DIWANI :WASAKATONGE
MWANDISHI: MUHAMMED SEIF KHATIBU
MCHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS
MWAKA: 2003
UTANGULIZI
Diwani ya Wasakatonge ni miongoni mwa diwani za hivi karibuni zinazotanabaisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii katika maisha yake ya kila siku. Matatizo hayo yanaonekana kuwa kama saratani isiyo na tiba. Hata hivyo, msanii ana matumaini kwamba, iwapo wananchi wa kawaida wataungana na kuamua kupambana, ni dhahiri kwamba matatizo hayo yatatoweka kabisa. Miongoni mwa matatizo hayo yataoneshwa kwenye kipengele cha maudhui huku yakishadidiwa na fani.
DHAMIRA:
Ni jumla ya maana anayovumbua mwandishi aandikapo kazi yake na jumla ya maana anayoipata msomaji pindi anapoisoma kazi fulani ya kifasihi. Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira kuu ni lile wazo kuu la mwandishi katika kazi, wakati dhamira ndogondogo ni zile dhamira zinazojitokeza ili kuipa nguvu dhamira kuu. Dhamira zilizojitokeza katika diwani hii ni kama ifuatavyo:
UONGOZI MBAYA:
Jamii nyingi za kiafrika zinakabiliwa na suala la uongozi mbaya. Wapo viongozi ambao hawataki kuachia madaraka kama ilivyooneshwa katika shairi la “MADIKTETA”
"Mizinga nayo mitutu,
Haitoi risasi,
Hutoa marais,
Walio madikteta"
Ni kweli kuwa viongozi madikteta ndio chanzo cha kukosekana kwa maendeleo katika bara la afrika.
MATABAKA
Migogoro mingi inaibuka katika jamii kati ya tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho katika kugombea mahitaji ya kila siku. Mfano katika shairi la "TONGE LA UGALI"
“Wanapigana
Wanaumizana,
Wanauwana,
Kwa tonge la ugali!”
Tunaoneshwa kuwa tabaka masikini linajaribu kupambana na tabaka la tajiri ili liweze kupata tonge la ugali.
UMASIKINI
Mshairi amejadili kwa kina kuhusu tatizo la umaskini katika shairi la WASAKATONGE anaonyesha jinsi ambavyo masikini wanavyotokwa jasho kwa sababu ya kufanya kazi ngumu zenye mishahara ya kijungujiko.
"Jua kali na wasakatonge,
Wao ni manamba,
Mashambani,
Ni wachapakazi viwandani,
Lakini bado ni masikini."
Wasakatonge wanafanya kila jitihada ili waweze kujinasua kutoka katika umasikini lakini inashindikana na jasho linaendelea kuwatoka.
MMOMONYOKO WA MAADILI
Dhamira hii imejadili katika shairi la JIWE SI MCHI. Mshairi amekemea tabia ya wanawake wanaooana wao wenyewe kana kwamba wanaume wamekwisha. Mshairi anayalaani mambo haya mapya yanaingilia taratibu na kutaka kuharibu tamaduni zetu za kiafrika
UKOLONI MAMBO LEO
Hali hii hutufanya tuwe watumwa wa ukoloni mamboleo baada ya kuondokana na ukoloni mkongwe. Katika shairi la “BUNDI” (uk.43) tunaambiwa kuwa uhuru wetu tulioupata hatujaufaidi hata kidogo kutokana na kupigwa nyundo ya kichwa na ukoloni mamboleo. Ukoloni huu ambao umefanikishwa na Bundi, tunaambiwa kuwa uko nasi kila kukicha. Ukoloni mamboleo ni mfumo usio na usawa hata kidogo. Ni mfumo ambao unawafanya wanyonge waendelee kuwa masikini, wasiomithilika huku matajiri wakiendelea kuwa watu wenye mali kupindukia. Haya yote tunayapata katika shairi la “KLABU” (uk.50) juu ya ukoloni mamboleo kwa kutuasa tuchapekazi, tujenge viwanda, tuboreshe kilimo na ufugaji, tuinue elimu, kukuza uchumi na tupige vita rushwa.
UNAFIKI:
Katika diwani hii tunaambiwa kuwa baadhi yetu hasa wanasiasa, viongozi au wananchi ni wanafiki wakubwa. Kwani kitendo cha baadhi ya watu kujiona kuwa hawana dhambi ni cha kinafiki kwa sababu, hakuna mwanadamu asiye na dhambi kama shairi la “WASO DHAMBI” (uk.1) linavyosema;
Wavilemba!
Wavilemba, na majoho, tasibihi,
Wajigamba, safi ni roho, ni kebehe,
Wanotenda,
Unafiki.
Unafiki mwingine unajionesha katika siasa ambapo baadhi ya viongozi hupata uongozi kwa kujipendekeza na kutoa maneno ya hapa na pale kwa wale wanawapatia hivyo vyeo. Haya tunayapata katika shairi la “WARAMBA NYAYO” (uk.46-47)
‘Wajikomba,
Ili kupata vyeo,
Na uluwa.”
USALITI:
Mshairi Mohammed Seif Khatibu ameonesha suala la usaliti katika diwani hii ya WASAKATONGE, kwani tunaambiwa kuwa, mara nyingi tunakuwa pamoja katika safari ya kutafuta kitu fulani lakini pindi kinapopatikana tu tunawatenga baadhi ya watafutaji wenzetu. Haya yanadhihirishwa wazi katika shairi la “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23) ambapo msanii anabainisha kwa kusema kuwa;
“Nilitoswa baharini,
Ya dharuba na tufani,
Walitaka nizame,
Wao wanitazame,
Nife maji wakiona,
Waangue na vicheko,
Na kushangilia,
Ushindi wao!”
MAPENZI/MAHABA
Kwa vile mshairi huyu anaona kuwa mapenzi ndicho kitu cha thamani kubwa kwake ayakosapo au amkosapo yule ampendaye hukonda na kudhoofika mwili kama asemavyo katika shairi la “SILI NIKASHIBA” (uk.17)
“Sili nikashiba, nikikukumbuka,
Hula haba, na kushikashika,
Ni chozi za huba, kweli nasumbuka.
UJUMBE
- Uongozi mbaya ndiyo chanzo cha kukosekana Kwa maendeleo katika Bara la afrika. Ujumbe huu unapatikana katika shairi la MADIKTETA.
- Uhusiano wa unyonyaji umesababisha matabaka na masikini ndiye anayeumia. Haya yamejadiliwa katika shairi la TONGE LA UGALI.
- Umasikini Ni tatizo sugu katika jamii. Shairi la WASAKATONGE
- Viongozi wengi hubadilika Kama vinyonga hivyo katika uchaguzi wapiga Kura wawe makini. Katika shairi la VINYONGA
MSIMAMO
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi anashauri kuwa, ili kuondoa matatizo yanayojitokeza katika jamii lazima jamii ifuate misingi ya usawa na haki.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa jamii yenye maendeleo ni ile inayofuata misingi ya haki na usawa.
FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia miundo hii:
Tathlitha
Ni muundo ambao ubeti mmoja huwa na mistari mitatu. Mfano wa mashairi yaliyotumia muundo huu ni “Nilinde”, “Tutabakia wawili”, “Itoe kauli yako”, “usiku wa kiza” na “Sikujua”.
Tarbia
Ni muundo unaotumia mistari minne. Na n i muundo unaopendwa kutumiwa na washairi wengi.Mfano wa mashairi yaliyotumia muundo huu ni “Mahaba”, “Machozi ya dhiki”, “Mcheza hawi kiwete”, “Sivui maji mafu”
Sabilia
Muundo huu hutumia zaidi ya mistari sita na kuendeleaka katika beti. Mfano ni mashairi ya “Waso dhambi”, “Sikuliwa sikuzama”, “Madikteta”, “Si wewe?”, “Vinyonga”
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo yote miwili: mtindo wa kimapokeo na mtindo wa kisasa.
Baadhi ya mashairi ya kisasa ni: “Sikujua”, “Tutabakia wawili” na “Jiwe si mchi”
Baadhi ya mashairi ya kimapokeo ni: “Mahaba”, “mcheza hawi kiwete” “Sivui maji mafu” na mengine.
MATUMIZI YA LUGHA
Vipengele vya matumizi ya lugha vinajadiliwa.
Tamathali za semi
Tashibiha
“Linanuka kama ng’onda” – “Kansa”
Sitiari
“Usijigeuze Popo” – “Itoe kauli yako” “Uchoyo ni sumu” – “Pendo tamu”
Tashihisi
“Inaumwa Afrika” – “Tiba isotibu” “Radi yenye chereko” – “Afrika” “Pendo lenye tabasamu” – “Pendo tamu”
Mubaalagha
“Pendo tamu kama letu duniani hulikuti” – “Pendo tamu”.
Mbinu nyingine za kisanaa
Takriri
Mfano “nilikesha”- “nilikesha”
“Buzi” – “Buzi lisilochunika”
Matumizi ya semi
Misemo
“mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao” – “Mcheza hawi kiwete”
UJENZI WA TASWIRA
- Vinyonga” – “viongozi wasaliti mwenye tabia ya kigeugeu” Katika shairi la VINYONGA
- Miamba”- watu wenye mamlaka/ watu wa tabaka la juu au wale wenye dhamana” katika shairi la MIAMBA
- Asali"- mwandishi ametumia taswira ya asali akiashiria uhuru uliopatikana toka kwa wakoloni. Katika shairi la ASALI LIPOTOJA
- Bundi” – wakoloni wanyonyaji” Katika shairi la BUNDI
- Jiko –mwanamke asiyejitunza na kujieheshimu yaani Malaya katika shairi la "WEWE JIKO LA SHAMBA"
- Fahali la dunia”. “Fahali la dunia” – “nchi za ulaya”
- Wasakatonge –watu wa tabaka la chini (masikini). Katika shairi la WASAKATONGE
- Tonge la ugali- malighafi katika shaili la TONGE LA UGALI
Kazi kazi kaak
ReplyDelete