Monday, April 13, 2020

RIWAYA YA VUTA N’KUVUTE


UHAKIKI WA RIWAYA YA VUTA N’KUVUTE
KITABU- VUTA N’KUVUTE
MWANDISHI – SHAFI ADAM SHAFI
WACHAPISHAJI – MKUKI NA NYOTA PUBLISHERS
MWAKA – 1999
Utangulizi
Riwaya hii inazungumzia matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu kwa sasa. Matatizo hayo ni kama vile matabaka, umaskini, ndoa za kulazimishwa, wivu katika ndoa, n.k 

MAUDHUI
DHAMIRA KUU: UKOMBOZI
Katika riwaya hii, mtunzi anajadili aina nne za ukombozi ambazo ni ukombozi wa kiutamaduni, ukombozi wa kisiasa, ukombozi wa kiuchumi na ukombozi wa kifikra. 

UKOMBOZI WA KIUTAMADUNI
Katika kujadili ukombozi wa kiutamaduni, mwandishi anaonesha kuwa baadhi ya mila na desturi zetu zinamkandamiza mwanamke. Baadhi ya mila hizo ni ile ya kumlazimisha mwanamke kuolewa na mtu asiyemtaka. Kama walivyofanya wazazi wa Yasmin kwa kumwozesha binti yao kwa nguvu kwa Bw. Raza. Yasmin hakumpenda Raza kwa sababu halikuwa chaguo lake. Hivyo, 
 msanii anaonesha kuwa ili tujikomboe kiutamaduni lazima tuachane na mila hizo. 
Pili, kuna mila ya kumweka mwanamke utawani, kama alivyofanya Shihab baada ya kumuoa Yasmin. Shihab baada ya kumuoa Yasmin alimweka utawani. Jambo hili linazorotesha maendeleo ya mwanamke, kwani badala ya kushughulika na kazi za kimaendeleo hukaa ndani tu na kusubiri kuletewa kila kitu na mwanaume. Katika kupiga vita mila hii msanii anaonesha kuwa, Yasmin alitoroka kwa shihab kwa lengo la kuonesha kuwa mila kama hizi zimepitwa na wakati na jamii haina budi kuzitupilia mbali mila hizo. 
Hivyo, msanii anaishauri jamii kuwa, ili tuweze kujikomboa kiutamaduni hatuna budi kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati zinazomnyanyasa mwanamke, kwani zinarudisha nyuma maendeleo ya jamii nzima kwa ujumla. 
Ukombozi wa kisiasa 
Hapa msanii anazungumzia harakati za wananchi wa Unguja na Pemba za kujikomboa kutoka katika minyororo ya kunyonywa, kukandamizwa, kunyanyaswa na kuonewa na wakoloni wa Kiingereza pamoja na vijibwa vyao. 
Katika kujadili hayo, msanii anaonesha wazi jinsi Denge na kundi lake wanavyojishughulisha na harakati hizo kwa kutawanya vitabu vyenye mawazo ya kijamaa, magazeti yanayopinga ukoloni na makaratasi mengine ya uchochezi dhidi ya wakoloni. Wao waliamini kuwa kwa kutumia vitabu, magazeti na makaratasi hayo, wananchi wa kawaida wangeamka na kuzijua haki zao na hatimaye kuanza kupambana na ukoloni huo. 
Katika kujadili dhamira hii ya ukombozi wa kisiasa, msanii anaonesha kuwa lazima tuwe na watu waliojitolea muhanga katika harakati hizo. Denge na kundi lake walijitoa muhanga katika kuhakikisha kuwa nchi yao inakombolewa kutoka katika mikono ya wakoloni kama asemavyo Denge (uk. 145); 
“Yasmin mimi najua unanipenda na mimi nakupenda vilevile, lakini kuna kitu kimoja napenda uelewe, kuna mapenzi na wajibu wa mtu katika jamii. Kila mtu ana wajibu fulani katika jamii na mimi wajibu wangu mkubwa ni kufanya kila niwezalo kwa kushirikiana na wenzangu ambao wengine unawajua na wengine huwajui ili kuona kwamba nchi hii inakuwa huru. Hii ni kazi ngumu ina matatizo mengi na inahitaji kujitoa muhanga na mimi ni miongoni mwa hao waliojitolea muhanga kufa, kupona, potelea mbali. Tupo wengi tuliojitolea namna hiyo, tena wengi sana, maelfu.” 
Denge na kundi lake walifuatwa sana na askari, lakini hawakuacha kueneleza harakati zao za kudai uhuru. 
Vilevile msanii anaonesha kuwa ili tujikomboe kisiasa, lazima tuwe na umoja na mshikamano, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Denge na kundi lake walishirikiana sana katika harakati zao za kupambana na wakoloni. Walishirikiana katika kutawanya vitabu, magazeti na makaratasi ya uchochezi dhidi ya ukoloni. Ingawaje mpaka mwisho wa riaya hii ukombozi wa kisiasa ulikuwa bado haujapatikana, lakini bado harakati hizo zilikuwa zinaendelea na kuna siku ukombozi utapatikana. 

UKOMBOZI WA KIUCHUMI
Katika riwaya hii, msanii annaonesha harakati za watu wa Unguja na Pemba za kujikomboa kiuchumi kutoka katika minyororo ya kunyonywa na wakoloni wa Kiingereza. Uchumi wa Zanzibar kabla ya uhuru ulikuwa mikononi mwa wazungu wachache ambao walikuwa wanamiliki njia zote za uzalishaji mali. 
Harakati za akina Denge na wenzake zililenga katika kuwakomboa Waafrika kiuchumi kwa kuchukua njia kuu za kuzalisha mali toka kwa wazungu wachache na kuziweka mikononi mwa Waafrika walio wengi. 

UKOMBOZI WA KIFIKRA
Ukombozi wa kifikra ni ile hali ya kujua na kutambua matatizo yanayoikabili jamii yako na wewe mwenyewe na kutafuta mbinu za kujinasua kutoka katika matatizo hayo. 
Kitendo cha Yasmin kuona kuwa baadhi ya mila na desturi zinamnyanyasa mwanamke na kuamua kuachana nazo, inadhihirisha wazi kuwa Yasmin alikuwa na uwezo wa kufikiri na kuona mbali. Mila hizo ni kama vile mwanamke kulazimishwa kuolewa na mtu asiyemtaka na kuwekwa utawani. 
Pili, kitendo cha Denge na kundi lake kugundua kuwa wananyonywa, wanaonewa na kukandamizwa na wakoloni ulikuwa ni ukombozi wa kifikra na ndio maana walianzisha harakati za kudai haki zao za msingi. 

DHAMIRA NDOGONDOGO 

1. MAPENZI NA NDOA
Katika kujadili dhamira hii ya mapenzi, msanii ameainisha aina mbili za mapenzi, mapenzi ya kweli na mapenzi ya pesa. Mapenzi ya kweli tunayaona kati ya Mwajuma na Yasmin. Hawa walipendana hasa ndio maana Yasmin baada ya kutoroka kwa mume wake, alikimbilia kwa Mwajuma wakaishi pamoja. Katika kuonesha hayo msanii anamwonesha Mwajuma kama mtu mwenye roho nzuri na mkarimu.
Japokuwa alikuwa mtoto wa kimaskini lakini aliamua kumsaidia rafiki yake Yasmin. Msanii anasema (uk. 22); 
“Mwajuma ijapokuwa ni mtoto wa kimaskini alikuwa na roho nzuri ya ajabu na roho nzuri yake ilichanganyikana na ukarimu usiokuwa na mfano. Alikuwa yuko tayari kumkirimu mtu chochote kidogo alichokuwa nacho. Alikuwa mwingi wa huruma na siku zote alikuwa tayari kumsaidia yeyote aliyemweleza shida zake, pindi akiwa na uwezo wa kumsaidia mtu huyo.” 
Yasmin, baada ya kumtoroka mume wake, aliishi maisha yake yote kwa Mwajuma mpaka alipoolewa na Shihab na baada ya kifo cha Shihab, Yasmin aliendelea kuishi kwa Mwajuma mpaka alipokuja kuolewa na Bukheti. 
Mapenzi mengine ya kweli ni kati ya Bukheti kwa Yasmin. Bukheti alimpenda sana Yasmin na ndiyo maana alifunga safari kutoka Mombasa kuja Unguja kwa ajili ya kumtafuta Yasmin. Msanii anaonesha hayo (uk. 41); 
“Kwa Bukheti safari ya kutoka Mombasa mpaka Unguja ni safari ndefu lakini safari hiyo ina urefu ulioje utakaomzuia yeye kukisaka kitu azizi kama pendo la Yasmin.” 
Bukheti licha ya kukataliwa na Yasmin hakukata tama, ndiyo maana baada ya kifo cha mume wake Yasmin, Bukheti alifunga tena safari kutoka Mombasa kwenda Zanzibar kubahatisha tena kwa Yasmin (uk. 230-231). Bukheti licha ya kupewa masharti; bado aliyatimiza na hatimaye akamuoa Yasmin (uk. 274-277). 
Mapenzi mengine ya kweli ni kati ya Denge na Yasmin. Hawa walipendana hasa na wote wawili walikuwa na mapenzi ya kweli kwa kila mmoja. Denge alimpenda sana Yasmin na Yasmin vilevile alikuwa anampenda sana Denge katika shida na raha (uk. 115-127), (214-219). 
Mapenzi mengine ya kweli ni kati ya Denge na kundi lake kama vile Mambo, Chande, Sukutua, Mwajuma, Hussein, Pazi, Salehe, n.k. hawa walipendana hasa na ndio maana walishirikiana katika shughuli mbalimbali. 
Kwa upande wa Mwajuma, naye alikuwa na mapenzi ya pesa. Aliwapenda watu wenye pesa na ndiyo maana alimshauri Yasmin amwache Denge na kuolewa na Shihab ambaye alikuwa na pesa (uk. 169-179). 
Kuhusu suala la mapenzi, msanii anaonesha kuwa uzuri na ubaya siyo unaoamua mtu kupenda au kupendwa, kwani kuna wazuri wanaopendwa na wasiopendwa. Pia kuna wazuri wasiojua kupenda wala kupendwa, hali kadhalika kuna wabaya wanaopendwa na wasiopendwa au wabaya wasiojua kupenda au kupendwa vilevile (uk. 88-89). 
Msanii anaendelea kusisitiza kuwa, katika suala la mapenzi ni lazima wale watu wanaohusika wapende wote, hayo ndiyo yatakuwa mapenzi ya kweli. Kama mmoja anapenda zaidi ya mwenzake hapo kunakuwa na walakini katika mapenzi hayo. 
Katika suala la ndoa, msanii anaonesha ndoa za kulazimishana na madhara yake kwa jamii. Yasmin alilazimishwa na wazazi wake kuolewa na Raza lakini ndoa yao haikudumu. Kwa ujumla Yasmin hakumpenda kabisa Raza, kwani alikuwa sawa na baba yake wa kumzaa. 
Vilevile katika suala hili, msanii anaonesha kuwa suala la ndoa lazima waachiwe wale wanaopendana na siyo maamuzi ya wazee ndio yatawale, kwani hayo ni mambo ya kizamani. Msanii anasema hivi (uk. 259); 
“Hivyo! Humtaki huyo mchumba wako! Huyu Bashiri ana mambo ya kizamani kwelikweli anataka akuchagulie mke yeye…..huyu ami yako mpuuzi hayajui mambo leo. Bashiri. Hajui kama siku hizi vijana wanatafutana wenyewe, kijana anatafuta wake. N‟do mnamwita vile siku hizi geli-friend sijui au sivyo Bukheti.” 
Hivyo anachosisitiza msanii ni uhuru katika suala zima la kuchagua mchumba. Msanii anaeleza kuwa, suala hili lisiingiliwe na wazee. 
Vilevile msanii amezungumzia suala la wivu katika ndoa. Shihab baada ya kumwoa Yasmin kutokana na wivu aliokuwa nao, alimweka utawani akafungwa kama wafungwa, msanii anayasema hayo (uk. 196-197); 
“Wakati Denge amefungwa gerezani kumbe Yasmin naye amefungwa kwa mumewe. Hakufungwa kama afungwavyo mahabusu ila yeye alikuwa ametawishwa hana tofauti na mfungwa. Alikuwa hendi harudiyumo ndani tu kama kizuka; kwa sababu ya wivu aliokuwa nao Shihab…..” 
Msanii akijadili zaidi juu ya wivu katika ndoa vilevile ameonesha madhara ya wivu. Wivu unapozidi katika ndoa kwanza ni rahisi ndoa hiyo kuvunjika. Mfano, kutokana na wivu, Shihab aliwaacha wanawake watatu na Yasmin alikuwa mke wake wan ne ambaye naye aliwekwa utawani (uk. 197). 
Pili, msanii anaonesha kuwa wivu ukizidi katika ndoa unamnyima uhuru yule anayeonewa wivu. Katika ndoa yake na Shihab, Yasmin alikosa uhuru kabisa, msanii anaonesha hayo (uk. 197) anasema; 
„Alimpa kila starehe, ila uhuru wa kutoka na starehe zake zote ziliishia ndani ya nyumba yake kubwa iliyokuwa na kila aina ya anasa ndani yake, zote asizione kitu, kutwa akawa ananing‟inia madirishani akiangalia wapiti njia na kuwahusudu jinsi walivyo huru. Alijiona kama ndege aliyefungiwa tunduni akapewa kila kitu isipokuwa uhuru wake wa kuruka hewani.” 
Ni kutokana na wivu huo ndiyo maana Yasmin alimkimbia Shihab akarudi tena Unguja kwa Denge ambaye hakuwa na wivu (uk. 207). Vilevile kifo cha Shihab kinatokana na wivu huohuo. Kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda na wivu juu yake (uk. 211), na baada ya kuona ajali ya ndege ile aliyoamini imemchukua mke wake naye alipofika nyumbani kwake alikata roho kwa kihoro (215). 
Hivyo, msanii anatahadharisha jamii kuwa wivu katika ndoa ni kitu chenye madhara. Kwa hiyo, ni lazima tuwe waangalifu katika kudumisha ndoa zetu. 
2. Mivutano 
Mvutano huu upo katika mgongano kati ya wazee na vijana. Huu mgongano unadhihirisha mifumo miwili inayotofautiana kiuchumi, kifalsafa na kimawazo kwa ujumla. 
Uwezo wa mwanaume au mwanamke kutaka amchague mtu wa kuishi naye ni jambo la kisasa ambalo miaka michache iliyopita, lilileta matatizo makubwa huku kwetu. 
Riwaya ya Vuta n‟kuvute inajadili mgongano wa namna hiyo, yaani baina ya wazazi na watoto wa kisasa akina Yasmin na Bukheti na wazazi wao. Mgongano anaouonesha katika riwaya hii unatokana na utamaduni wa kisasa na vile unavyopingana na utamaduni wa wakati uliopita. Ni mvutano wa ukale na usasa. 
Kwa hiyo, tunaziona taratibu mbalimbali za kijadi zilizochakaa. Kwa mfano, wazazi wa Yasmin kumwoza binti yao kwa mzee Raza ambaye ni sawa na baba yake wa kumzaa kwa nguvu, ni desturi za zamani ambazo zinaendelea kupigwa kumbo na wakati. Yasmin na Raza hawakulingana kabisa kiumri. Raza alikuwa mzee hasa kama anavyosema msanii (uk.10); 
“Alikuwa ni mume asiyelingana naye hata kidogo, si kwa umri wala tabia kwani wakati Yasmin ni kigoli wa miaka kumi na tano tu, mumewe Bwana Raza alikuwa zee la miaka hamsini na mbili. Wakati bwana Raza kasha zeeka, Yasmin alikuwa mtoto mbichi asiyeelewa kitu chochote” 
Yasmin alikubaliana na matakwa ya wazazi wake ili kuwaridhisha, lakini yeye mwenyewe hakuona fahari yoyote kuolewa na mzee anayeweza kumzaa (uk. 1) msanii anasema; 
“Yasmin hakupenda hata kidogo kuolewa na mume yule kwani yeye mwenyewe angelipendelea sana kupata mume kijana kama yeye mwenyewe. Alipenda kumpata mume ambaye yeyote angelimuona angelisema: “Kweli Yasmin kapata mume.” Alikuwa anatamani kupenda lakini hakumpata wa kumpenda. Yeye alitaka kijana wa makamu yake ambaye angelimuonesha pendo nay eye angelimmiminia pendo lote alilokuwa nalo moyoni mwake.” 
Kutokana na Yasmin kulazimishwa na wazazi wake, hakumpenda kabisa huyo mume wake, hata akayachukia maisha yake mwenyewe. Alitamani kufa kuliko kuendelea kuishi na bwana yule, msanii anasema (uk. 2); 
“Kutokumpenda Bwana Raza pamoja na utumishi wa kutwa dukani pale kulimfanya Yasmin ayachukie maisha ya unyumba na mumewe. Alitamani kufa kuliko kujitolea mwili wake kwa bwana yule….” 
Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Yasmin alikosa adabu kwa mume wake na baadaye alimtoroka mume wake huko Mombasa na kurudi Unguja kuanza maisha mapya. 
Kitendo cha Yasmin kumwacha mume wake kilileta mvutano mkubwa sana kati yake na wazazi wake. Kwanza mjomba wake alimfukuza (uk.18) hali kadhalika na mama yake alimfukuza na kumtenga kabisa (uk.42-43). 
Hivyo msanii anaonesha kuwa mara nyingi ndoa za kulazimishwa hazidumu na pia zinaleta mfarakano wa kifamilia kama ilivyokuwa kwa Yasmin ambaye alitukanwa matusi mengi sana na wazazi wake kama vile mwanaharamu, mhuni, na matusi mengine mengi. 
Katika riwaya hii msanii anawashauri wazee wasiwadharau watoto wao wa kisasa, kwa kufikiri kuwa ati hawaelewi wafanyayo. Watoto hawa yaani Yasmin amejitolea mhanga kuonesha kuwa katika dunia hii ya leo desturi za kizamani hazifai tena. Mtoto asichaguliwe mchumba na wazee wao bali mtoto mwenyewe. Mapenzi na mahaba ya kweli hayashindwi lakini yatashinda kila kitu katika kujitekeleza na kujikamilisha. Kabila, rangi, jadi, dini, ukoo – haya yote hayana nguvu za kutosha mbele ya mapenzi ya dhati kama anavyosema Yasmin (uk. 98); 
“……mimi Bwana Raza simtaki! Nimekubali kukosana na wazee wangu, kuhasimiana na jamaa zangu, kubughudhiwa na wote wanaonijua! Yote nimeyakubali kwa kumkataa bwana Raza. Jambo la uke na ume ni jambo la hiari jamani….” 
Kutokana na hilo, msanii anaitaka jamii kukubaliana na mabadiliko yanayokuja katika jamii, kung’ang’ania mambo yaliyopitwa na wakati ni kuleta migongano ya bure kati ya wazee na vijana wa kisasa ambao wanautaka huo uhuru. Vijana wa sasa wanataka uhuru katika suala zima la mapenzi. Sio wachaguliwe na wazazi wao tena. Vijana wa sasa wanachojali ni pendo la dhati na mahaba ya kudumu, wala wao hawajali asili zao. Haja kubwa ni tabia njema na ubinadamu usio na ubaguzi wa mambo hayo. Msanii anasisitiza hayo (uk. 170) anasema; 
“…..pendo jambo la hiari, hawawezi kunilazimisha kumpenda nisiyemtaka.” 
Anachosisitiza msanii katika dondoo hiyo ni kuwa, suala la mapenzi waachiwe wale wanaopendana na sio mila au wazee ndio waamue. Ndiyo maana baada ya Yasmin kumwacha Raza aliandamana na Denge, akamwacha akaolewa na Shihab naye akamwacha akaenda tena kwa Denge kisha akaenda kuolewa na Bukheti. Huo ndio uhuru alioutaka Uk 9 Yasmin navijana wenzake wa rika kama lake, uhuru wa kutoingiliwa katika suala la mapenzi. 

3. MATABAKA
Mtabaka ni dhamira nyingine inayojitokeza katika riwaya hii. Katika kuonesha matabaka, msanii ameyagawa kwa kufuata rangi zao. Hapa tuna Wazungu, Wahindi na Waafrika. Wazungu ni wale wakoloni wa Kiingereza kama vile Inspekta Wright na wazungu wenzake. Wahindi wanawakilishwa na akina Raza, Gulam na wengine, hawa walikuwa wafanyabiashara. Waafrika wanawakilishwa na watu wa kawaida wote kama vile Denge, Mwajuma, Mambo, Koplo Matata, Chande, Salehe, Pazi, Huseni na wengine. Hawa walikuwa watu maskini, kula yao kwa taabu, kulala kwao kwa taabu, n.k 
Kuhusiana na aina tatu hizi za matabaka, kulikuwa na ubaguzi kati ya matabaka haya. Ilikuwa si rahisi kwa Mzungu kuchanganyikana na Mwafrika na vilevile ilikuwa si rahisi kwa Mhindi kuchanganyikana na Mwafrika. Ndiyo maana baada ya Yasmin kukimbilia kwa Mwajuma, Wahindi wenzake waliona amevunja mila na miiko ya Kihindi kama asemavyo msanii (uk. 85); 
“Kwa Wahindi Yasmin alikuwa asi, aliyevunja mila na miiko yao yote kwa kuchanganyika na Waswahili.” 
Kwa upande wa makazi, Waafrika waliishi ndani ya vibanda vidogo vya uswahilini wakati Wazungu na Wahindi wanaishi kwenye marosheni na majumba ya watukufu (uk. 98). 
Vilevile kwa upande wa huduma zingine Waafrika walikwenda kwenye maduka ya mchangani na darajani ambayo yaliuza bidhaa hafifu, Wazungu na Wahindi waliingia ndani ya maduka ya Shangani na Baghani ambayo yaliuza vitu kwa bei ghali na maduka hayo yalitoa huduma za kila namna kwa hawa Wazungu na Wahindi (uk. 126). 
Kwa upande wa starehe vilevile kulikuwa na ubaguzi kati ya Waafrika, Wazungu na Wahindi. Wakati Wahindi wakistarehe Karimjee Club (uk. 130), Wazungu wao walistarehe English Club wakinywa bia za kila aina, lakini Waafrika walikunywa gongo.
Kwa ujumla, Wazungu na Wahindi walikuwa wanawanyonya, wanawaonea na kuwanyanyasa Waafrika. Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana watu hawa walianzisha harakati za kutokomeza utawala huo wa Kiingereza kwa kutawanya vitabu vyenye mawazo ya Marx na wengine wenye msimamo kama wake huko Zanzibar. 
Watu kama Denge waliamini kuwa, kwa kutumia vitabu hivyo pamoja na magazeti yenye misimamo hiyohiyo, ndiyo itakayowaamsha Waafrika ili waweze kupambana na ukoloni huo. 
Mpaka mwisho wa kitabu, ukombozi wa Waafrika ulikuwa bado haujapatikana na Waafrika wenyewe walikuwa bado hawajaelimishwa vya kutosha. Vilevile watetezi wenyewe wamefungwa gerezani. Hapa anachotaka kuonesha mtunzi ni kwamba, ukombozi si lelemama. Unahitaji umoja na mshikamano, pamoja na kujitoa muhanga. 

4. DHANA POTOFU NA DHARAU
Hii ni dhamira ingine inayojitokeza katika riwaya hii. Kwa upande wa dharau, tunaona Wazungu na Wahindi wakiwadharau Waafrika kutokana na rangi yao nyeusi. Pamoja na umaskini wao. Msanii anaonesha hayo (uk. 43) anasema; 
“Sasa sina mwingine ila mimi na Waafrika, nd‟o ndugu zangu. Na wanawadharau kwa sababu gani hasa? Wao si watu? Au kwa sababu maskini? Ikiwa wao maskini na mimi nishakuwa maskini, nakula fadhila zao, nakula fadhila za Mwajuma….” 
Wakati wa ukoloni hali hii ya kumdharau Mwafrika ilikuwa imekithiri sana katika bara hili la Afrika. Mwafrika aliwekwa katika daraja la tatu, Mhindi la pili na Mzungu daraja la kwanza. Kwa upande wa huduma Wazungu na Wahindi walipata huduma nzuri na Waafrika huduma duni. Hali hii bado inaendelea hata baada ya uhuru, Wahindi na Wazungu bado wanawadharau Waafrika. 
Kutokana na dharau waliyonayo Wazungu kwa Waafrika, ilikuwa si rahisi kwa Mwafrika kumwoa Mhindi au Mzungu. Hayo yanaoneshwa (uk. 251). Msanii anasema; 
“Hapana. Yeye mwenyeji wa Mombasa.” 
“Mswahili?”
“Ndiyo”
“Sasa Yasmin Bai unafikiri Gulam atakubali posa ya Mswahili” 
“Uncle mimi n‟nachotaka ni stara. Nipate mume nistirike. Akiwa Mswahili, akiwa Mhindi, akiwa Mzungu mimi kwangu ni sawasawa. Wote hao ni watu.” 
Yasmin alikuwa Mhindi lakini hakuwa na dharau kwa Waafrika. Aliona nao ni watu kama watu wengine, hivyo nao wanahitaji kuheshimiwa kama watu wengine. Katika (uk. 252) msanii anaonesha zaidi jinsi isivyo rahisi kwa mhindi na Mwafrika (Mswahili) kuonana. 
Kwa upande wa dhana potofu, kuna baadhi ya wahusika wana dhana potofu hasa Wazungu na vibaraka wao. Koplo Matata na mabwana zake wana dhana potofu juu ya mfumo wa kikomunisti na watu wake. Yeye anaamini kuwa, ukomunisti ni mfumo ambao unakanusha kuwepo kwa Mungu na dini. Vilevile kila kitu katika mfumo huu ni kugawana, msanii anasema (uk. 100); 
“Makoministi ni watu wasioamini Mungu wala dini, makafiri. Ni watu wanaoamini kugawana kila kitu, kugawana wake zao, dada zao na hata kugawana mama zao.” 
Mawazo kama haya yanayotolewa na Koplo Matata, ambaye ni kijibwa cha wakoloni, ni mawazo potofu. Wakoloni wanaupaka matope mfumo huu kwani wanajua utawaamsha watawaliwa na kudai uhuru wao. Mfumo huu unadai haki kwa kila mtu, usawa wa binadamu na mambo mengine yanayotetea maslahi ya wengi. 
Wakoloni kwa vile walitetea maslahi ya wachache waliwapiga vita sana watu waliosomea Urusi na kuanza kuwapaka matope kuwa wanaleta vurugu nchini. Katika kuhakikisha wananchi wa kawaida hawajihusishi na harakati za kudai uhuru wao, wakoloni waliwaita wanaharakati hao kama Komunisti ambao hawaamini Mungu hata dini, msanii anasema (uk. 68); 
“Sikiliza sista hawa wakoloni na vijibwa vyao ni watu wapumbavu kabisa, kwao kila mtu ni Koministi; ukidai haki yako wewe Koministi, ukisema kweli wewe Koministi. Ukipinga kutawaliwa wewe Koministi. Lolote utakalolifanya madhali halina maslahi kwao basi wewe ni Koministi. Maumau wa Kenya wameitwa makoministi. Wapigania uhuru wa Algeria wameitwa Makoministi. Kila anayedai haki kwao ni Koministi, na sumu yao kubwa wanayoitumia ya kutaka kuwatenganisha watu kama hao na wananchi wenzi wao ni kusema kwamba watu hao wanaowaita Makoministi hawaamini Mungu.” 
Haya ndiyo mawazo ya wakoloni na vijibwa vyao. Mawazo yanayochochea chuki miongoni mwa wananchi wa kawaida dhidi ya wapigania uhuru. Haya ni mawazo ambayo yamekusudiwa kusambaratisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waafrika. Ni mawazo potofu, kwani yanamdumaza mtu kifikra na hivyo hawawezi kujikomboa kutoka katika minyororo ya kugandamizwa, kunyonywa na kuonewa na ukoloni huo. 

5. UVUMILIVU NA UJASIRI
Uvumilivuna ujasiri katika maisha ni dhamira mojawapo inayojadiliwa katika riwaya hii. Kwanza, Yasmin alivumilia sana kuishi na Raza mume wake wa kwanza ambaye alikuwa mzee sawa na mzee wake wa kumzaa. Akiwa na Raza muda wote alishinda dukani, halafu kutokana na kuwa aliozeshwa kwa nguvu na wazazi wake, hivyo hakumpenda kabisa mume huyo. Uvumilivu wa jambo una kikomo chake, mwisho Yasmin alishindwa na akaamua kuondoka na kumkimbia mume wake. 
Vilevile Yasmin alimvumilia sana mume wake wa pili, Shihab. Shihab baada ya kumwoa Yasmin alimuweka utawani kwa sababu ya wivu wake. Yasmin aliyavumilia maisha hayo kama asemavyo msanii (uk. 198); 
“Taratibu Yasmin aliyazoea maisha ya utawa, akawa mke wa nyumbani aliyewekwa akakaa, akatulia na Shihab akawa anajisifu kwa rafiki zake wote.” 
Katika ndoa yake na Shihab, Yasmin muda wote alishinda ndani tu kama mahabusu, hakuwa na ruhusa ya kwenda apendako. Yasmin hakuwa na rafiki, shoga au jirani wa kuongea naye kama asemavyo msanii (uk. 211); 
“Nakuambia kaniweka ndani kama mwari, hata huyo mwari ana afadhali sina shoga, sina jirani, sina jamaa, mimi na ndani na ndani na mimi, siendi sirudi.” 
Haya ndiyo maisha aliyoishi Ya hula mbivu lakini kwa Yasmin hakuona ukweli wowote, ndiyo maana Yasmin aliomba ruhusa ya kwenda kuwaona wazazi wake na hakurudi tena kwa Shihab kama Yasmin anavyosema (uk. 214); 
“Sitorudi Abadan, sitorudi Abadan.” 
Vilevile Yasmin aliyavumilia maisha aliyoishi kwa Mwajuma baada ya kuachana na mume wake Raza na Shihab. Yalikuwa maisha magumu sana kwake lakini aliyavumilia. Mwajuma na Yasmin waliishi maisha ya dhiki na unyonge (uk. 21). Maisha yao yalitegemea rusuku kutoka kwa marafiki na wahisani wa Mwajuma (uk. 33). Lakini Yasmin aliyavumilia maisha haya yote. 
Kwa upande wa tabaka la chini, waliishi maisha magumu sana, kula kwao kulikuwa kwa tabu, kulala kwa tabu, lakini waliyavumilia maisha haya. Kwa upande wa ujasiri tunaona kuwa kitendo cha Yasmin kumkimbia mume wake wa kwanza ambaye vilevile hakumpenda, kwani alilazimishwa na wazazi wake ni kitendo cha ujasiri. Yasmin hakuona sababu kwanini aendelee kuishi na mume ambaye si chaguo lake bali la wazazi wake. 
Vilevile kitendo cha Yasmin kumkimbia Shihab, mume wake wa pili, ni cha ujasiri kwani mume yule alikuwa na wivu mno na matokeo yake ukamnyima uhuru Yasmin. Katika kutafuta uhuru huo, Yasmin alimkimbia Shihab. 
Kwa upande wa Denge na kundi lake walikuwa jasiri, ndiyo maana waliendesha propaganda za kudai uhuru nchini Zanzibar kwa kutawanya vitabu vya kijamaa na magazeti yanayopinga ukoloni. Walifuatwa sana na wakoloni hao pamoja na vijibwa vyao lakini hawakuacha kudai haki zao. Walifungwa gerezani lakini walipotoka msimamo wao ulikuwa uleule wa kutaka wakoloni waondoke nchini mwao. 
Hivyo, msanii anaonesha kuwa uvumilivu na ujasiri katika maisha ni chachu ya maendeleo katika jamii. Na watu wasipokuwa wavumilivu hukata tama haraka. Wasipokuwa jasiri huwa waoga. Matokeo yake ni kurudisha nyuma maendeleo ya jamii husika. 

6. UMOJA NA MSHIKAMANO
Umoja na mshikamano ni dhamira ingine inayojadiliwa katika riwaya hii. Msanii anaonesha kuwa, katika harakati zozote za kudai uhuru, umoja na mshikamano ni kitu muhimu sana. 
Denge na kundi lake yaani Mambo, Chande, Zanga, Salehe, Pazi, Huseni na wengine walishirikiana sana katika harakati za kuutishia utawala wa kikoloni nchini Zanzibar, walishirikiana kwa kugawa vitabu vya akina Marx, magazeti pamoja na makaratasi mengine yaliyochapwa maalumu kwa kupinga ukoloni Zanzibar. 
Vilevile tunaona wafanyakazi wa Unguja walivyoonesha mshikamano na umoja wao katika maandamano yaliyofanyika tarehe mosi Mei. Katika maandamano hayo, wafanyakazi walikuwa wengi sana na walibeba mabango na vitambaa vilivyoandikwa maneno ya kuhimiza kuungana kwa wafanyakazi na kuulaani ukoloni (uk. 139). 
Katika kuhakikisha kuwa Denge anatolewa gerezani, Mambo, Yasmin, Mwajuma na Bukheti walishirikiana sana pamoja na Sukutua. Kutokana na ushirikiano huo waliweza kumtorosha Denge kutoka Unguja na kumpeleka Kenya ili kukwepa mkono wa serikali ya wakoloni (uk. 272-274). 
Vilevile Mwajuma na Yasmin walikuwa na umoja na mshikamano wa hali ya juu sana katika maisha yao yote. Yasmin baada ya kwenda kuishi kwa Mwajuma walishirikiana katika taabu na raha bila ubaguzi wowote kati yao. 

7. USALITI 
Usaliti ni dhamira nyingine inayojadiliwa na mwandishi katika riwaya hii. Katika kujadili dhamira hii, msanii ameonesha jinsi Yasmin alivyowasaliti wazazi wake kwa kumwacha mume wake Raza, na matokeo yake ni kutengwa na jamaa zake. Yasmin hakumpenda kabisa Raza kwa sababu hakuwa chaguo lake, bali alilazimishwa na wazazi wake kuolewa naye na hatimaye akamwacha. Huu ni usaliti mzuri kwani hapa msanii anaitahadharisha jamii kuwa si vizuri kumlazimisha mtoto wako kuolewa na mtu asiyemtaka. 
Usaliti mwingine ni ule wa Yasmin kwa Koplo Matata na wakubwa wake (Wazungu). Koplo Matata alimweka Yasmin amchunguze Denge pamoja na mienendo yake yote na alitakiwa kutoa taarifa zake polisi  Uk 15 lakini badala ya kufanya kazi hiyo kwa siri alimwambia yote Denge (uk. 145-148). Kwa hiyo taarifa zote alizozipeleka Yasmin polisi zilipikwa na Denge makusudi. Kama hiyo baada ya Yasmi kupewa karatasi za kwenda kupeleka kwa Denge kwa siri ili ziwe kidhibiti cha kumtia hatiani Yasmin alimkabidhi Denge karatasi hizo kama asemavyo (uk.154); 
“Waliingia ndani na baada ya kuingia tu, Yasmin alimkabidhi Denge yale makaratasi. “Koplo Matata kanambia niyalete kwako, lakini wewe usijue kama nimeyaleta.” 
Usaliti wa Yasmin kwa Koplo Matata ni usaliti mzuri kwani aliwaonesha wakoloni na vijibwa vyao kuwa hakuna hata mtu mmoja katika nchi ile anayekubaliana na matendo yao. Vilevile aliwajulisha kuwa katika harakati hizo Denge hayupo peke yake bali kuna wengine pia, hivyo huo ni usaliti mzuri. Ni kutokana na usaliti huo ndio maana Koplo Matata akafukuzwa kazi (uk. 161). 
Usaliti mwingine ni wa Askari jela aliyewasaidia kina Mambo na Yasmin kumtorosha Denge jela (uk. 143). Askari yule alikiuka maadili ya kazi yake kwa kuwasaliti wakoloni na vibaraka wao na kuanza kushirikiana na wapigania uhuru ambao walikuwa wakisakwa kila kona ya nchi (uk. 245); 
“Unamjua Yasmin?” aliuliza yule askari. Denge alinyamaza kimya, hakumjibu kitu, usiwe na wasiwasi mimi mwenzako, najua mnataka nini.” 
Kwa upande wa wakoloni, huu ni usaliti mbaya lakini kwa wapigania uhuru huu ni usaliti mzuri, kwani inaonesha kuwa hata walinzi wa utawala huo wa kikoloni nao wamechoka kutawaliwa na kunyanyaswa na ukoloni huo, ndiyo maana wanamua kuwasaidia wapigania uhuru. Kama alivyofanya askari huyu kwa kusaidia kumtorosha Denge gerezani. 
Kwa upande mwingine, watu kama Koplo Matata na askari wengine wa kiafrika waliomtumikia mkoloni. Hawa ni wasaliti wa Waafrika wenzao, kwani walisaidiana na wakoloni katika kuwakandamiza na kuwaonea wananchi wa kawaida. Hawa walikuwa vijibwa vya wakoloni na walitumiwa na wakoloni kwa lengo la kutimiza malengo yao, ambayo ni kinyume kabisa na mahitaji ya wananchi wa kawaida. Akina Koplo Matata walikuwa vibaraka wa wakoloni hao kwani walikuwa wanalipwa kutokana na kazi zao hizo. Hivyo msanii anaitahadharisha jamii kuwa suala la ukombozi si lelemama, lazima tuwe macho na wasaliti. 

8. NAFASI YA MWANAMKE
Katika riwaya hii, mwanamke amechorwa katika nafasi mbalimbali. Kwanza mwanamke amechorwa kama kiumbe duni asiye na maamuzi yoyote katika jamii. Mfano mzuri ni pale Yasmin anapolazimishwa na wazazi wake kuolewa na mtu asiyemtaka (uk. 1). Hili linaonesha kuwa mwanamke ni kiumbe duni ambaye hana maamuzi yoyote katika jamii. 
Vilevile Yasmin kuwekwa utawani na Shihab inaonesha uduni wa mwanamke katika jamii. Shihab baada ya kumuoa Yasmin alimuweka utawani, kila wakati akawa anafungwa ndani na hivyo kukosa uhuru aliotakiwa kuupata (uk. 197). 
Pili, mwanamke amechorwa kama mwanamapinduzi ambaye hataki kung’ang’ania mila na desturi zilizopitwa na wakati. Mfano ni Yasmin kwenda kutafuta uhuru wake baada ya kumkimbia Raza. Vilevile tunamuona Yasmin akimwacha Shihab ambaye alimuweka utawani baada ya kumuoa na kwenda kwa Denge na kuishi naye. Huu wote ni uwanamapinduzi alioonesha Yasmin katika riwaya hii. 
Tatu, mwanamke anaoneshwa kama mtu mpole na mwenye huruma. Mfano mzuri ni Mwajuma ambaye alimsaidia sana Yasmin baada ya kumuacha mume wake Raza. Mwajuma alimchukua Yasmin na akaanza kuishi naye katika hali yake ya umaskini, wakasaidiana katika shida na raha. 
Nne, mwanamke anaoneshwa kama chombo cha starehe. Mfano ni Mwajuma na Yasmin. Yasmin alikuwa akimstarehesha Denge na Mwajuma kwa Mambo. 

UJUMBE
1. Suala la mapenzi waachiwe wale wanaopendana na sio wazazi kuwalazimisha watoto na uhuru huo lazima uwe na mipaka yake. 
2. Mila na desturi zilizopitwa na wakati katika jamii hazina budi kutupiliwa mbali k3. Uvumilivu, ujasiri, umoja na mshikamano ni mbinu muhimu za kujikomboa 
4. Ubaguzi wa rangi katika jamii ni kikwazo cha ujenzi wa jamii 
5. Ushauri ni kitu muhimu, lakini lazima kuwe na mipaka yake 
6. Ukweli humuweka mtu huru 

MIGOGORO 
a) Yasmin v/s wazazi wake 
b) Yasmin v/s Raza 
c) Yasmin v/s Denge 
d) Denge v/s serikali 
e) Yasmin v/s Mwajuma 
f) Yasmin v/s Koplo Matata 

MSIMAMO
Mwandishi anaonesha msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha wazi kuwa jamii yetu ina baadhi ya mila na desturi zilizopitwa na wakati, hivyo jamii lazima izifutilie mbali. 

FALSAFA 
Mtunzi anaelekea kuamini kuwa mapenzi ya kweli yatapatikana katika jamii ikiwa kutakuwa na uhuru wa kuchagua yule unayemtaka, badala ya kulazimishwa na wazazi. 

FANI

MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja. Anaanza masimulizi yake kwa kuelezea ndoa ya Raza na Yasmin, Yasmin kumwacha Raza, Yasmin kwa Mwajuma, Yasmin kuolewa na Shihab na mwisho ndoa ya Yasmin na Bukheti. 

MTINDO
Mwandishi ametumia mtindo wa monolojia (masimulizi) kwa kiasi kikubwa ingawa pia kumejitokeza dayalojia. Katika kuukamilisha mtindo wake msanii pia ametumia barua (uk. 168), nyimbo (uk. 85-86). Pia nafsi zote tatu zimetumika. 
Matumizi ya lugha 
Mwandishi ametumia lugha rahisi inayoeleweka hata kwa msomaji wa kawaida, pamoja na misema, methali,tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa. 

Misemo/Nahau 
a) Kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa (uk. 205) 
b) Hujui kama mkono wa serikali ni mrefu (uk.71) 
c) Wacha kutia chumvi (uk. 54) 
d) Hana mbele wala nyuma (43) 
e) Alipiga moyo konde (uk. 42) 
f) Kuna dansa la kukata na shoka (uk.35) 
g) Maji yamezidi unga (uk. 15) 
Methali 
a) Asiyekubali kushindwa si mshindani (uk. 271) 
b) Mwangaza mbili moja humponyoka (uk. 230) 
c) Mzoea punda hapandi farasi (uk. 207) 
d) Heri nusu shari kuliko shari kamili (uk.42) 
Tamathali za semi 
Tashibiha 
1. Bwana Raza amekaa juu ya kiti amevimba kama kiboko (uk. 9) 
2. Kijana yule aliyekuwa na macho makali kama kurunzi (uk. 13) 
3. Ametoa macho kama chui (uk. 31) 
4. Yeye na ndani na ndani nay eye kama mwari (uk. 33) 
5. Mweupe kama mgonjwa wa safura (uk. 82) 
Tashihisi 
1. Chumbani mle watu wakaanza, hawaonani na mbu wakaanza kujiandaa kwa karamu yao (uk. 194) 
2. Nuru ya jua iliingia kwa hamaki chumbani mle na ilikashifu uchafu wote wa chumba kile (uk. 49) 
Tabaini 
1. Mabinti waliolelewa wakaleleka, waliofunzwa wakafunzika, waliotunzwa wakajitunza (uk. 85) 
2. Hatua si hatua, mseto si mseto, ugali si ugali (193) 
3. Sina shoga, sina jirani, sina jamaa, mimi na ndani na ndani na mimi, sirudi sirudi (uk. 211)
Mbinu nyingine za kisanaa 
Takriri 
1. Yeye hakuona isipokuwa Yasmin, Yasmin, Yasmin gani naye? (uk. 84) 
2. Haweshi, ingia toka na kila wakija Denge, Denge na umewakosea nini hasa? (uk. 86) 
3. Haya tunywe, tunywe kwa afya ya mgeni wetu (uk. 26) 
Mjalizo 
1. Raha ya kuwa karibu naye wakaongea, wakacheka, wakafurahi (uk. 14) 
2. Kula mkate wa ufuta, mkate wa maji, mkate wa mayai (uk. 80) 
Mdokezo 
1. Naona siku hizi…….(uk. 15) 
2. Unani…..(uk. 16) 
3. Mbona unaogopa dada, unafikiri si……(uk. 25) 
4. Halafu kanigaia shilingi ishirini na ……..(uk. 67) 
Tanakali sauti (Onomatopea) 
1. Oooooh, Yasmin alijilaza kitandani akapumua kwa machofu ya safari aliyokwenda (uk. 44) 
2. Ngo, ngo, ngo, aligonga mlango (uk. 8) 
Matumizi ya Kiingereza 
1. Passing showa (uk. 17) 
2. Brother, you fool (uk. 31) 
3. Come on (uk. 32) 

WAHUSIKA

YASMIN
Huyu ndiye mhusika mkuu katika riwaya hii. Yasmin alikuwa na kijuso kidogo, macho makubwa, pua ndogo na nyembamba, alikuwa na nywele nyingi. Vilevile alikuwa si mrefi lakini hakuwa mfupi. 
Kwa tabia Yasmin alikuwa mwanamke aliyekuwa akipenda mabadiliko ndiyo maana aliamua kumkikimbia mume wake wa kwanza aliyelazimishwa na wazazi wake kuolewa naye. 
Vilevile Yasmin alikuwa anapenda uhuru wa kuchagua mchumba wake yeye mwenyewe na hakupenda wivu ndiyo maana alimkimbia Shihab kutokana na wivu wake. Yasmin alikuwa mvumilivu na mtu jasiri sana. Aliyavumilia maisha magumu aliyoishi kwa Mwajuma, pamoja na vituko vyote alivyokumbana navyo. 
Wahusika wadogo 

MWAJUMA
Alikuwa na uso mwembamba uliochongoka sawasawa na macho remburembu. Alikuwa mrefu wa wastani. Mwajuma alikuwa mpole, mkarimu na mwenye roho nzuri, na alikuwa tayari kumsaidia mtu chochote kidogo alichokuwa nacho. Vilevile alikuwa na huruma sana kwa Yasmin. 
Kadhalika alikuwa ni msichana asiyependa kujikera nafsi yake na aliutumia uhuru wake wa maisha kama alivyopenda. Alikuwa tayari kufanya lolote lile ambalo alihisi litamletea furaha bila ya kujali wengine watasema nini. Vilevile alikuwa mwanachama wa chama cha “Cheusi dawa”, kikundi cha taarabu. Kutokana na huruma, upole na ukarimu wake Mwajuma anafaa kuigwa na jamii. 

DENGE
Alikuwa mrefu wa futi sita, mwembamba na mkakamavu. Umbile lake ni la rangi ya maji ya kunde, pua yake ilikuwa ya wastani. Denge alikuwa mwanaharakati wa kupinga utawala wa Mwingereza kisiwani Unguja na Pemba. Katika harakati zake alisambaza vitabu vya Karl Marx, magazeti yanayopinga ukoloni, pamoja na makaratasi ya uchochezi dhidi ya ukoloni. 
Denge ni mfano mzuri wa vijana ambao wako mstari wa mbele katika harakati za kupambana na ukoloni hapa nchini, hivyo ni mfano mzuri wa kuigwa. 
Wahusika wengine katika riwaya hii ni Koplo Matata, Chande, Sukutua, Raza, Salehe, Inspekta Wright, Shihab, Bukheti, n.k 

MANDHARI
Riwaya hii imetumia mandhari halisi ya visiwa vya Unguja, maeneo ya Tanga na Mombasa –Kenya. Lakini matukio mengi yamefanyika Unguja. Vilevile kuna mandhari ya dukani, gerezani, baharini, nyumbani, mtaani, baa, klabuni, n.k 

JINA LA KITABU
Jina la kitabu linasadifu vizuri yaliyomo ndani ya kitabu hiki. Msanii anaonesha mivutano mbalimbali katika kitabu hiki. 
Kwanza, kuna mvutano kati ya Yasmin na wazazi wake. Huu unatokana na Yasmin kumwacha mume wake Raza ambaye wazazi wake walimlazimisha aolewe naye. 
Pili, kuna mvutano kati ya Yasmin na Raza. Yasmin hakumpenda kabisa Raza, kwani kiumri Raza alikuwa ni sawa na baba yake wa kumzaa. Hivyo katika maisha yake ya ndoa na Raza wakawa na mivutano ya kila siku. 
Tatu, kuna mvutano kati ya wakoloni na vijibwa vyao na wananchi wa kawaida wakiwakilishwa na Denge, Chande, Sukutua, Mambo na wengine. Hawa wanataka uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe, wanataka uhuru wa kumiliki njia kuu za uchumi badala ya wakoloni. 
Nne, kuna mvutano kati ya Yasmin na Shihab. Huu unatokana na wivu wa kimapenzi. Shihab alikuwa na wivu sana kwa mke wake, matokeo yake akamnyima uhuru kwa kumweka utawani hatimaye Yasmin akamkimbia. 
Mwisho, kuna mivutano ya kinafsia ambayo iliwahusu wahusika wenyewe. Hawa walikuwa na migongano ya kimawazo katika vichwa vyao. Mfano ni Yasmin, Bukheti, Denge, n.k 

KUFAULU KWA MWANDISHI
Mwandishi amefaulu sana kwa kuonesha mvutano wa vijana na wazee. 
Kifani amefaulu sana hasa katika uteuzi mzuri wa lugha na ujenzi wa wahusika. Lugha ni rahisi na inayoeleweka kwa kila mtu. 

KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Suluhisho la mgogoro kati ya wakoloni na wananchi halijaoneshwa, kwani tunaona tu wapigania uhuru wanawekwa ndani na wengine wanatoroka kwenda nje ya nchi. Je, hawa watu watatumia mbinu gani katika kujikomboa? Msanii hajaonesha. 
Matumizi ya lugha ya Kiingereza ni udhaifu mwingine wa msanii, kwani mtu asiyefahamu lugha hiyo hataweza kuelewa ujumbe uliomo kwa urahisi.
Msanii hajaonesha mipaka ya uhuru unaotakiwa kwa watoto wetu. Kwa mfano, Yasmin ametumia uhuru wake wa kumchagua Shihab lakini naye ndoa yao haikudumu. Au uhuru wa Yasmin wa kuolewa na kuachika ndio uhuru unaotakiwa? Msanii hajaonesha vizuri.

No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...