Sunday, April 12, 2020

FAFANUA MAANA YA FASIHI SIMULIZI KWA KUREJELEA MAONI YA WATAALAMU TOFAUTI.

FAFANUA MAANA YA FASIHI SIMULIZI KWA KUREJELEA MAONI YA WATAALAMU TOFAUTI.
Maana ya fasihi simulizi
Fasihi simulizi imeelezwa kwa namna tofauti na wataalamu mbalimbali wa fasihi.
Finnegan (1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalumu. Katika fasili hii Finnegan hajagusia mambo muhimu katika fasihi simulizi kama vile muktadha, namna ya uwasilishaji, uhifadhi na badala yake amejikita zaidi katika ubunifu alionao msanii anayeiumba fasihi husika. 
Kirumbi (1975:15) ameona kwamba, fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu awali, kwa ajili hii basi, tutaona katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kusema).
Matteru (1983:26) anatueleza kuwa fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo kwa kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake. Aidha Matteru anaendelea kusema kwamba, fasihi simulizi ikiwa ni sanaa itumiayo maneno katika kutoa dhana fulani, hutegemea sana nyenzo mbalimbali za kuonekana na kusikika zitumiwazo na binadamu katika kujieleza.
Msokile (1992:3) anasema kuwa fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha. Kazi hiyohuifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Anamalizia kwakusema kwamba, fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Fasili hii ina ubora wake kwa sababu ni kweli fasihi simulizi hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na pia njia kuu ya uwasilishaji wake ni masimuliizi ya mdomo, lakini kwa upande mwingine ina mapungufu kwa sababu inaonesha njia moja tu ya uifadhi wa fasihi simulizi kwa maana kwamba fasihi simulizi huhifadhiwa kichwani tu, haijazungumzia njia zingine za uhifadhi wa fasihi simulizi zilizotokana na maendeleo endelevu ya sayansi na teknolojia kama vile vinasa sauti, kanda za kurekodi na maandishi.
Mlacha (1995:16) ametueleza kwamba fasihi simulizi ni nyanja katika maisha ya jamii am- bayo huchangia sana katika kuiendeleza na kuidumisha historia ya jamii husika. Alipokuwa akifafanua zaidi juu ya fasihi simulizi Mlacha alisema kuwa ‘fasihi simulizi huchangia katika kuelimisha jamii kuhusu asili yake, chanzo na maendeleo ya utamaduni wake na maisha ya jamii hiyo kuanzia zamani’.
Wamitila (2003:44) anatueleza kwamba, fasihi simulizi ni dhana inayotumika kurejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo. Yeye kwa hakika hayuko mbali sana na msingi mkuu wa fasihi simulizi uliosababisha kuwepo kwa tawi hili la fasihi. Kwa upande mwingine Wamitila (2003:15) anatueleza kuwa tawi hili la fasihi linatu- miwa katika jamii kama njia ya kupashana maarifa yanayohusu utamaduni fulani, historia ya jamii, matamanio yao, mtazamo wao na historia yao. Kwa mtazamo wake huo, tunaweza ku- jumuisha kuwa fasihi simulizi ndicho chombo muhimu cha jamii.
Mwanafasihi Kimani Njogu (2006: 2) anatueleza kuwa fasihi simulizi ina ubunifu na uhai wa kipekee wenye kutoa fursa njema ya kuibua nadharia za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Pia a- naifananisha aina hii ya fasihi na uti wa mgongo wa maendeleo ya binadamu, kwani ndani yake kuna masimulizi, maigizo, tathmini za mazingira na mahusiano ya kijamii.
Kezilahabi (1989) anasema; fasihi simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhanna ya fasihi itolewayo kwa mdomo bila kuandikwa. Istilahi hii ina dosari kwani neno simulizi halina maana ya kinachosemwa –oral- bali ni kitu kinachosimuliwa –narrative-.

TUKI (2004) inatoa fasili ya fasihi simulizi kuwa ni fasihi inayo uhifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine kwa njia ya mdomo kama vile hadithi, ngoma, navitendawili. fasili hii inamaana kuwa nyenzo kuu ya uwasilishwaji wa fasihi simulizi ni mdomona kwamba fasihi simulizi hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine baada ya kuhifadhiwa.Lakini fasili hii ina mapungufu yake kwa mfano haijaelezea hiyo fasihi simulizi inahifadhiwawapi ili iweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kwa mujibu wao njia kuu yakuwasilisha fasihi simulizi ni mdomo kwa maana kwamba hakuna njia nyingine inayowezakutambulisha fasihi simulizi zaidi ya njia ya mdomo pekee.
Kwa mawazo ya wataalamu hawa, twaweza kuhitimisha ya kuwa fasihi simulizi ni sanaa ina- yotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira husika. Hii ni sanaa ambayo ujumbe wake upo katika mfumo mzima wa pande mbili za mawasiliano kuwepo pamoja ana kwa ana hii ikimaanisha fanani yaani mtu anayerithisha (msimuliaji) na Hadhira yaani mtu anayerithishwa (msimuliwaji). Kwa njia hii fasihi simulizi hushirikisha au huwafikia watu wengi na mawazo ambayo jamii iliyakubali, imeyakubali, ina- endelea kuyakubali yatokeapo na inayapitisha na au kuyakabidhi kwa kuendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine kwa njia ya mdomo. Kwa hali hiyo basi, kwa vile taarifa zinazopatikana ni za mdomo, upo uwezekano wa utata, upotoshwaji na upoteaji wa taarifa muhimu za kale ambazo kama zingeliandikwa zingelidhihirisha ukweli wa mambo yalivyo- kuwa.
Haiyumkini mapokeo ya fasihi simulizi yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuiunda, kuirekebisha, kuifundisha na kuiboresha jamii.
Vile vile kutokana na fafahuzi hizo inaweza kueleweka kuwa fasihi simulizi ni sanaa inayoitumia lugha ya kusemwa( masimulizi na utendaji) inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya ana kwa ana, mfano njia ya elekroniki kama vile CD, redio na runinga. Fasihi simulizi hii huhifadhiwa kwa njia ya kichwa, maandishi au kurekodi ili iweze kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Fasihi simulizi ndiyo fasihi ya awali. Aina hii ya fasihi imeanza wakati binadamu alipoanza kutumia lugha kama moja ya chombo cha mawasiliano. Tangia hapo ndipo mwanadamu alipoanza kuimba, kutumia methali, vitendawili, nahau, n.k.
Jinsi dunia ilivyobadilika kimaendeleo, na fani za fasihi simulizi ziliendelea kubadilika. Kuto- kana na mabadiliko hayo ya binadamu tangu alipomudu kutumia lugha, uwepo wa maendeleo endelevu hadi kutokea kwa mapinduzi ya viwanda na baadaye mwishoni kuingia kwa tekno- lojia mpya, haya yote yalisababisha mabadiliko hadi katika fasihi simulizi.
Mabadiliko haya yaliigawa fasihi simulizi katika fasihi simulizi ya zamani ambapo ilianza sambamba na bina- damu kujua kutumia lugha. Baada hapo, kulipotokea maendeleo ya mitambo na kutokea ma- pinduzi ya viwanda, pakatokea mabadiliko katika fasihi simulizi na kukatokea fasihi simulizi ya kisasa.
Kuingia kwa teknolojia mpya kuliibadili fasihi simulizi ya sasa, hivyo kuanzia sasa twaweza kuipa jina la fasihi simulizi teknolojia mpya. Kwa nadharia hiyo basi, makala haya yataangalia aina kuu mbili tu za fasihi simulizi yaani fasihi simulizi ya zamani na ile ambayo kwa mapokeo ya kisasa ni ya fasihi simulizi teknolojia mpya.
Utata uliopo wa kufasiri fasili ya fasihi simulizi
Hadi sasa kuna tafsiri nyingi juu ya dhanna ya fasihi simulizi kutokana na kutoafikiana kwa wataalamu wa fasihi. Kirumbi (1975) anasema: fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo. Katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kucheza na lugha). Kwa maelezo ya Kirumbi ni kwamba chombo cha kutongolea fasihi simulizi ni midomo na kwa hiyo katika fasihi simulizi tunakuwa na masimulizi.
Kuna baadhi ya wataalamu wanadai kuwa fasihi simulizi ni masimulizi ya kale ambayo hurithishwa kizazi kimoja hadi kingine. Kwa baadhi ya watu fasihi simulizi hufungamanishwa na masimulizi ya mambo ya kale. Kwa jina la kashifa fasihi hii huitwa fasihi ya kimapokeo. Baadhi ya wanafasihi hudai kuwa istilahi yenyewe ina mgogoro hivyo wanataka Istilahi mbadala itumiwe badala ya Simulizi. Kezilahabi (1989) anasema; fasihi simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhanna ya fasihi itolewayo kwa mdomo bila kuandikwa. Istilahi hii ina dosari kwani neno simulizi halina maana ya kinachosemwa –oral- bali ni kitu kinachosimuliwa –narrative.
Hivyo tafsiri ya fasihi simulizi katika Kiingereza ni –narrative literature- sio –oral literature-.Pamoja na migogoro  huu kikubwa kufahamu ni kuwa fasihi simulizi ni utanzu mmoja wa fasihi. Na fasihi simulizi ni sanaa ya masimulizi na matendo inayofikisha ujumbe kwa hadhira iwe ni kwa kuimba, kutenda au kuzungumza. Fanani katika fasihi simulizi hufaulu kutoa picha halisi ya dhanna anayoikusudia iwe ni huzuni, furaha, kuchekesha au kusononesha. Katika usimuliaji fanani hujitathmini kama anafaulu au la kwa kuitazama hadhira yake. Hali hii humsaidia kubadili mbinu za usimuliaji, vilevile fanani huweza kushirikisha hadhira yake na kuleta uhai katika masimulizi yake.
Usuli wa fasihi simulizi
Nadharia ya fasihi simulizi ni mawazo yanayotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jambo fulani katika fasihi simulizi.
Kwa kufanya hivyo, nadharia hizo zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo kwa mfano utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, uchongaji, jando na unyago umeathiriwa na ujio wa wageni.
Watafiti wa Kimagharibi na wa Kiafrika wameangalia mambo mengi yaliyoikabili fasihi simulizi ya Kiafrika na mawazo yao ni kama yafuatavyo:
MSAMBAO
Waasisi wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na wanaubadilikaji taratibu ambao waliamini kuwa kufanana kwa fani mbili za kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa za kimaendeleo.
Wanamsambao wanaamini kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea, sababu ya msingi ya mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani, jamii hizo ziliwahi kukutana kwa namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana baadhi ya mila na desturi.

Wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa kutoka katika jamii imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo dhaifu. Hivyo basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi ya Kiafrika ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda sehemu nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano ushairi simulizi wa Kiswahili ulitoka Uarabuni na Uajemi kuja Afrika.

KISOSHOLOJIA
Nadharia hii ina mihimili mitatu ambayo ni ule wa Umahususi, mkazo katika utendaji na dhima ya fasihi simulizi katika jamii. Umahususi, ulijikita zaidi katika jamii peke yake badala ya taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla kama walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi.

Katika Utendaji, Wanasosholojia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji wa kazi mbalimbali za fasihi simulizi.
Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya fasihi wana ujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa
husika na jambo hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha utendaji.
Katika msisitizo kuhusu dhima ya fasihi simulizi katika jamii, wanaamini kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.
Kutokana na mawazo ya wananadharia, hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni ndani ya jamii za Kiafrika zenyewe na si vinginevyo.

UTAIFA
Nadharia hii ilizuka kwenye vuguvugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa wanadai kuwa wananadharia wa utandawazi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za Kiafrika.
Kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na Wazungu kupitia mlango wa ukoloni.
Utaifa umeasisiwa na Adeboye, Babalola, Daniel Kunene na Clark. Katika nadharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa kuondoa kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti. Wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.
Ili kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu na wanachuo wa taifa au jamii hiyo kwa sababu wataalamu na wanazuoni hao ndio wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.
HULUTISHI
Nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni wa Kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza taaluma ya fasihi ya Kiafrika. Wananadharia hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni na ya kijadi zimeathiriana na kuingiliana.

Miongoni mwa waasisi na wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Mulokozi, Johnson na Ngugi wa Thiong’o. Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na wa kijadi.

Hata hivyo, fasihi simulizi ya Kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni lakini ilianza kupata athari mara baada ya ujio wao. Athari na mwingiliano wa fasihi simulizi hauonyeshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwa kuwa fasihi yoyote lazima iathiriwe na iathiri fasihi nyingine.

Hivyo basi kila jamii au taifa huwa na fasihi yake na utamaduni wake ambapo maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza kuathiriana na hivyo kuathiri pia fasihi ya jamii husika.
UAINISHAJI WA TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Uanishaji wa tanzu za Fasihi simulizi unakumbwa na matatizo mbalimbali, jambo linalopelekea wataalamu kutofautiana katika kuainisha tanzu hizo na kupelekea kuchanganya watu mbalimbali hasa wanafunzi katika kujua ni zipi hasa ndizo tanzu za fasihi simulizi. wataalamu wengiwametofautiana katika kuainisha tanzu za fasihi simulizi kwa mfano:
Kutofautiana kwa uainishajiwa tanzu za fasihi simulizi miongoni mwa wataalamu hao kumetokana na matatizo mbalimbali yanayoikumba fasihi simulizi kama yafuatayo:
Utajiri wa tanzu za fasihi similizi miongoni mwa jamii za kiafrika. fasihi simulizi huumbwa kutokana na mazingira ya jamii husika na hali ya shughuli zao, jamii hutofautiana  sana kimazingira pamoja na shughuli zao hali inayosababisha kuwepo kwa fasihi nyingi na za namnatofauti tofauti miongoni mwa jamii mbalimabali, hali hii inasababisha kuwepo kwa tanzu nyingi za fasihi simulizi yaani zikikusanywa fasihi simulizi za kihaya, kilugulu, kinyiha,kinyakyusa,kigogo,Kikuyu, kikamba, kichaga, kipare, na nyingine nyingi unaweza kubaini tanzu nyingi zisizo na ukomo jambo ambalo si rahisi kwa mtaalamu yeyote kuainisha tanzu na vipera vyote vya fasihi simulizi, hivyo kila mtaalamu huainisha kulingana na ufinyu wa uwelewa wa jamii mbalimbali na ukomo wa utafiti wa mtaalamu husika. Hivyo basi kila jamii ina tanzu zake za fasihi simulizi ambapo zaweza kufanana na jamii nyingine au kutofautiana kabisa kutokana na utofauti wa tamaduni moja na nyingi.
Kutokuwepo kwa vigezo mahususi vitakavyokubalika na wataalamu wote vya uainishajiwa tanzu za fasihi simulizi ni jambo jingine linalosababisha ugumu katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi.
Ni wazi kwamba katika shughuli yoyote inayohusisha uelezeaji, uainishajiauubainishaji wa tanzu za fasihi simulizi haifungwi na mipaka mahususi jambo ambalo kilamtaalamu anaamua kutumia vigezo au hatua azitakazo yeye na kwa kuwa vigezo ni tofauti basi wataalam au wanafasihi huishia kutofautiana na kila mtaalamu kuona vigezo vyake ni borakuliko vigezo vya mtaalamu mwingine. Hivyo basi kutokuwa na vigezo mahususi katikauainishaji wa tanzu za fashi simulizi ni tatizo. Mfano:
Mulokozi(1996) Kwa upande wake Mulokozi anaainisha tanzu za fasihi simulizi katika makundi sita ambayo ni  MAZUNGUMZO, MASIMULIZI, MAIGIZO, USHAIRI, SEMI, na NGOMEZI. 
(1)MAZUNGUMZO
Hotuba
Malumbano ya watani
Ulumbi 
Soga 
mawaidha
(2)MASIMULIZI
a)     Hadithi  -
Ngano  (Istiara, Mbazi, Kisa)
b) Salua –
kisakale,
mapisi,
tarihi,
kumbukumbu,
kisasili
(3)  MAIGIZO (tanzu zake hutegemea na shabaha na muktadha
 (4)USHAIRI
a)     Nyimbo
Tumbuizo
Bembea ·       
Za dini ·       
Wawe ·       
Tenzi /Tendi ·       
Mbolezi ·       
Kimai ·       
Nyiso ·       
Za vita ·       
Za taifa ·       
Za watoto ·       
Za kazi

(b) Maghani (ya kawaida, ya sifo- kivugo na tondozi)             
Ghani masimulizi – rara, ngano, sifo, tendi
(5)SEMI
methali
vitendawili
misimu
mafumbo
lakabu
(6)NGOMEZI -       
Za taarifa         
Za tahadhali         
Za mahusiano k.m mapenzi
semi
masimulizi
mazungumzo
maagizo
ushairi
ngomezi
Okpehwo(1992) kwa upande wake anaziainisha katika makumbo yafuatayo:
Nyimbo za maghani
masimulizi
semi
ngomezi
Mwanafasihi huyu anatoa mchango wake ifuatavyo kuhusiana na uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi.
Okpewho anaeleza kuwa uainishaji wa hadithi/ngano ni tatizo la muda mrefu. Hata hivyo anaeleza kuwa kuna vigezo/njia nne mpaka sasa ambazo zimetumiwa kuainisha hadithi/ngano.
Kwanza, kigezo cha unguli (protagonist of the tale), katika kigezo hiki kunajitokeza ngano zihusuzo wanadamu, ngano za wanyama, ngano za vichimbakazi, na ngano za miungu. Hata hivyo kigezo hiki kinaonyesha kuwa na matatizo
Matatizo hayo ni pamoja na kufanana kitabia kati ya jamii moja na nyingine.       Kwa mfano katika ngano za wanyama, wanyama hupewa uwezo wa kuzungumza, kufikiri, na kutenda kama wanadamu. ·
Pia kigezo hiki kinapuuza namna mbalimbali katika ngano ambazo vichimbakazi, wanadamu na wanyama huhusiana.
Pili, kigezo cha lengo la ngano husika (purpose of the tale), katika kigezo hiki ngano zinaainishwa kwa kuzingatia lengo la simulizi husika. Hapa panajitokeza ngano za kimaadili, ngano za kuhimiza kazi n.k. Okpewho anaeleza kuwa katika kigezo hiki kundi kubwa la ngano ni zile za kimaadili.
Tatu, kigezo cha sifa ya ubora wa ngano (characteristic quality of the tale), kigezo ambacho ndicho kinaonekana kubeba kundi kubwa la ngano. Katika kigezo hiki kuna ngano ayari (trickster tales)-hizi huambatana na uelevu au ulaghai wa wahusika; ngano za mtanziko (dilemma tales) na ngano za kihistoria ambazo huhusu vita, vizazi, mashujaa, usuli wa kitu/jambo fulani n.k.
Nne ni Kigezo cha muktadha wa utendaji wa ngano husika. Katika kigezo hiki kinachoangaliwa ni ngano inatendwa wakati gani na katika mazingira gani. Kwa mfano, kwa kutumia kigezo hiki tunaweza kupata ngano zinazotendwa wakati wa mbalamwezi (moonlight tales), ngano zinazotendwa wakati wa ibada (divination tales), ngano zinazotendwa wakati wa mapumziko ya wawindaji (hunters’ tales) na nyinginezo.
Kwa ujumla vigezo hivyo vina matatizo kwa sababu kuna uwezakano wa aina moja ya ngano kujitokeza katika vigezo vyote. Kutokana na utata huo, Okpewho anazianisha ngano katika makundi yafuatayo:
Kundi la kwanza ni hekaya (legends). Kundi hili linaelezwa kuwa ndio kundi kubwa kabisa la hadithi na hujumuisha tarihi, ngano za mashujaa, ngano za mapenzi n.k.
Kundi la pili ni ngano fafanuzi (explanatory tales). Hizi hufafanua asili ya kitu au wazo kwa kuzingatia mazingira na tajiriba za jamii. Kundi hili linajumuisha aina mbili kubwa: (1) Ngano zinazoelezea asili ya kuumbwa kwa ulimwengu, (2) Ngano zinazosawiri sifa na tabia za viumbe mbalimbali katika mazingira yao.  Aina hii ya pili hujumuisha visasili na visaviini.
Kundi la tatu ni ngano zisizo fafanuzi (fables). Kundi hili hujumuisha hadithi zinazohusu tajiriba zihusuzo wanyama, viongozi wa dini iwe katika ulimwengu au vinginevyo. Katika hadithi hizi msimulizi hatoi maelezo maalumu ni namna gani hadhira iifasili hadithi hiyo.

Balisidya (Matteru) (1987) Anagawanya fasihi simulizi  katika tanzu tatu ambazo ni:
Nathari,
Ushairi
Semi
(1) NATHARI
A.      Ngano
Istiara ·
Hekaya ·
Kwa nini na kwa namna gani ·
kharafa
B.      Tarihi ·
Kumbukumbu ·
Shajara 
Hadithi za historia ·
epiki
C.      Visasili ·       
Kumbukumbu ·       
Tenzi ·       
Kwa nini na kwa namna gani
(2) USHAIRI
A. Nyimbo
Tahlili
Bembea
Tumbuizo 
Ngoma 
Mwiga 
Watoto 
kwaya
B.Maghani
Majigambo 
Vijighani 
Shajara 
tenzi
(3) SEMI
A.   Vitendawili
Kitendawili 
Mizimu 
mafumbo
 B.    Methali
Msemo
nahau
C.      Misimu
Utani 
Masaguo
soga
Upungufu wa uainishaji huu
Katika uainishaji wake, baadhi ya tanzu hazionekani ama tunaweza kusema zimeachwa kabisa. Mfano visakale, ngomezi, Balisidya anauweka utenzi kuwa ni kipera cha visasili katika kundi la nathari.
Hapa anaibua mjadala kwani kama tujuavyo kuwa utenzi katika fasihi simulizi huhusisha uimbaji pia. Hivyo swali la kujiuliza ni je utenzi ni nathari?
Vilevile kuna kuingiliana kwa tanzu. Mfano kumbukumbu na kwanini na kwa namna gani ni tanzu ambazo zinajitokeza katika kundi zaidi ya moja.

Ngure(2007) yeye anaainisha kama ifuatavyo:
usimulizi
tanzu fupi
ushairi simulizi
Wamitila(2010) ameainisha tanzu zifuatazo:
hadithi
maagizo
ushairi
semi
ngomezi
Simiyu (2013) ameainisha tanzu hizi nne kama ifuatavyo:
semi bunifu
ushairi
maagizo
hadithi.
Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi.
Kwa upande wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan  kinachoitwa Oral Literature in Africa  (1970) . Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kuna miongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile  Balisidya, N  (1975)  na Taasisi ya Elimu (1987)
Kule nchini Tanzania Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.
Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.
Hivyo basi utata umekuwa ukijitokeza katika uanishaji na ugawaji wa tanzu na vipera vya fasihi simulizi. Utata huu unatokea kutokana na kutofautiana kwa vigezo vinavyotumiwa na wataalamu mbalimbali katika ugawaji huu, kwani kila mtaalamu hutumia vigezo vyake kulingana na matakwa ama mtazamo wake. Hebu sasa tuwatazame baadhi ya wataalamu ambao wameainisha tanzu za fasihi simulizi, tukiangalia pia udhaifu na ubora wa vigezo walivyotumia.
Kuingiliana kwa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kiuwasilishwaji ni moja ya
matatizo ya uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi. wanafasihi wanakubali kwamba katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi kuna ugumu kutokana na kwamba tanzu hizo huingiliana katika uwasilishwaji.kwa mfano muziki huweza kuuwasilishwa kama sanaa ya maonesho na semi kuuwasilishwa kama mazungumzo au masimulizi. Hivyo kutokana mwingiliano huo si rahisi kuainisha tanzu zafashi simulizi. Ambapo katika vipera upo ugumu katika utanzu wa ushairi hasa kati ya kipera cha nyimbo na maghani mfano: kazi za kifasihi alizoshiriki Mrisho Mpoto kama vile“Gongo lamboto” Jomba”, “Adela”
na nyingine kama hizo ni kazi kuhitimisha kama ni maghani au ni nyimbo kwani kuna sifa za kuitwa nyimbo na zipo sifa pia za kazi hizo kuitwa maghani.
Mabadiliko yanayoikumba fasihi simulizi ni moja ya tatizo katika uainishaji wa tanzu zake.Fasihi simulizi sio tuli kwa maana ya kwamba hupokea mabadiliko kulingana na mfumo wamaisha ya watu na kwasababu si tuli basi tanzu zake huweza kuongezeka kutokana na mfumohalisiwa maisha kwani maendeleo endelevu ya sayansi na teknolojia yamepanua uwanja wakimaingiliano wa kifasihi katika nyanjaya maisha, mwingiliano huo  husababisha uchanganyaji wa tanzu za fasihi simulizi wa jamii zinazokutana jambo ambalo kimsingi ni endelevu hivyohuleta ugumu katika kuainisha tanzu za fasihi simulizi.
Kutokuwepo kwa nadharia zinazoongoza uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi ya Kiswahili.1japokuwa fasihi simulizi ni kongwe lakini kitaaluma fasihi simulizi ni changa kwa sababu imeanza kuchunguzwa hivi karibuni. Hivyo inapelekea mahitaji ya taaluma hiyo, kwa upande huu wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za fasihi simulizi kwa undani ni kitabu chaRuth Fennegana kinaChoitwa (Oral Literature in Africa, 1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za fasihi simulizi na badala yake kuna miongozomichache kwa ajili ya shule za sekondari mfano:( Taasisi ya Elimu 1987 ) Hivyo kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza uanishaji wa tanzu za fasihi simulizi, wataalamu wengiwemekuwa wakitumia vigezo mbalimbali kama vile fani na maudhi na kuleta utofauti katika kuainisha kwao.
Kutokana na kuwepo kwa ugumu katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi kama kikundi tunapendekeza njia ambayo itakuwa ni msingi wa uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi.
Kama inavyofahamika kuwa utendaji ndio msingi mkubwa wa fasihi simulizi. hivyo basi kama utendaji ndio msingi wa fasihi simulizi si ngumu kukubali kuwa tanzu zote za fasihi simulizi zijulikanazo na zisizojulikana labda kwa sababu ya ufinyu wa mazingira tunayoyafahamu au mipaka ya tafiti zina utendaji.
Kwa hiyo, njia bora ya uanishaji wa tanzu za fasihi simulizi ni utendekaji wa tanzuya fasihisimulizi husika, hii inamaana kuwa kwa kila utafiti utakaofanywa katika kubaini uwepo wa tanzufulani ya fasihi simulizi ni lazima zihusianishwe na utendekaji wa tanzu hizo.
Sifa bainifu za fasihi simulizi
Fasihi simulizi ina sifa zake mbalimbali ambazo ni pamoja na zifuatazo:
Husambazwa kikalima
Huwa na hadhira mahususi iliyo hai
Huwa na wakati na mahali maalumu pa uwasilishaji
Huwa na fomula ya kiada ya kuanza na kumaliza
Hulenga utendaji kunaoifanya hai
Mtunzi asiyejulikana bali ni mali ya jamii
Hubadilika kulingana na wakati
Wahusika wa aina mbalimbali
Huwa na vipera vingi
Hutungwa kila wakati
Msimuliza ndiye mhusika wa kati
Ala zake kuu ni sauti, mdomo na ishara za mwili

Majukumu yake/dhima katika jamii.
Kukuza, kueneza, kuboresha na kuhifadhi utamaduni.
Kukuza, kueneza, kupanua na kuhifadhi lugha.
Kuitumbuiza jamii.
Kuhifadhi historia ya jamii.
Kuwahamasisha wanajamii kujikomboa kisiasa na kitamaduni.
Kusifia viongozi au asasi za kijamii zilizo bora.
Kukosoa na kuelekeza uongozi na asasi za kijamii.
Kuelimisha jamii kuhusu mazingira yake.
Kuhamasisha wanajamii kudumisha na kuimarisha utu na utanmaduni wao.
Kuhifadhi amali, maarifa na mmmsingi wa jamii.
Vikwazovinavyoikabili fasihi simulizi.
Uvumbuzi wa maandishi. Awali Fasihi Simulizi ndiyo iliyokuwa sanaa ya pekee ya lugha. Kupitia kwayo wanajamii walijifurahisha na kuhifadhi mila na tamaduni zao. Mengi sasa huhifadhiwa katika maandishi
Washindani badala. Awali, watoto walijumuika kusimuliwa hadithi au vitendawili. Siku hizi pumbao la watoto halitokani na masimulizi kwa sababu wametekwa na vitumeme vya kila nui. Fasihi Andishi, redio, runinga, tarakilishi, mtandao, pataninga na vifaa vinginevyo hutumiwa siku hizi kama njia badala za kujipumbaza.
Mapisi. Watoto wa sasa hushughulika mno na elimu ya vitabu kuliko ya Mapokeo
Mwingiliano na mtagusano wa jamii mbalimbali. Mtagusano wa watu wa jamii mbalimbali umepunguza uhalisia wa Fasihi Simulizi. Vijana hawawezi kujieleza kwa lugha moja. Kumeibuka jamii isiyo na lugha wala utamaduni imara. Wamerithi mchanganyiko wa mawazo kadhaa. Labda tuuite utamaduni mseto au chotara.
Uhakiki wa Fasihi Simulizi. Ulinganishi wa Fasihi Simulizi za jamii mbalimbali hudumaza tanzu hizi. Tamasha za muziki na maigizo shuleni na vyuo huwa zimetengwa na hali halisi ya utendaji wa tanzu hizi.
Mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu hutilia mkazo masomo mengine huku Fasihi Simulizi ikipuuzwa
Ya kuzingatia ili fasihi simulizi iendelee kuwepo
Kusisitiza utafiti wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi
Kuifundisha Fasihi Simulizi shuleni na taasisi nyinginezo
Kuhimiza uhifadhi wa Fasihi Simulizi
Kuhakikisha lugha za kienyeji hazifi
Kupambana na lugha za kikoloni ili wanajamii wasidharau Fasihi Simulizi

Hitimisho.
Kwa kuzingatia yaliyajadiliwa katika makala haya ni dhahiri shairi  kuwa fasihi simulizi ina nafasi kubwa kabisa katika jamii kwani huindama na kuifinyanga jamii katika kila pembe. Waadha ni wazi kuwa umri wake nimkongwe zaidi kwani usuli wake ni tangu jadi binadamu alipopata tu uwezo wa kuzungumza.
Tukitazama kwenye ufafanuzi wake ni kuwa wanafasihi wengi wameinukia na maana na maelezo mbalimbali kuhusiana na fasihi simulizi ingawa kipengee kinachowaunganisha ni kuwa ni aina ya fasihi ambayo ni ya ana kwa ana kupitia mdomo huku hifadhi zake zikiwa kichwani mwa binadamu.
Uainishaji wa tanzu za fasihi vile vile una changamoto zake kwa kuwa kila mwanafasihi huzichanganua kama anavyozidhania kibinafsi kwa kuwana ufinyu wa nadharia zinazochanganua tanzu hizi.
Waaidha fasihi simulizi inazo dhima zake pamoja na sifa zake bainifu katika jamii bila kusahau kuwa vipo Vikwazo mbalimbali ambavyo vinaikumba fasihi simulizi.
Hivyo basi fasihi simulizi ni mihimili katika jamii yoyote ile.

Balisidya, M. L, (1983), Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi, kutoka kwa Mulika namba 19 (1987), Taasisi ya Uchunguzi  wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mwanbusye, D (2012), Lugha, Utamaduni na Fasihi simulizi ya Kinyakyusa, Dar es Salaam.
Ngure, A (2003), Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari, Nairobi, Phoenix Publishers Ltd.
Finnegan, R. (1970), Oral Literature in Africa, Open Book Publishers, Cambridge.
TUKI, (1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Nairobi, Oxford University Press Ltd.
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Knappert, J. (1979). Four centuries of Swahili Verse. Heinemann. London.
Mayoka, J.K. (1993). Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka. Ndanda Mission Press.Tanzania.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Ushairi, Nadharia na Tahakiki. DUP. Dar-es-Salaam.
F. E. M. K. Senkoro (1982) Fasihi. Press and Publicity Centre. Dar es Salaam.
K. W. Wamitila (2004) Kichocheo cha Fasihi, Simulizi na Andishi. Focus Publications Limited: Nairobi
M.M. Mulokozi (1989) Tanzu za fasihi simulizi. Katika Mulika. Na 21
M. MsM. MSokile ( 1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. E.A.E.P. Nairobi
P.Mhando na N.Balisidya (1976) Fasihi na sanaa za maonyesho. T.P.H. Dar es Salaam
S. OSS. Okpewho (1992) African Oral Literature. Backgrounds, Character, and Continuity. Indiana University Press. U.S.A

No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...