Monday, April 13, 2020

TAMTHILIYA YA MORANI

UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA MORANI
KITABU – MORANI
MWANDISHI – E. MBOGO
WACHAPISHAJI – DUP
MWAKA – 1993
UTANGULIZI

Morani ni tamthiliya inayozungumzia juu ya matatizo yaliyoikumba nchi ya Tanzania mwaka 1980 na kusababisha hali ngumu ya uchumi kwa tabaka la chini. Matatizo haya ni kama uhujumu uchumi, wizi wa mali ya umma, ulanguzi, rushwa na kukosekana kwa haki, unafiki wa viongozi na matabaka, n.k. mwandishi wa tamthiliya hii E. Mbogo anaonesha kuwa, kukithiri huko kwa matatizo kunakwamisha maendeleo hapa nchini.

MAUDHUI

DHAMIRA KUU: UJENZI WA JAMII MPYA

Ujenzi wa jamii mpya ndiyo dhamira kuu ya tamthiliya hii ya Morani. Katika kujadili dhamira hii mwandishi anapendekeza kuwa jamii mpya itakayojengwa iwe ni jamii inayopiga vita aina yoyote ya unyonyaji, ukoloni mamboleo pamoja na wahujumu uchumi wan chi, msanii anasema (uk. 41);
“Tuandike risala itakayoamsha chuki dhidi ya ubeberu, ukoloni mamboleo, risala yenye mishale ya sumu. Sumu itakayounguza maini na mapafu ya wahujumu uchumi, mabepari uchwara na vibaraka popote walipo.”
Hapa msanii anaonesha wazi nia yake ya kupinga unyonyaji na uhujumu uchumi katika jamii itakayojengwa ili kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Vilevile msanii anapendekeza kuwa, katika jamii hiyo mpya, lazima njia kuu za kuzalisha mali zimilikiwe na umma. Msanii anasema (uk. 4);
“Tena risala hii iwakumbushe wananchi sherehe za harusi – matanga: sherehe za kutaifisha viwanda, mabenki, majumba, mashamba, hospitali na maduka kila kitu mali ya umma”
Hapa msanii anakumbusha kuwa ili umma umiliki njia hizi za uzalishaji mali ni lazima zitaifishwe toka kwa watu binafsi na ziwekwe mikononi mwa umma ambapo zitatumika kwa faida ya umma. Katika kujadili dhamira hii, mwandishi anaona kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima jamii nzima iungane kuwa kitu kimoja, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, msanii anasema (uk. 41);
“Risala itoe mwito kwa Morani wote. Morani waungane na umma. Waungane ili kuendeleza safari ya kuitafuta nguzo ya uswezi”
Pili msanii anaonesha kuwa, ili tujenge jamii lazima tujitoe muhanga. Tuwe na ujasiri na ushujaa ili tusiogope upinzani wa watu wanaonyonya. Vilevile msanii anawahimiza wanajamii kushika silaha ili, kuweza kujenga jamii mpya. Hivyo anasema (uk. 44);
“Enyi Morani nyakueni sime na ngao ili kulitetea dongo”
Dongo na Jalia ni mfano mzuri wa watu waliojitoa muhanga kupigania ujenzi wa jamii mpya. Hawa hawajali upinzani wa aina yoyote wakisaidiwa na Mapoto, Malongo na Hadikwa. Hawa wapo mstari wa mbele katika ujenzi wa jamii mpya ambayo itafutilia mbali ukoloni mamboleo na aina zote za unyonyaji (uk. 40-42).
Vilevile msanii anaitahadharisha jamii kuwa katika ujenzi wa jamii mpya kuna wasaliti wasiopenda mafanikio ya umma. Yusufu na Mlemeta ni mfano wa waliopewa jukumu la kuliongoza gurudumu la ujenzi wa jamii mpya lakini kutokana na ubinafsi pamoja na kushirikiana na wahujumu, wanakwamisha zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya.

DHAMIRA NDOGO NDOGO

KUPIGA VITA UHUJUMU UCHUMI
Ni mbinu mojawapo inayojitokeza katika Morani. Msanii anaonesha kuwa uhujumu uchumi ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya.
Katika tamyhiliya hii, msanii anaonesha kuwa wafanyabiashara wengine pamoja na viongozi wa juu ndio wahujumu, kwani wanavusha mazao ya nchi kwenda nchi za nje. Nungunungu ni mfano wa watu matajiri wahujumu uchumi wan chi. Kuhusu Nungunungu msanii anasema (uk. 12);
“Unafahamu kuwa Nungunungu anavusha kahawa na karafuu, katika nchi ya jirani kwa magendo? Ana akaunti ya fedha Uswisi, Eee”
Kutokana na hali hii, msanii anaonesha kuwa, vitendo kama hivyo vinalikosesha taifa kupata fedha ambazo zingetumika kuendeleza nchi na badala yake pesa hizo zinaingia mikononi mwa watu binafsi kwa faida yao binafsi. Kana kwamba haitoshi, Nungunungu pia anaingilia kuvusha madini nje kwa magendo kama anavyosema jalia (uk. 29);
“Ninyi ndio mnaotuvurugia nchi. Mbona husemi chochote kuhusu karafuu na Tanzanite mnayovusha nje kwa magendo? Mbona husemi lolote kuhusu madola yenu mnayolundika ughaibuni? Hata ufunike mavi kwa bakuli haitakusaidia kitu”
Msanii anaonesha kuwa uhujumu uchumi unakwamisha maendeleo, na watu wanaohujumu ni watu wa juu wala sio wa chini, msanii anasema (uk. 13);
“ Katikati hakuna wahujumu, wahujumu wako juu”
Katika harakati za kutokomeza uhujumu uchumi hapa nchini, msanii anasema kuwa lazima kampeni zianzie juu. Wahujumu wako juu halafu unakuja kwa watu wa chini msanii anasema (uk. 13);
“Hatuwezi kuacha mapapa tukavua pelege”
Haa mapapa huwakilisha watu wa tabaka la juu wanaohujumu uchumi wan chi ambao huvusha mazao nchi za jirani. Wana akaunti, mahoteli nchi za nje na kulikosesha taifa pesa. Pelege ni watu wa kawaida kama Masulupwete ambao husingiziwa kuhujumu uchumi kwa kukutwa na tenga mbili za kisanvu na dawa tatu za meno. Hivyo msanii anapendekeza kuwa vita dhidi ya wahujumu uchumi lazima vianzie kwa mapapa na sio pelege.
Uhujumu uchumi, magendo na ulanguzi vinapokithiri katika nchi husababisha kuadimika kwa bidhaa muhimu. Bidhaa zinapoadimika zile chache zinazopatikana huwa ghali sana kiasi kwamba watu wa tabaka la chini hushindwa kuzimudu na kubaki kuwa za watu wa tabaka la juu, msanii anasema (uk. 29);
“Vitu vimepanda bei chumvi, mchele, sukari, unga kila kitu. Ninyi tu mnaolalia magodoro ya manoti ndio mnaozimidu hizo bei makabwela na watoto wao wakale wapi?”
Hapa msanii anaonesha hali halisi iliyopo kwenye jamii: wakati wengine wanalalia manoti ya fedha watu wa hali ya chini wanashindwa hata pesa ya kununua chumvi kwa sababu ya bei kuwa juu. Hii inasababisha hali ngumu ya maisha kwa tabaka la chini. Hivyo kujaa vitu madukani hakusaidii lolote kutatua shida za maskini. Kwani vitu hivyo vinauzwa kwa bei ghali kiasi kwamba wanakosa hela ya kununulia, msanii anasema (uk. 41);
“Tena risala hii ieleze jinsi maisha yalivyo magumu kwa watu wa chini. Ieleze jinsi maduka yalivyojaa vitu, vitu vyenye bei ya kutisha makabwela na watoto wao wakiendelea kuandamwa na utapiamlo”
Kana kwamba haitoshi, msanii anasema fedha kidogo zinazopatikana badala ya kuendeleza uchumi zinatumika kununulia vitu vya anasa ili kuwanufaisha wenye hela kama Nungunungu (uk. 41);
Msanii anaeleza kwa masikitiko makubwa kuwa nchi yetu ni tajiri, lakini ni kutokana na kuhujumiwa na wachache ndio maana uchumi wetu uko chini ukilinganisha nan chi nyingine. Msanii anasema (uk. 41);
“Tena risala hii ieleze jinsi nchi ilivyotajiri, ardhi tele, maji, maziwa, mamilioni ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, samaki na kwamba kusingizia hali ya hewa na opeki ni uzandiki-dhambi nyekundu pyuu! Isiyofutika wala kusameheka”
Hivyo msanii anasema, ili kuijenga jamii mpya ni lazima tupige vita wahujumu uchumi wan chi. Kwa upande mwingine vita iliyoanzishwa dhidi ya uhujumu uchumi ilionekana kama ni kuwaonea wahujumu uchumi hao. Wao walifikiri kuwa vita hii imeanzishwa na wachache wenye wivu dhidi yao. Nungunungu ni mmoja wa wenye mawazo hayo kama anavyosema (29);
“Hii kampeni mmeivaa kama koti la kutungua. Akina fulani wachache wameibua hii vurugu isiyokuwa na mbele wala nyuma”
Kwa upande wa wahujumu uchumi wanaona hizi kampeni ni kama vurugu za kuwavurugia maslahi yao kama anavyosema Nungunungu (uk. 29);
“Ukifungua duka unaambiwa hujuma, mtu akinunua lori hujuma! Ukijenga kajumba ka ghorofa moja hujuma, ukiweka vielfu vichache benki hujuma. Baadaye mtasema mtu akioa wake wawili au watatu pia ni hujuma! Uyai huo! Mnataka kutuvurugia nchi”
Mawazo kama haya anayosema Nungunungu ni potofu, kwani haelezi waziwazi hizo pesa kapata wapi, labda tungekubaliana naye. Katika Morani msanii anasema ili kuijenga jamii mpya lazima tupige vita wahujumu uchumi, kwani wanakwamisha zoezi hilo.

KUPIGA VITA UNAFIKI NA USALITI
Unafiki ni hali ya mtu kutokuwa mkweli au kujifanya mkweli huku sivyo. Katika tamthiliya hii ya Morani mtunzi anaonesha wazi kuwa zoezi la kupambana na uhujumu uchumi wa nchi halitafanikiwa iwapo wanaoendesha zoezi hilo watasalitiana na kuwa wanafiki miongoni mwao. Yusufu na Mlemeta ni mfano wa watu wanaokwamisha suala hili. Hii ni kwa sababu wanakubali kununuliwa na Nungunungu kama anavyosema Jalia (uk. 13);
“Mlemeta kama wewe umenunuliwa sio mimi”
Kutokana na kununuliwa huko wanashindwa kumweka Nungunungu kwenye orodha ya wahujumu uchumi na hivyo kukwamisha zoezi zima. Licha ya hayo Yusufu na Mlemeta wako mstari wa mbele kutetea hujuma. Wanawazuia askari ili wasimkamate Nungunungu. Mlemeta anasema (uk. 23);
“Na wewe mzee umeponea chupuchupu kama tusingetumia mbinu ya kuzuia askari wa Jalia, basi saa hii tungekuwa tunazungumza hadithi nyingine”
Wakati wahujumu wengi wamekamatwa na mali zao kufilisiwa, Nungunungu analindwa na watekelezaji wa kampeni hiyo. Kana kwamba hiyo haitoshi, Mlemeta na Yusufu wamepewa jukumu la kumtafutia Nungunungu wakili pindi akamatwapo, kama msanii anavyosema (uk. 24);
“Nungunungu: “itabidi mwende mkamwone…..advocate mpange kila kitu tayari. Lazima ahakikishe nikiwekwa ndani, nishinde kesi”
Mlemeta: “Sawa mzee”
Kutokana na Yusufu na Mlemeta kutetea hujuma, wanakwamisha zoezi la ujenzi wa jamii mpya na ili tujenge jamii mpya lazima tuwaondoe watu kama hao. Msanii hakuishia hapo anasema pia utaona wanaopinga maendeleo ya nchi ndio kwanza wanapandishwa vyeo na kuwa mabalozi Uchina, na kuwa mkuu wa jimbo. Hapo msanii anakejeli tabia ya nchi yetu kuwapandisha vyeo watenda maovu na kuwaacha wale wanaotimiza vyema wajibu wao (uk. 37).

KUPIGA VITA MATABAKA
Katika kujadili dhamira hii, msanii anaonesha matabaka ya aina mbili. Kwanza kuna tabaka la juu la wenye pesa. Tabaka hili humiliki njia zote kuu za uzalishaji mali, vyombo vya dola, ili kulinda maslahi yao (uk. 27, 30). Wana mapesa na vitega uchumi nchi za nje (uk. 12). Pia tabaka hili hupata huduma muhimu kama matibabu, bila matatizo yoyote (uk. 38). Msanii anaonesha kuwa tabaka hili pia hupendelewa hata kwenye sharia pindi wanaposhitakiwa kwa makosa mbalimbali. Kwa uthibitisho mwandishi anaonesha kesi ya Nungunungu (uk. 34);
“Basi unajua yule Jaji alifungua mbuku wake mweusi wa sharia akasoma……kamati na mahakama imechunguza na kuona kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa ndugu Nungunungu amejihusisha na biashara haramu. Mahakama inaridhika na bila mashaka kuwa ushahidi uliotolewa dhidi ya Nungunungu ni majungu matupu yenye nia ya kumpaka matope. Hivyo mahakama inamuachilia Nungunungu huru”
Kwa upande mwingine takaba hili wapo mstari wa mbele kufanya biashara haramu inayohujumu uchumi wa nchi.
Tabaka la pili ni la chini, kwanza maisha yao ni duni ukilinganisha na tabaka la juu (uk. 41). Hufanyishwa kazi ngumu na tabaka la juu yaani mizuke (uk. 2) na pia hunyanyaswa na vyombo vya sharia kama vile mahakama ukilinganisha na tabaka la juu. Msanii anasema (uk. 35);
“Juzi juzi kasimama Misulupwete, yule mbele ya mahakama. Hakimu wala hakujisumbua kufungua ule mbuku wake wa sharia. Hakupoteza muda. Aliegesha miwani yake katika ncha ya pua jicho kali la hakimu lilimtambaa kabwela toka vidoleni hadi utosini. Mvua saba, kazi ngumu!….Mvua saba!! Muhujumu uchumi mkubwa! Eti kakutwa nyumbani kwake na tenga mbili za kisamvu na dawa tatu za kolgeti. Dawa tu za mswaki. Maskini haokoti, akiokota – mwizi”
Msanii anaonesha jinsi vyombo vya sheria vinavyowatendea watu wa tabaka la chini kutokana na kutokuwa na sauti yoyote katika jamii. Tabaka hili linanyonywa, linanyanyaswa, linaonewa na kugandamizwa. Ili kujenga jamii mpya ni lazima kuondoa matabaka haya katika jamii.

KUJITOA MCHANGA
Msanii anaonesha kuwa, ili tujenge jamii mpya ni lazima tujitoe muhanga katika kuondoa unyonyaji na uonevu wa kila aina. Dongo, Jalia, Mapoto, Malongo na Hadikwa ni mfano mzuri wa wahusika walio mstarri wa mbele katika kupiga vita hujuma. Mzee, Malongo na Mapoto walijitoa muhanga kwa safari ya mbali kuitafuta nguzo ya uswezi, ingawa safari yao ilikuwa ya shida sana lakini hawakukata tama (uk. 7-8).
Pia Jalia alionesha ujasiri bila woga kwenda kwa Nungunungu kumpiga (uk. 28-30) na kuongoza harakati za kupiga vita hujuma (uk. 40-45). Pia aliwakemea Yusufu na Mlemeta kuwa wamenunuliwa na Nungunungu bila woga, hata walipotaka kumpiga, alimpiga Yusufu na wala hakujali lolote (uk. 12-14).
Kwa upande mwingine, tunamuona Dongo akipambana na wahujumu ili kuwaendeleza na kuwasaidia wanyonyaji bila kuogopa kitu chochote. Na ni kutokana na msimamo wake wa kutotetereka anauawa na wahujumu (uk. 43-45). Ili kuijenga jamii mpya lazima tuwe na ujasiri.

KUWA NA UMOJA NA MSHIKAMANO
Katika Morani msanii anaonesha kuwa, ili kuipata jamii mpya lazima pawepo umoja na mshikamano kwani huipa jamii nguvu na kinyume chake ni udhaifu. Msanii anawahimiza Morani wote waungane ili waweze kupiga vita hujuma nchini. Msanii anasema (uk. 41);
“Morani waungane na umma. Waungane kuendeleza kutafuta nguzo ya uswezi”
Pia katika kauli mbalimbali za Dongo naye anawahimiza Morani ili kupiga vita hujuma. Ni kutokana na utengano uliokuwepo katika jamii ndio maana zoezi la kupiga vita wahujumu linashindwa na matokeo yake kushindwa kujenga jamii mpya.
Mfano mzuri unaonekana kupitia Yusufu na Mlemeta waliokuwa viongozi wa kusimamia zoezi zima likakosa mshikamano miongoni mwa watekelezaji (uk. 8-25). Msanii anapendekeza kuwa ili tuijenge jamii mpya lazima umoja na mshikamano viwepo, kwani bila hivyo hatuwezi kufanikisha zoezi hilo.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Katika Morani mwandishi anaonesha nafasi ya mwanamke katika pande mbili, kwanza kama mwanamapinduzi aliye mstari wa mbele katika kupiga vita hujuma. Jalia ni mfano wa wanawake wanamapinduzi katika kutokomeza hujuma akishirikiana na Dongo, Mapoto, Malongo na Hadikwa (uk. 39-42).
Pia Jalia alikuwa na ujasiri wa kuwaambia waziwazi kina Mlemeta na Yusufu kuwa, wamenunuliwa na Nungunungu ndio maana wakawa wanakwamisha zoezi zima la kuwakamata wahujumu (uk. 13-18).
Vilevile Jalia ndiye aliyeongoza kikosi cha kumkamata Nungunungu aliyeogopwa na watu wote kwa ajili ya umaarufu wake. Licha ya kumkamata  alimwambia wazi madhambi yake aliyoyafanya (uk. 28-30). Kama hiyo haitoshi, Jalia alimpiga Nungunungu bila kuogopa vitisho vyake atoavyo kwa wengine tena bila wasiwasi (uk. 38). Katika kuandaa mipango ya kupinga hujuma, Jalia alifanya kazi bega kwa bega na akina Mapoto bila kujali vitisho alivyopewa na Nungunungu (uk. 40). Kwa upande mwingine mwanamke amechorwa kama chombo cha kustarehesha wanaume. Hapa tunamuona Aisha alivyokuwa akimstarehesha Nungunungu hata akajisahau na kufukuzwa shule nhatimaye kutimuliwa nyumbani kwao (uk. 26-27).

UZURUFU
Katika tamthiliya hii ya Morani msanii anajadili kwa mapana dhamira ya uzurufu. Mwandishi anaonesha jinsi wazee wanavyofanya mapenzi na watoto wadogo. Mfano mmojawapi ni Nungunungu ambaye anajiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na Aisha ambaye pia ni mwanafunzi. Kutokana na hali hiyo, Aisha anasahau hata majukumu yake ya shule na matokeo yake anafukuzwa shule. Msanii anasema (uk. 26);
Nungu: Nini Aisha!!!
Aisha: Wamenifukuza shule
Nungu: (anagutuka) Ee! Umefanyaje?
Aisha: Nakueleza mie!
Kitendo cha watu wazima kufanya mapenzi na watoto wa shule kina madhara yake kwa jamii kama inavyoonekana kwa Aisha. Madhara hayo ni kama vile kutozingatia masomo na kufukuzwa shule, kupata ujauzito na pengine kuambukizwa magonjwa ya zinaa kama UKIMWI.
Aisha alifukuzwa shule kwa sababu hakuhudhuria siku nyingi, na hakwenda shule kwa sababu ya starehe alizokuwa akipewa na Nungunungu usiku kucha. Msanii anasema (uk. 26);
Aisha: Siku nyingi sijaenda shule mie mwezi. Walimu wameleta barua  
             mzee. Wamenifuta……utanisamehe mpenzi Nungu.
Nungu: (Anamsukuma) mpumbavu mkubwa. Hutaki shule halafu
               unakuja kunililia mimi? Mpumbavu mkubwa?
Aisha: mpumbavu! Mpumbavu nini? Mimi mpumbavu? Siku zote narudi saa nane usiku nyumbani baada ya hekaheka za night – club mimi na wewe. Ulitegemea nini? Ee ?
Matukio kama haya yapo katika jamii yetu. Akina Nungunungu wako wengi na akina Aisha pia wapo wengi. Jambo la muhimu ni kupiga vita vitendo kama hivyo. Vitendo vya kurubuni watoto wa shule kwa hela zao nyingi halafu wanawaharibia maisha yao ni kinyume na maadili ya jamii. Nungunungu alimfundisha Aisha umalaya, ulevi na kuvuta sigara kitu ambacho ni kinyume na maadili ya jamii. Waswahili husema mshika mawili moja humponyoka, na ukweli Aisha alifukuzwa shule, kwani aliendekeza starehe. Starehe hizo zikamfanya asahau shule na matokeo yake akafukuzwa shule.

MIGOGORO
Mgogoro wa wahujumu uchumi na wale wapiga vita wahujumu uchumi.
Mgogoro kati ya Jalia na Mlemeta pamoja na Yusufu
Mgogoro kati ya Malongo na Yusufu kwenye baa
Mgogoro kati ya Jalia na Nungunungu
Mgogoro kati ya Aisha na Nungunungu
Mgogoro kati ya Aisha na wazazi wake

UJUMBE
Hujuma, unafiki na matabaka katika jamii ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya
Umoja na mshikamano, ujasiri na ushujaa pamoja na kujitoa muhanga ni mbinu za        ujenzi wa jamii mpya
Kikulacho ki nguoni mwako, yule anayekwamisha maendeleo ya nchi ni   mwananchi   mwenyewe – Nungunungu, Yusufu na Mlemeta
Ujenzi wa jamii mpya si lelemama
 Mapenzi na shule haviendi pamoja
Tamaa mbele mauti nyuma

FALSAFA
Mwandishi anaelekea kuamini kuwa morani (vijana) ndio wenye jukumu kubwa la kuijenga jamii mpya, hivyo wakiamua kukaa kimya na kuacha mambo yajiendee tu ndivyo jamii itakavyoharibika. Hivyo jukumu la kupambana na vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya ni la vijana wote.

MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi, kwani ameonesha waziwazi matatizo yanayoikabili jamii yake na kuweka bayana namna ya kukabiliana na matatizo hayo (uk. 27).


FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja. Mchezo unaanza kuonesha kifo cha Dongo na utata uliojitokeza kwa wananchi juu ya kifo chake. Mchezo unaendelea kwa kueleza vita dhidi ya wahujumu uchumi na matokeo yake. Mchezo umegawanyika katika sehemu nne.

MTINDO
Msanii ametumia dayalojia kama ilivyo kawaida ya tamthiliya, maelezo ya majibizano baina ya wahusika. Pia msanii ametumia nafsi zote tatu. Katika kuutajirisha mtindo msanii ametumia nyimbo katika mchezo huu (uk. 42).

MATUMIZI YA LUGHA
Lugha iliyotumika ni ya kawaida inayoeleweka kwa msomaji wa kawaida. Pia pamejitokeza misemo, methali, tamathali za semi, n.k
Misemo/Nahau
Ndumilakuwili (uk. 13)
Anatuchomea utambi (uk. 15)
Paka shume (uk. 17)
Kuwapaka watu matope (uk. 29)
Umeota meno jana (uk. 8)

Methali
Penye nia pana njia na subira yavuta heri (uk. 4)
Siri ya kaburi ajua maiti na siri ya maiti aijua kaburi
Fimbo ya mbali haiuwi nyoka (uk. 23)
 Mfuga punda fadhila hukujambia mashuzi (uk. 23)
Mwosha huoshwa (uk. 24)
Bandu bandu unataka kumaliza gogo? (uk. 31)
Usimsifu sana la sivyo tembo atalitia maji (uk. 23)
Mwenzako akinyolewa wewe tia maji (uk. 23)

Tamathali za semi
Tashibiha
Kesho tutawasambaza kama punje za mtama
Nungunungu na Mlemeta ni kama kupe na mkia wa ng’ombe
Watu wengi kama sisimizi (uk. 39)
Hii kampeni mmeivaa tu kama koti la kutungua (uk. 29)

Tashihisi
Jicho kali la hakimu lilimtambaa kabawela yule toka vidoleni hadi utosini
Jua lilipotabasamu na kutandaza mabawa yzake

Tafsida
Nikakumbatie blanketi mwenyewe ? (uk. 27)
Tutaenda umana au wasiwasi? (uk. 27)
Tanakali sauti
Uuuu! Uuuu! Dongo! Dongo jamaa……….(uk. 1)

Takriri
Mpumbavu, mpumbavu mimi? Mimi mpumbavu ? (uk. 26)
Nimekosea nimekosea niseme hivi niseme (uk. 22)
Mnachuja, mnachuja mnachuja hadi lini? Mlemeta

Mdokezo
Hallo bado tunaendelea na kazi…..mambo magumu mzee….lakini nadhani tutayamudu…..yaa saa ngapi….sawa (uk. 15)
Lakini mzee …..(uk. 18)

Taswira
Msanii ametumia lugha ya picha (uk. 2) kuna picha ya mizuka inayolima shamba la tajiri – hiyo huwakilisha tabaka la chini, watu wanaofanya kazi kubwa kwa kuwatajirisha matajiri wao wenyewe wananyonywa.
Pili kuna nguzo ya uswezi, hii inaashiria amali za azimio la Arusha. Dongo anaashiria wanamapinduzi wanaotaka kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na utamaduni. Mti uliokuwa karibu na ofisi pamoja na wachawi. Hizi zote mbili huashiria wahujumu uchumi. Morani inaashiria vijana wanaotakiwa kuungana ili kuleta mabadiliko katika jamii.

WAHUSIKA
DONGO
Huyu ndiye mhusika mkuu anayeongoza vita dhidi ya wahujumu uchumi. Dongo alikuwa mstari wa mbele katika mapambano akisaidiwa na Mapoto, Malongo, Hadikwa na Jalia. Dongo ni mfano wa viongozi wanaofaa kuigwa.

JALIA
Ni mhusika mwanamke aliyejitoa muhanga kuongoza kampeni ya kutokomeza wahujumu. Jalia aliongoza askari kumkamata Nungunungu bila woga. Pia katika maandalizi ya maandamano Jalia alishirikiana na Mapoto, Malongo na Hadikwa katika kufanikisha maandamano hayo. Vilevile alimpiga Yusufu na Nungungu bila woga wala wasiwasi. Hivyo Jalia ni mwanamke anayefaa kuigwa na jamii kutokana na matendo yake.

MAPOTO NA MALONGO
Hawa ni wahusika wadogo, walikuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa, ukoloni, ubepari na hujuma. Walishirikiana bega kwa bega na Jalia katika vita hiyo. Ni mfano mzuri wa kuigwa na watu katika jamii.

NUNGUNUNGU
Huyu anawakilisha wahujumu uchumi. Anashiriki kuvusha kahawa na karafuu nje ya nchi kwa magendo. Anamiliki hoteli Marekani na ana akaunti Uswisi. Ni mfano wa watu wanaolikosesha taifa fedha za kigeni kwa kufanya magendo nan i mfano wa watu wasiofaa kuigwa katika jamii.

YUSUFU NA MLEMETA
Hawa ni viongozi wanafiki na wasaliti walioko mstari wa mbele katika kukwamisha shughuli zote za maendeleo. Wanashirikiana na Nungunungu kuhujumu nchi. Wakati wa kampeni za kutokomeza wahujumu, wao walitetea wahujumu mfano Nungunungu, hivyo hawafai kuigwa na jamii. Wahusika wengine ni Mzee, Aisha, Dala Bonge, Okasha, n.k

MANDHARI
Mandhari yake ni ya Kitanzania kutokana na matukio yanayoelezwa katika tamthiliya hii kujitokeza wazi katika jamii ya Tanzania. Matukio haya ni kama vile hali ngumu ya maisha, hujuma na vita dhidi yake. Matukio haya ndiyo yaliyotawala Tanzania kuanzia miaka ya 1980 na kuenelea. Vilevile kuna mandhari ya nyumbani, ofisini, porini, baa, kumbi za starehe, mitaani, hospitalini, n.k

JINA LA KITABU
Kwa ujumla jina la kitabu linasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu, msanii anatoa wito kwa vijana – morani kuungana na umma katika kupiga vita hujuma nchini.

KUFAULU KWA MWANDISHI
Mwandishi amefaulu kwa kiasi kikubwa kuonesha matatizo ya jamii kama vile umaskini, hujuma, rushwa, usaliti, matabaka na unafiki wa viongozi. Pia ametoa wito kwa vijana kushirikiana katika kupiga vita matatizo hayo.

KUTOFAULU
Msanii ametumia taswira nyingi mno si rahisi kwa mtu wa elimu ya chini kupata maana zake na hivyo kushindwa kupata ujumbe uliokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...