahidi wa maovu yote uliyoyatenda ya kudidimizana kuangamiza.
Mikono – Sisi ni mashahidi …….
Miguu – Nami pia nilikuchukua kwenye mienendo yako……
Kitaswira viungo vya mwili wa Bi Kirembwe ni wale watu waliokuwa karibu sana na Bi Kirembwe kama vile wazee na mtangazaji ambao wanamsaliti Bi Kirembwe kutokana na matendo yake mabaya.
Hali hii ilitokea kutokana na vuguvugu la mapinduzi kupamba moto.Vizazi vipya kwa kutumia mawazo ya Mtolewa viliendeleza mapambamano kama asemavyo mwandishi (uk 128).
‘’Sisi ni vizazi vipya Giningi,vizazi vya walioangamia ………Vizazi vya waliodidimia ………Sisi sasa tuna kinywa kipana….tuna uwezo wa kuamua tunavyotaka, kuamua wenyewe……….kwa maslahi ya wote………Hatutachagizwa tena na uchawi. Tunakuja ……. Tunakuja……..’’
Pia mwandishi ameonesha jinsi Bi Kirembwe anavyogwaya na kuanza kuhangaika kutokana na wimbi la mapinduzi kupamba moto.(uk 129),Mwandishi anasema;
‘’Ah, hata wewe Bi Kirembwe leo unagwaya? Unatetemeka kama…..? Unalialia kama mtoto mchanga au mwanamke aliyefiwa na mumewe? Unahofu matokeo ya matendo yako mwenyewe…..’’
Nadharia ya kujenga jamii mpya kwa njia ya mapinduzi inaoneshwa kutetewa na waandishi wengi. Nadharia hii inaonekana kuwa muhimukwa sababu tabaka tawala halipendi kuachia madaraka kwa hiari hasa katika utawala wake.
‘’Unasubiriwa kwa hamu ndani……..Ingia na ukishaingia keti juu, usikubali kuporomoka chini . Chini kuna udhia……..’’
Hivyo mwandishi anapendekeza kuwa,ili tujenge jamii mpya ni lazima tufanye mapinduzi au mageuzi ya kuwaondoa viongozi wabovu.
KUJITOA MHANGA
Bila kujitoa mhanga hakuna mapinduzi ambayo yanaweza kufanikiwa.Mtolewa na Wari walijitoa mhanga kuleta mabadilko katika jamii ya Giningi.Pia Mtolewa alianzisha mabadiliko makali dhidi ya Bi Kirembwe.Aliamua kufanya hivyo baada ya kutembelewa na mizimu.
Vilevile Mtolewa alijitoa mhanga katika kuwakomboa Wari wenzake kifikra kwa kuwalisha unga wa rutuba kama asemavyo mwandishi katika (uk 90);
‘’Hamtoweza kufahamu mpaka niwatoeni mzigo mlio nao…..hamtatambua mpaka nikufumbueni macho na kukuzibueni masikio……’’
Mtolewa aliwafumbua macho Wari wenzake kwa kuwalisha unga wa rutuba – elimu ambayo inamfanya mtu ajitambue na atambue nafasi yake katika jamii na uwezo wa kuwaelimisha wenzake.
Mtolewa alijibizana na Bi Kirembwe kwa kujiamini na bila matatizo yoyote na hii yote inatokana na moyo wa ushujaa na ujasiri aliokuwa nao katika harakati za kutokomeza utawala mbaya wa Bi Kirembwe (uk 108).Mtolewa alijibu;
‘’Najiamini kama mchawi yeyote anavyojiamini………’’
Mwisho mwandishi ameonesha kuwa Mtolewa aliuawa na kuangamizwa kabisa.Mtolewa alijua wazi kuwa atauawa lakini hakuogopa,bali aliendesha mapinduzi kwa ujasiri.Hii hudhihirisha kuwa jamii mpya haitoshi kujengwa kwa siasa safi na uongozi bora bali kuwepo kwa watu waliojitoa mhanga kufanya mapinduzi hayo.
KUWEPO KWA DEMOKRASIA YA KWELI
Demokrasia ni mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu.Katika jamii ya Giningi hakuna demokrasia ya kweli kutokana na uongozi mbaya wa Bi KIREMBWE.
Bi Kirembwe amebadili madaraka ya serikali ya Giningi na kujitangaza kama mtawala wa milele. Hivyo amewanyima wananchi wazalendo wa Giningi demokrasia.(uk 71).
‘’Ndiye mwenye kustahiki kukalia kiti hiki daima…..kukikalia daima dawamu’’
Katika jamii ya Giningi wananchi wananyimwa haki ya kuwachaguaviongozi wao wenyewe wanaowataka kwa kuwa hakuna demokrasia, kwani demokrasia imetekwa nyara na Bi Kirembwe.
Vilevile Bi Kirembwe hakuruhusu majadiliano nchini Giningi.Watu walifundishwa kusema uongo badala ya ukweli au kulazimishwa kukubali masharti magumu pasipo majadiliano.Mfano usiku kuwa mchana na mchana kuwa usiku.
Watu wanaoonekana kutoa mawazo ya hekima mbele ya Bi Kirembwe,hivyo adhabu yao huwa kifo.Mfano wa watu hao ni mkulima,tabibu na mwalimu ambao walielezea waziwazi matatizo hayo.
Vilevile wale wazee watatu waliuawa kwa sababu walifikiri kinyume namatakwa ya Bi Kirembwe hatakama walikuwa na mawazo mazuri ya kuiendeleza Giningi kimaendeleo,(uk 74) kama anavyosema mwandishi;
‘’Tulidhani tutaweza kutoa mchango wetu; tulijisemea tu, tena ndani ya nyoyo zetu kwamba sisi pia tulikuwa na sehemu ya kutaka kuiona Giningi ya namna tofauti kama tunavyofanya.’’
Halikadhalika Mtolewa aliuawa na Bi Kirembwe kwa sababu ya kutaka kuiona Giningi inajengwa kwa misingi ya haki na usawa.Alionekana machoni pa Bi Kirembwe kama msaliti wa utawala wake (uk 114).
Hivyo kuwepo kwa demokrasia ya kweli katika jamii ni mbinu moja wapo itakayosaidia ujenzi wa jamii mpya katika nchi zinazoendelea.
UMUHIMU WA ELIMU
Elimu ni kitu muhimu sana katika ujenzi wa jamii mpya.Elimu inaweza kumpumbaza mtu akapumbazika,huweza kumlaza mtu akalala nahata kushindwa kujenga jamii mpya.Kwa upande mwingine,elimu inaweza kumuamsha mtu aliyelala usingizi akaamka na usipokaa chonjo huyo mtu aliyeamka anaweza kufanya makubwa yasiyotegemewa katika jamii.
Katika tamthiliya hii,elimuimetumika katika nafasi zote mbili.Elimu ilitumika kuwapumbaza Wanaginingi waamini kuwa Bi Kirembwe ni Mungu mdogo.Giningi hakuna kubisha,unapotaka kusema lazima upate amri kutoka kwa Bi Kirembwe.Giningi hakuna matatizo kwa mtazamo wa Bi Kirembwe.Bi Kirembwe hakosei katika utawala wake huko Giningi.Giningi wanaendeshwa kwa mwendo wa ngoma.Elimu hii waliipata kwa njia ya unga wa ndere (mawazo ya Bi Kirembwe) na mawazo haya ndio yanayowafanya hata watawala wetu kuanzisha itikadi mbalimbali ambazo kila mtu anatakiwa azifuate.
Kwa upande mwingine,mwandishi ameonesha jinsi elimu ya kimapinduzi waliyoipata akina Mtolewa ilivyosaidia kufanikisha kuleta mapinduzi katika jamii ya Giningi.Elimu hii ilimwezesha Mtolewaasikubaliane na mambo ya Bi Kirembwe hata siku moja.Elimu hii ndiyo iliyomwezesha Mtolewa kuwalisha Wari unga wa rutuba.Kupitia elimu hii ndipo Wari walipojitambua wana nafasi gani katika jamii yao.Ndipo walipogundua kuwa katika Giningi hakuna Amani bali kuna mateso makali.Kutokana na elimu waliamua kufanya mapinduzi.
Kwa hiyo,mwandishi anatuonesha kuwa elimu ni kitu chenye ncha kali na itategemea utaitumia jinsi gani, ukiitumia vizuri itakuamsha na ukiitumia vibaya itakupumbaza akili.Hivyo elimu ni kitu kinachokata nyuma na mbele.
KUPIGA VITA RUSHWA
Kukithiri kwa rushwa katika jamii ya Giningi kunakwamisha ujenzi wa jamii mpya.Bawabu II anapokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara (uk 24-25).Vilevile alipokea rushwa ya Shs. 5,000/- kutoka kwa Mtolewa ili aruhusiwe kuingia ndani yaani aingizwe Giningi.
Kutokana na kukithiri kwa rushwa,haki haitendeki hata kidogo.Watu wasio na uwezo wa kutoa rushwa wananyimwa haki zao katika jamii ya Giningi na vilevile wanapewa mashtaka ya uongo ambayo hatimaye yanawaangamiza.Mfano mzuri ni tabibu,mwalimu na mkulima.
Hivyo mwandishi anapendekeza kuwa, ili tuweze kujenga jamii mpya yenye kufuata haki na usawa, hatuna budi kupiga vita rushwa na badala yake haki itendeke kwa kila mmoja (raia).
KUPIGA VITA MATABAKA
Katika tamthiliya hii,mwandishi ameonesha matabaka ya aina mbili.Ambapo kuna tabaka tawala na tabaka tawaliwa.Tabaka tawala linawakilishwa na Bi Kirembwe,wazee,mtangazaji na Bawabu I – II.
Tabaka tawaliwa linawakilishwa na Wari pamoja na sauti za wahenga walioangamizwa na Bi Kirembwe.Linaonewa,linanyanyaswa,linadhulumiwa,linagandamizwa na kusingiziwa kila uovu mfano:kuuawa kwa mkulima,tabibu na mwalimu.
Katika tamthiliya hii,tabaka tawala linanyonya,linaonea,linagandamiza na kunyanyasa tabaka tawaliwa.Vilevile tabaka hili linawalazimisha watu wa tabaka la chini kusema uongo ni kweli na kweli ni uongo.
Vilevile tabaka hili hutafuta kila aina ya visingizio kuhalalisha matatizo yanayowakabili watu wa tabaka la chini kama vile mvua,ukame,mbolea,vita,mafuta,n.k.Hivyo ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita matabaka.
USHIRIKINA (UCHAWI)
Habari nzima ya maisha ya Giningi imefungamana na imani ya uchawi.Bi Kirembwe anafanya mambo yake kama anavyotaka kwa sababu ya uchawi wake,anaogopwa na kuabudiwa na kila mtu.(uk 34) Mwandishi anasema;
“ Mchawi wa wachawi mjua yote ya ndani nay a nje, ardhini na hewani, mtambua mema na maovu,mruka hewani na mwota ndoto……”
Ushirikina kama ulivyokuwa tatizo katika Giningi ndiyo unavyoelekea kuwa tatizo katika nchi zetu. Viongozi wetu wanaamini kuwa wanaweza kuendelea kuwa viongozi kwa kujizindika madawa na ndiyo maana baadhi ya viongozi hutafuta uongozi (madaraka) kwa mbinu ya uchawi.
Ni vigumu kujua dhima ya uchawi au ushirikina katika ujenzi wa jamii mpya kwa sababu njia zake si za wazi,walio wengi hawawezi kuona wazi yanayotendeka;isipokuwa waliozindikwa kama anavyofanya Bi Kizee kwa watoto (uk 7).
“………..haya aje mmoja hapa. Watoto wanasogea………”
Mwandishi anaonesha kuwa jambo hili la uchawi na ushirikina lipo kama kawaida ya mambo yote lina nafasi yake na wakati maalumu na wakati huo ukiisha halina nguvu tena kama asemavyo Bi Kirembwe (uk 115);
“………..Tuseme uchawi wangu unaanza kupungua?……….Lakini aaa, potelea mbali, mimi najijua ni umbo la milele………….”
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Katika tamthiliya hii mwandishi amechorwa mwanamke katika pande kuu mbili,ambazo;
Kwanza amechorwa kama mtawala wa kidikteta, atishaye watu na si kiumbe duni tena kama waandishi wengine wanavyochora.Bi Kirembwe amepewa nafasi na dhamana kubwa kwa Giningi. Amechorwa kama mama wa Giningi baba wa Giningi, mlezi wa Giningi, mzee wa Giningi, mfalme wa Giningi, mchawi na hakimu wa Giningi (uk 33-35) na (uk 56-60).
Pamoja na kupewa dhamana Bi Kirembwe ametumia nafasi hii vibaya,kwani anaitumia kwa kunyanyasa,kuonea,kugandamiza na kunyonya watu.Anashindwa kutumia vizuri nafasi hii ya uongozi aliyopewa kuendeleza Giningi pamoja na wananchi wake:
Kwa upande mwingine mwanamkeamechorwa kama mwanamapinduzi,mfano mzuri Bi Kizee ambaye ameonekana wazi kuchukia matendo maovu ya Bi Kirembwe pamoja na viongozi wengine Giningi.Amesimulia watoto hadithi hii ili waone wenyewe matendo hayo ili waweze kurekebisha mfumo wa aina hii wa maisha (onyesho la 1, 6, 10).
HALI NGUMU YA MAISHA
Katika tamthiliya hiimwandishi ameonesha kuwa hali ngumu ya maisha huwakumba sana watu wa tabaka la chini.Watu wa tabaka hili wana hali ngumu ya maisha kulinganisha na ile ya watu wa tabaka la juu.
Tabaka la juu hutoa ahadi za uongo kwa tabaka la chini lakini halitekelezi ahadi hizo (uk 18);ndio maana shule hazina vitabu,madawati,chaki,vifaa vingine,mishahara kidogo,hakuna chakula,madawa na vifaa vingine vya hospitalini hakuna hospitalini (uk 21).Kukosekana kwa vifaa hivi vyote kunasababisha hali mbaya ya maisha kwa watu wa tabaka la chini ambao ndio wengi.
Kwa upande wa tabaka la juu (tawala) linaona kuwa, hali hiyo mbaya ya maisha imesababishwa na vita vya Wanaginingi pamoja na ukame. (rejea uk 44-45).
Pia tabaka hili (tawala) linaona kuwa, hali ngumu ya maisha inasababishwa na kushuka kwa bidhaa zetu katika masoko ya nje na kupanda kwa bei za vifaa kutoka nje.Katika (uk 98), kwa upande mwingine mwandishi anaonesha kuwa mvua,ukame,mbolea,vita,mafuta….vimechangia kwa kiasi kidogo sana kuleta hali mbaya ya maisha.Ukweli ni kwamba,hali mbaya ya maisha imeletwa na ubinafsi wa viongozi wetu,rushwa na unyonyaji unaoendeshwa na watawala.Mtolewa kwa upande mwingine anaona kuwa,hali mbaya ya maisha inasababishwa na kuwa na maneno mengi bila matendo.
UJUMBE
Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na uongozi mzuri,tufanye mapinduzi, tujitoe mhanga, tupige vita rushwa na tuzingatie elimu itakayowakomboa watu kifikra.
Kila jambo lina wakati wake ukiisha na jambo hilo linaisha; kamwe wakati haulazimishi kufanya jambo la milele.
Kufanya mapinduzi katika jamii si mchezo na lelemama bali kunahitajika wapatikane ambao wako tayari kuifia jamii yao kama alivyofanya Mtolewa.
Dunia imejaa matatizo mbalimbali, hivyo lazima watu wafanye bidii kuyatatua matatizo hayo.
Tuchukie, tuyaangamize na kuyakemea maovu katika jamii, kwani hayana faida yoyote kwa jamii.
Tusipendelee urahisi katika maisha.Maisha ni mapambano,lazima tupambane ndipo utaishi maisha mazuri.
MIGOGORO
Mgogoro kati ya Mtolewa na Bi Kirembwe,chanzo cha mgogoro huu ni mtolewa kutaka mabadiliko kwa kuwalisha wari unga wa rutuba ili wampinge bi kirembwe,suluhisho ni mtolewa kuuawa.
Mgogoro kati ya Mtolewa na Sauti za wahenga,chanzo cha mgogoro huu ni mtolewa kuwasaliti wahenga ambao walimsomesha ,walikumlea na walimtuma giningi akafanye mapinduzi ya utawala Bi kirembwe badala yake yeye aliungana na bi kirembwe.Suluhisho ni wahenga kumkumbusha mtolewa.
Mgogoro kati ya Bi Kirembwe na viungo vyake vya mwili yaani macho,mikono na miguu (mgogoro binafsi),chanzo cha mgogoro ni viungo vya bi kirembwe kushindwa kufanya kazi na suluhisho ni bi kirembwe aliachia madaraka (alikufa).
Mgogoro kati ya bi kirembwe na mtangazaji,chanzo cha mgogoro huu ni mtangazaji kuanza kumpinga bi kirembwe na utawala wake,suluhisho ni bi kirembwe kumkaba na kumuua mtangazaji.
FALSAFA
Mwandishi anaelekea kuamini kuwa palipo na mvutano kati ya wema na ubaya,lazima wema hushinda na hivyo haki hutawala.
MSIMAMO
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani ameonesha wazi matatizo mbalimbali yanayoikabili njamii yetu kama vile uongozi mbaya, rushwa, dhuluma, kukosekana kwa demokrasia ya kweli, hali ngumu ya maisha, n.k.
FANI
MUUNDO
Tamthiliya Ina muundo changamano; yaani kuna visa viwili ndani ya kimoja au tamthiliya mbili ndani ya moja.Kuna kisa cha Bi Kizee na Watoto na kisa cha Maisha ya Giningi.
Kimpangilio tamthiliya imegawanyika katika maonyesho kumi.Onyesho la 1, 6 na 10 yanahusu Bi Kizee na Watoto lakini maonyesho yaliyobaki yanahusu maisha ya Giningi.Mwisho maonyesho yote yanafanya kisa kionekane kama mduara, kwani kisa kinamalizika pale kilipoanzia tena kwa maneno yaleyale.Kuhusu mtiririko wa matukio, msanii ametumia muundo rukia ambapo matukiohurukiana na huenda nyuma na mbele
MTINDO
Mwandishi ametumia mtindo changamano.Kuna mtindo wa monolojia (masimulizi) na dayolojia (majibizano).Vilevile mwandishi amechanganya tanzu tatu katika tamthiliya hii: Ngano,Ushairi na Tamthiliya na Nafsi zote tatu zimetumika.
WAHUSIKA
Wahusika wakuu: Bi Kirembwe, Mtolewa na Bi Kizee.
BI KIREMBWE
Mtawala mkuu wa Giningi
Amejilimbikizia madaraka
Ni mwakilishi wa viongozi madikteta,mfano:Anaua watu ovyo,anawanyima watu uhuru, hapendi mabadiliko.
Amejitangazia utawala wa maisha
Anapenda starehe
Anatumia elimu yake kuwafumba watu macho
Hafai kuigwa katika jamii
MTOLEWA
Mwanamapinduzi
Aliwalisha Wari unga wa rutuba
Jasiri na mvumilivu
Alijitoa mhanga kuifia nchi yake
Mpigania haki
Mtetea wanyonge
Mpinga dhuluma
Anafaa kuigwa katika jamii
BI KIZEE
Ndiye anayesimulia habari za maisha ya Giningi
Anapenda haki na usawa
Anawatayarishia vijana kufanya mapinduzi
Anafaa kuigwa katika jamii
BAWABU I – II
Ni wahusika wadogo na ni wawakilishi wa vyombo vya dola ambavyo vinaendeleza rushwa na ukandamizaji wa watu wa tabaka la chini. Hivyo hawafai kuigwa katika jamii. Wahusika wengine ni: wari, watoto, wazee, wasichana, n.k.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha iliyotumika ni lugha ya kawaida yenye misemo, methali, tamathali za semi, taswira na picha mbalimbali.
METHALI
Kuishi kwingi kuona mengi (uk 6).
Unachumia juani unalia kivulini (uk 24).
Kikulacho kinguoni mwako (uk 67).
Majuto ni mjukuu (uk 111).
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
Mbona tumeambiwa una hadithi tele tumesikia hazikauki kwako kama maji ya bahari (uk 5).
Watoto wa siku hizi………tena wana maneno makali kama chiriku (uk 7).
Watu wenyewe hufanya kazi kama punda…………(uk 19).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
MDOKEZO
Subirini, subirini………
Sawa………sawa………..sawa
Ndiyo…..ndiyo…….ndiyo…….Sawa! Sisi ni Wari,
TANAKALI SAUTI
Lakini…………he……….he………he………(uk 52).
Ha…………ha……………..haaaaaaa!
Ha, ha, ha……………ha, ha, ha, haha!
UJENZI WA TASWIRA
Unga wa ndere – Itikadi zinazomfanya mtu katika tabaka tawala akubalike na kushika miiko yaani elimu ya kuwapumbaza watawaliwa ili waone kila kinachofanywa na tbaka tawala ni sawa.
Unga wa rutuba – elimu ya kujitambua katika jamii na kujitambua nafasi yako na kuwa na uwezo wa kuelimisha wengine.
Sauti – mawazo ya tabaka la chini lililoathirika kutokana na utawala wa Bi Kirembwe.
Kivuli kinaishi – mawazo ya kimapinduzi yaliyokwisha pandikizwa kwa vizazi vipya ili kudai haki na usawa.
Uchawi – itikadi za viongozi wasiotaka mabadiliko.
Giningi – ngazi ya utawala wa juu katika jamii.
MANDHARI
Mwandishi ametumia mandhari ya Kitanzania kutokana na kutajwa kwa miji kama vile Unguja na Pemba.Vilevile mambo kama rushwa,uongozi mbaya na hali ngumu ya maisha vinaashiria nchi za dunia ya tatu kama vile Tanzania,ambapo baadhi ya viongozi hutumia vibaya madaraka yao.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu linasadifu yote yaliyomo ndani ya kitabu.Kitaswira linaashiria mawazo ya kimapinduzi yaliyopandikizwa na Mtolewa kabla hajauawa ambayo vizazi vipya vilivyofuata viliyatumia hadi vikaleta mapinduzi.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui mwandishi amefanikiwa kuonesha matatizo na mbinu za kuondokana na matatizo yanayozikumba jamii zetu.
Kifani, mwandishi amefanikiwa kuchora wahusika katika pande mbili yaani Wana – mapinduzi na wapinga mapinduzi.
No comments:
Post a Comment