Monday, April 13, 2020

Uhakiki wa ushairi

KITABU: KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI GORA HAJI
WACHAPISHAJI: TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani inayozungumziwa juu ya mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja na suala zima la ujenzi wa jamii mpya. Katika diwani hii, mwandishi ametoa maadili na maonyo mbali mbali pamoja na mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii hapa nchini.
Maudhui
DHAMIRA KUU- UJENZI WA JAMII MPYA
Mwandishi amejadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya katika kazi yake. Katika diwani hii mwandishi ameonesha vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini. Vikwazo hivyo ni kama vile uongozi mbaya, rushwa, tamaa, ukosefu wa elimu, ukoloni mamboleo, n.k.
Katika kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia  katika zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.


UONGOZI BORA
Mwandishi ameonesha kuwa Uongozi bora unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta ufanisi mzuri katika utendaji na utekelezaji wa  majukumu mbalimbali kwani  Uongozi mbaya unasababisha kushindwa kufikia malengo. Kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana jamii hufikia kufanya mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika uongozi mpya ili kuijenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi  anaongelea juu ya mapinduzi yanayofanywa na tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala.mwandishi anasema;
‘’kimbunga mji wa siyu,kilichowahi kufika,
Si kwa yule wal huyu,ilikua patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika.
 Ametumia mji wa Siyu kama kielelezo kizuri kwa jamii  yoyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi wabovu na kuleta viongozi bora. Katika mapinduzi hayo mwandishi amefafanua kuwa wengi ndio wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi la “Madanganyo”  linazungumzia jinsi uongozi mbaya unavyowadanganya wananchi, unavyowaathiri na kuwakera wananchi. Wananchi hushiriki katika shughuli za uzalishaji mali (miradi mbli mbali) lakini matunda ya jasho lao hufidiwa na wachache. Wachache hao husahau wale waliosulubika katika uzalishaji na mtokeo yake wnanchi wanaishia kuishi maisha ya taabu. Ubeti wa 6, msanii/mwandishi ansema;

“Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, Kwa mapanga Na mshoka,
Manufaa Kwa wakuu, wadogo yetu mashaka,
Wezeni kutukumbuka, mjue nasi wenzenu.”
Shairi la “Wenye Vyao Watubana” (uk 8) mwandishi amejadili namna matajiri  au vitu jinsi wanavyowagandamiza, kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote. Mwandishi anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii. Hii ni kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi hawachukui tahadhari.Ubeti wa 7, mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga, kwa lochi wa darajani,
Kujitole mhanga, kwa bei hiwezekani,
Mvao wake wa kanga, ni shilingi elifeni,
Wakubwa tuteteeni, wenye vyao watubana.”
Shairi la “Kibwangai”  linajadili dhana ya usaliti wa viongozi wetu kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi wanavyowachagua viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au wakishashika nyazfa wanageuka na  kuwasaliti wananchi waliowachagua. Msanii anathibitisha hayo kwenye ubeti wa 7;
“Kibwangai alipoona, ni mtu kakamilika,
Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya,
Wala hakujali tena, wenzake waliwambiya,
Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu.”
Shairi hili, limetumia taswira ya Kibwangai  kuwakilisha viongozi wasaliti nanyani kuwakilisha wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai yaani watawaliwa.
Katika shairi la “Hili Mnatutakiya” , mwandishi anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi ,jeshi namna  vinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na kuwashughulikia wahalifu..Ubeti wa  1msanii anasema;
Twasema kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu mkatubwaga,hasa ukiangaliya,
Hao wezi mwafuga,wazidi kutuibiya,
 Msanii ameonesha kuwa vyombo hivyo ndivyo  vinavyowalinda wezi,majambazi na matapeli.Kwa ujumla  msanii wa  diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
 KUPIGA VITA RUSHWA 
Rushwa ni kikwazo kimojawapo kinachokwamisha kujenga  jamii kwa upya. Kutokana na rushwa kuota mizizi  katika jamii haki hupotea, wachache wanafaidi matunda ya nchi  na wengine wanaendelea kuumia. Shairi la “Rushwa”   mwandishi anasema;
“Rushwa kajenga kambi, na kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi, mkaidi hashindiki,
Tumzushieni wimbi, isiwe kutahiliki,
Tumchimbie handaki, rushwa tukamzikeni.”
Katika ubeti huu, mwandishi anatuonesha kuwa lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki na usawa vitawale.Kupiga vita rushwa ni njia pekee itakayoisaidia  kujenga  jamii mpya ambayo mwandishi ameipendekeza.
 UMUHIMU WA ELIMU
 Ili tuijenge  jamii mpya ni lazima watu wapate elimu na waelimike bila kujali umri. Mwandishi anawahimiza wazee kujiunga na kisomo chenye manufaa ili wafute ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.  Mwandishi anathibitisha haya katika shairi la “Kisomo cha Maarifa”  Msanii ansema;
Kisomo chenye manufaa,tusomeni kwa haraka,
Isiwe tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
katika shairi hili mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu wazima kwa sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya maendeleo. mwandishi anaonesha kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya kwani  bila kuwa  na wasomi katika jamii kama hii yetu zoezi la ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
 KUPIGA VITA UKOLONI MAMBOLEO
Ukoloni mamboleo ni kitendo cha nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini kimaamuzi inatawaliwa na nchi nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya uchumi hapa nchini. Na ili tuweze kufanikisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini hatuna budi kupiga vita ukoloni mamboleo . Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi anaonesha jinsi ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa chini. Ukoloni mamboleo unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na kuwasetiri matajiri au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
“Ambao ni matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri, salama kujipatiya,
Walokuwa mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye Chuwi gani?
Mwandishi ameeleza kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi zinazoendelea. Hivyo mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia) hizo na tuupinge ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii mpya.
 UMUHIMU WA KUJITAWALA
Ili tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja  zote za kifikra, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “ Mwandishi anaeleza kuwa ili tuweze  kujitawala ni lazima tuepukane na unafiki, vibaraka (wasaliti),  tusikate tama na tudumishe amani.  Katika ubeti wa 3 msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe, wasio wenye kuzuzuka,
Tamaa uwakalishe, yasiwe unayotaka,
Katu wasiwawezeshe, wabakie kuzuzuka,
Katu washindike mahusuda, wasiopenda bara letu.”
Katika shairi la “Kujitawala” Mwandishi anaeleza umuhimu wa kujitawala kwa jamii yoyote ile. Mwandishi anaonesha kuwa, kujitawala ni pale umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa au kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa 1 Msanii anasema:-

“Kujitawala ni kwema, kuliko kutawaliwa,
“Kujitawala ni umma, kila yao kuamua…”
Katika shairi hili la kujitawala mwandishi anonesha faida mbalimbali za kujitawala kama vile demokrasia, kuwepo umoja naushirikiano, kuwepo haki na usawa, amani hudumishwa, vile vile mila na desturiza nchi zinadumishwa. Hivyo mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tujitawale kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra.
UMUHIMU WA KAZI NA KUWAJIBIKA
Kazi ni nguzo muhimu  sana ya ujenzi wa jamii mpya. Mwandishi amesisitiza umuhimu wa kazi na kuwajibika katika shairi la “Kazi” Mwandishi anatuonesha kuwa kzi ndio msingi wa maendeleo. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na tuepukane na uvivu. Ubeti wa 1, mwandishi anasema;-
         “Pesa huletwa na kazi, ni njia zipitiayo….”
Katika shairi la “Uokolewe”, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano ili kuuinua uchumi wetu. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa  bidii kutumia vyema  rasilimali zetu za kuinua uchumi wetu. Hivyo  msanii aniasa jamii kujihusisha na ukulima, uvuvi, utalii na viwanda ili kujenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Dumizi”  mwandishi anakemea  tabia ya baadhi ya watu kukaa bila kazi (uvivu) na kuanza  maisha ya kunyonya. Hivyo mwandishi anapiga vita unyonyajiwa watu waishio kwa jasho la wenzao.


MAPENZI NA NDOA
Katika diwani hii, mwandishi ameonesha kuwa mapenzi yamegawanyika katika pande kuu mbili ambayo Kuna mapenzi ya kweli na udanganyifu. Katika shairi la “Usimpige Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga mke wake na vile vile  mwanaume hatakiwi kumwekea mkewe masharti magumu.
Shairi la “Hongera”  mwandishi anaendelea kujadili suala la mapenzi na ndoa katika jamii zetu. Anawaonya wanandoa(bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana wawapo nyumbani. Amewapa kila mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za  (4-5) mwandishi anasema:-
“Bi arusi yangu shika, uyatie akilini.
Mumeo akifika, anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
Hongera.”
5- “Bwana arusi sikia, ukiwa kwako nyumbani,
Maneno ya kutupia, hayafai asilani,
Kauli njem tumia, na lugha iwe laini,
Hongera”
Katika shairi la “Sifa ya Mke” Msanii  anaonesha kuwa sifa kubwa ya mwanamke ni tabia na wala  si sura. Sifa ya tabia njema humpa mwanamke taadhima, huruma, utiifu na hata uhodari. Anaeleza kuwa  mwanamke anapaswa kuwa  mtulivu, asiwe kiruka njia, asiwe na ufedhuli wa aina yoyote, uovu, n.k.

Katika shairi la “Sitaki” Mwandishi anakemea mapenzi ya udanganyifu yaliyoshamiri katika jamii zetu kwa wakati huu. Anasema:-
“Rabi simpe mapenzi, hakuna wa kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi, ni wachache duniani,
Mapenzi yamepotea, sasa Ni adimu Sana,”
Ni kweli mapenzi ya siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina pamoja na udanganyifu.
MAONYO NA MAADILI MEMA KATIKA MAISHA
 Mwandishi amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu kuhusiana na harakati mbali mbali za maisha. Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni kielelezo kizuri kinachofaa kufuatwa na kizazi hiki. Maadili na maonyo haya ni ya muhimu sana katika maisha. Maadili hayo ni kama vile:-
Umuhimu wa kuwathamini wazazi , Mwandishi ameonesha kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi. Katika shairi l “Wazazi”  ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao ya mtoto; mtoto hatakiwi kuwakasirikia, kuwaudhi wala kuwachikiza bali anatakiwa kuwa na mapenzi nao. Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni kumpa chakula, mavazi, malezi mema pamoja na elimu. Katika ubeti wa 4:-
“Wakatafuta walimu, kukupatia ujuzi,
Wakakufunza elimu, pamoja na matumizi,
Sasa ni mtu timamu, waendelea na kazi,
Usiwaudhi wazazi, hiyo ndiyo yako ngao”
Katika shairi la “Ulezi Kazi” Mwandishi ameonesha jinsi mama (wazazi) wanavyohangaika kubeba mimba hatimye kuzaa na kuanza kazi ya ulezi wa mtoto hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Anaonesha kuwa wazazi hupata taabu na shida mbalimbali katika ulezi wao. Hivyo mwandishi anashauri wazazi wathaminiwe napewe heshima zote.
Kuepukana na umbea, Umbea ni ile tabia ya kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii si nzuri, kwani huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika shairi la “Wacha Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na badala yake ijishughulishe katika shughuli za uzalishaji mali. Madhara ya umbea ni kama vile majungu, uchochezi,  n.k. Umbea pia husababisha utengano. Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
“Wacha kupika majungu, na kuleta uchochezi,
Kuwajaza walimwengu, kasumba zile na hizi,
Hicho kimoja kifungu, huletesha ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi, huvunja mafanikio.”
Katika shairi la “Hayafai Mitaani”  mwandishi anaionya jamii kuwa si jambo la busara au zuri kusambaza au kupeleka taarifa ya jambo fulani sehemu ambayo haihusiki. Anaona kuwa ni busara sana endapo jambo fulani limefanyikia sehemu fulani liishie huko huko lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu isiyohusika. Si tabia nzuri kupeleka mitaani kwa watu wasiohusika. Ubeti wa 2 unasema:-


“Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani, mitaani kufikisha,
Kwani siri ya mwituni, si vyema kuelewesha,
Ya kunini huishia kunini.”
Hivyo mwandishi anatushauri kuwa jambo mojalikitendeka sehemu moja ni bora liishie katika sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
Kuepukana na udokozi (tabia ya wizi), Udokozi ni ile hali ya kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au kunyang’anya. Mwandishi anakemea tabii hii kwani  si nzuri. Tabia hii ipo miongoni mwa wanajamii. Mwandishi anaonya kuwa tabia hii huhatarisha maisha ya wahusika yaani wenye tabia hii. Mwandishi amemtumia pakakuwakilisha watu wenye tabia hiyo. Aidha mwandishi anaendelea anaelezea kuwa tabia hii husababisha uchokozi, ugomvi  pamoja na chuki katika maisha.
Umuhimu wa shukrani katika maisha, Mwandishi anaieleza jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu mwingine. Katika shiri la “Punda”  mwandishi ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo na shukrani katika maisha . Ameonesha kuwa mwandamu asiye na shukrani hata umfanyie wema kiasi gani hawezi kutoa shukrani. Ameelezea kuwa mtu asiye na shukrani ni kuachana naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa. Anasema;


“Punda hakumbuki wema, hta kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na majianufaike,
Katu hawi salama, shukrani zake mateke,
Ndiyo tabia ya punda, kurusha rusha matee,
Kuchunga akikushinda, mwacheaende zake.”
Katika ubeti huu, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa fadhila.
UJUMBE
Dhana potofu ya kudhani bila ya kuwa na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa sababu hupotosha ukweli wa mambo.
 Mapenzi na ndoa ya dhati ni muhimu katika jamii zetu
Ukoloni mamboleo, uongozi, mbaya, rushwa na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msimamo na  mwendo bora wa maisha na anatetea misingi ya haki na utu katika jamii.


MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo katika jamii kwa kudhani tu bila kuwa na misingi ya kisayansi.
FANI
MUUNDO
Mwandisha ametumia miundo tofauti katika diwani hii kma vile;Tarbia (mistari 4), Tathlitha (mistari 3) katika shairi la “Kujitawala” (uk 7-8).
    Pia ametumia muundo wa takhimisa  (sabilia) – mistari 5 na kuendelea katika shairi la “Punda” (uk 21-22), shairi la “Bahati” (uk 36).
MTINDO
Mtindo uliotumika ni ule unaofuata kanuni za mapokeo za urari wa vina na mizani pamoja na mpangilio wa beti. Karibu mashairi yote yana vina vya kati na mwisho isipokuwa katika mashairi ya “Kimbunga” (uk 1), “Dumuzi” (uk 41), “Madereva” (uk 43), “Chuwi” (uk 42) yana nusu mstari katika kituo.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja yenye mafumbo na taswira mbali mbali na tamathali za semi kidogo na misemo kwa kiasi.



TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
Kwenye shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
Ufedhuli na uovu kama yake mazoea.
Awe kama malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi ametumia mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali, machafu, matusi kw kutumia tafsida. Mfano shairi la “Nyang’au” (uk 44) linahusu tamaa, “Paka” (uk 22) linahusu wizi, shairi la “Dumuzi” (uk 41) linakemea uvivu, n.k.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
Takriri
Mwandishi ametumia takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8) neno kujitawala limerudiwarudiwa.
MATUMIZI YA TASWIRA
Mwandishi ametumia taswira nyingi kama vile;
Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi wasaliti
Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi waliosalitiwa
Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni mamboleo, n.k.
JINA LA KITABU
Jina la Kitabu Kimbunga halisadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili katika kitabu hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya kimaisha. Asilimia kubwa ya mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo na maadili katika maisha.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui, Mwandishi amefaulu; Kutoa maadili mema na maonyo katika jamii na Kujadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya. Pia Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani, Ametumia lugha rahisi, mafumbo, taswira, n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Baadhi ya maadili aliyoyajadili katika kitabu hiki ameyajadili kidhanifu, ni sawa na yale tunayoyapata makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii mpya
Vile vile amejadili masuala mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu. Kama vile maswala ya kipaji (uk 38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani, Mwandishi ametumia lahaja ya Unguja badala ya Kiswahili sanifu ivyo ni vigumu kueleweka kwa watu wote. Pia Diwani hii ni ya hali ya chini sana katika muundo, mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya kisanaa.
KITABU: FUNGATE YA UHURU
MWANDISHI: MOHAMED S. KHATIBU
WACHAPISHAJI: DUP
MWAKA: 1988
UTANGULIZI
 Fungate ni kipindi cha siku saba baada ya harusi..Ni kipindi ambacho Bwana na bibi harusi hula na kunywa tena milo ya kuchagua wakati wote wa fungate.Fedha na vifaa vitumiwavyo na maharusi huwa ni vya kuazima au kuchangiwa(si lazima viwe vyao) Wanapewa  kutoka kwa ndugu na jamaa na hata na vijana wa kuwahudumia.Wachangaji hufanya hivyo kwa sababu wanajua kuwa fungate ni ya muda mfupi(siku saba tu),hivyo huvumilia.
Fungate ni lazima iwe na kikomo.Ikizidisha kikomo hicho ibadili jina labda iitwe unyang’anyi,ulimbwende,uvivu,uzembe au jina lolote lenye kashfa hasa unafiki au usaliti.Mwandishi wa diwani hii ameimwaga ghadhabu hiyo kwa hao maharusi waliohesabu ukarimu wao kuwa ni upumbavu.
Uhuru:Uhuru ni neno linalopendwa sana na wanasiasa wa ubepari au ujamaa.Hekaheka za uhuru(kudai,kuomba au kupigania) zinaweza kufananishwa na shughuli za kutafuta mchumba,kupeleka posa kulipa mahari,na kufunga ndoa.
Katika kipindi chote cha uhuru, watu, hususani viongozi,hufurahi na kufanya sherehe ambazo huwagharimu raia-mali na vitu mbalimbali.Lakini kwa kuwa uhuru ni kitu cha thamani kama maharusi,raia hukubali kugharimia sherehe hizo.Lakini pia sherehe za uhuru kama fungate hutazamiwa iwe ya muda mfupi –labda mwezi  mmoja au miwili.
Raia wanchi zilizopata uhuru barani Afrika walikuwa na shauku ya kupata maendeleo lakini hawajafikia lengo lao hadi sasa kwa sababu viongozi wetu wanaendeleza Fungate ya Uhuru.Hivyo viongozi wanchi za Afrika wamewasaliti wananchi wao waliowachagua.Katika utangulizi mwandishi anasema ;
Nikate tama,
Kwani tuendavyo,hatufiki,
Vile ipasavyo,hayakamiliki,
Mambo yalivyo,ni unafiki,
Tumesalitiwa!
MAUDHUI
Fungate ya Uhuru ni diwani inayojdili kwa mapana sana juu ya matatizo mbalimbali yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa Tanzania.Matatizo hayo ni kama vile usaliti,unafiki,wizi,hujuma,udanganyifu,rushwa pamoja na uongozi mbaya.
DHAMIRA KUU: UJENZI WA JAMII MPYA.
Mwandishi anajadili kwa kiasi kikubwa suala la ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi anaitaka  jamii  itupilie mbali unyonyaji , uonevu, dhuruma, udanganyifu, wizi, unafiki,  umasikini, uongozi mbaya na ukandamizaji wa watu wa tabaka la chini ili kuijenga jamii kwa upya.Jamii ambayo hatamu zote za uongozi (utawala,siasa na uchumi) zitakuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi kwa misingi ya haki na usawa.
Itikadi ya kujenga jamii mpya ilijengeka juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilitangazwa mwaka 1967 baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha.Hadi 1988,mwandishi anaandika kitabu hiki anaonesha kuwa bado hatujafanikiwa kujenga jamii mpya hapa Tanzania.Hii inatokana na sababu zifuatazo;
Kwanza,bado kuna dhuruma, usaliti,unyonyaji na wizi wa mali za umma.katika  shairi la “Wingu’’  mwandishi anasema;
Bado: Wingu limetanda,Limetanda,Na kutughubika ghubi,
Mvua:Lakini hainyeshi,Hainyeshi,Ukame umetanda waa!
Mimea:Tulipanda kwa miongo, Kwa miongo,Yote imekauka!
Pia katika shairi la “Wizi”mwandishi ameonesha dhahiri kuwa wizi umo ikuluni, bomani, kanisani, misikitini, na hekaluni.Mwandishi ameonesha kuwa dini zawabariki wezi, polisi hulinda wezi, na majeshi huhalalisha wizi.katika ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Wizi umo;  Kanisani,Msikitini,Kasirini,
Na bomani,Wanyang’anywao ni waumini.
Pili, mwandishi ameonesha kuwa bado kuna matabaka katika jamii zetu.Ameonesha kuwa kuna tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho.Tabaka la juu (utawala) unaolinyonya tabaka la chini(tawaliwa).Mfano katika shairi la “Fungate” mwandishi ameonesha jinsi tabaka tawala linavyofurahia maisha kwa kuishi katika majumba mazuri, kutembelea magari ya faharin, n.k.
Katika shairi la”Waja wa Mungu”mwandishi anaonesha jinsi tabaka la chini linavyoishi kwa shida.Kwa mfano, kula kwa shida, kulala kwa shida, kuvaa kwa shida, hawapati elimu na huduma nzuri za afya.
Tatu, mwandishi ameonesha kuwa, bado kuna uongozi mbovu katika jamii zetu.Mfano katika shairi la “Viongozi wa Afrika” mwandishi anashutumu vikali viongozi wanaotumia  madaraka  yao  vibaya na kugandamiza watawaliwa.Anasema;
“Viongozi wa Afrika, Wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,Wao wachache na werevu,
Na umma wote ni mpumbavu, Wanafiki, Wazandiki”.
Pia shairi la “Njama”  mwandishi anaonesha  jinsi viongozi wanavyotumia njama mbalimbali kulinyonya tabaka tawaliwa.Viongozi wanatumia njama mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hakuna anayewapinga wala kuhoji hata kidogo.
Nne, mwandishi anaonesha kuwa, kuna unyonyaji wanaofanyiwa wakulima katika kuuza mazao yao.Ameonesha kuwa wakulima hunyonywa na kudhurumiwa na kupewa bei kidogo wakati kuuza mazao yao.Shairi la “Naona”mwandishi  linadhihirisha haya katika ubeti wa 6,ansema;
Naona Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge ulele.
Ni kutokana na matatizo hayo ya wizi, rushwa, uongozi  mbovu, dhuruma, uonevu na unyonyaji ndiyo maana tumeshindwa kujenga  jamii mpya.
Mwandishi ameonesha mbinu mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia ili  kuijenga   jamii mpya na hizo ndizo  dhamira ndogo ndogo za diwani hii kama zifuatazo;
KUWA NA UONGOZI BORA
 Uongozi mbaya ni kikwazo kikubwa katika ujenzi wa jamii mpya.Shairi la”Fungate” Mwandishi ameonesha jinsi viongozi wanavyotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyonya wananchi wa kawaida.katika ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Fungate ya uhuru, bado inaendelea,
“Harusi” wana nuru, wazuri wanavutia,
Wengi inawadhuru, na tena wanaumia
Mwandishi anaeleza kuwa tangu tupate uhuru hadi leo bado viongozi wetu wapo Fungate wakila na kunywa huku wananchi wakiendelea kuteseka na maisha magumu,hivyo mwandishi anaitaka jamii kuung’oa  uongozi mbaya na kusimika uongozi uliobora unaowajali wananchi wake .
Shairi la “Viongozi wa Afrika”mwandishi anakemea viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kujinufaisha wao wenyewe, wenye hisa katika viwanda, mabenki, makampuni au mashamba ya mabepari kuwa ni wasaliti.Anawakemea wale viongozi wenye upendeleo, wanaotumia pesa za umma kwa kuendeshea sherehe.Mwisho anawakemea viongozi wanaopokea rushwa na amewaita magaidi au mafisadi.
Shairi la “Utawala” mwandishi amehimiza kuuangusha utawala wa kibepari ambao unawanufaisha wachache na walio wengi hunyonywa, hugandamizwa, huonewa na kunyanyaswa na hao wachache.
Shairi la “Kinyang’anyiro” mwandishi anaonesha jinsi viongozi walivyokimbilia kushika madaraka (hasa enzi za uhuru) lakini wanashindwa kuleta maendeleo hapa nchini. Kwa ujumla mwandishi anapendekeza kuwa, ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora.
KUWA NA UMOJA NA USHIRIKIANO
Mwandishi anaona kuwa ili tujenge jamii mpya ni muhimu tuungane sote tuwe kitu kimoja “Katika shairi la “Unganeni” mwandishi anawataka wananchi wote wa Afrika kuungana ili kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa. Anasema:-
“Wafanyakazi wa Afrika, tuungane,
Na wakulima kadhalika, tushikamane,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa mapambano, yalo marefu,
Ushindi ni wetu”.
Mwandishi anaitaka jamii hasa tabaka la chini kuungana na kuendeleza mapambano dhidi ya viongozi wanafiki, mabepari, mamwinyi wanaonyonya, wanaonyanyasa, wanaowatesa, wanaowadhurumu na kuwagandamiza watu wa tabaka la chini.
Mwandishi katika shairi la “Nikizipata Bunduki ‘’anapendekeza matumizi ya silaha Ili kuondokana na matatizo hayo yote. Hivyo ili tujenge jamii mpya ni lazima tuungane tuwe kitu kimoja kwani  ‘’Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’’.
UJASIRI NA KUJITOA MHANGA
Mwandishi anaona ili kuijenga jamii kwa  upya ni muhimu kuwa na ujasiri,kutoogopa vitisho. Katika shairi la “Gorila” ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Gorila, jasiri!
Wa Afrika, shujaa, mshupavu, umevinjari,
Mtutu shika, mevaa, ukakamavu,uko tayari,
Gorila, ruwaza,wa kizazi kipya
Mwandishi anaitaka jamii hasa vijana kuwa majasiri na mashujaa katika harakati za kuleta mapinduzi. Pia wanamapinduzi wanatakiwa wawe wavumilivu kwa sababu ujenzi wa jamii mpya sio lelemama, ni safari ndefu.
Vile vile katika shairi la “Umma”  mwandishi anahimiza ujasiri katika kuleta mapinduzi katika jamii. Mwandishi nasema:-
“Umma,Uliovinjari, kuangamiza  mtabaka,
Hima,Uwe tayari na usiwena shaka,
Ongoza mapambano,ya wafanyakazi, hadi ushindi.
Hivyo mwandishi anaitaka jamii ijitoe mhanga ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii mpya.


KUFANYA MAGEUZI (MAPINDUZI)
Mwandishi anapendekeza mbinu ya kufanya mageuzi ili kufanikiwa katika suala zima la ujenzi wa jamii mpya. Katika shairi la “Umma” mwandishi anawaasa wanajamii wajiandae kuangamiza matabaka yaliyokithiri katika jamii.
Mwandishi anapendekeza mbinu mbalimbali za kufanya mageuzi (mapinduzi), kwanza, jamii hasa watu wa tabaka la chini waungane ii kuondoa viongozi wanaotumia madaraka waliyopewa kwa manufaa yao binafsi. Katika shairi la “Ungameni” mwandishi anasema;
Msimamo wa kitabaka,tuwekeni,
Bepari wote kuwashika,wawe ndani,
Na mamwinyi bila ya shaka,wambaroni,
Tusizubae,kazi ianze,twangoja nini?
Wakati ni huu.
Pili, mwandishi anapendekeza kutumia silaha katika mageuzi hayo ikiwa unyonyaji hautaondoka kwa amani. Mfano shairi la “Siku Itafika” na “Nikizipata Bunduki” .Pia Katika shairi la “Utawala” mwandishi anapendekeza yafanyike mgeuzi ili kuuangusha utawala unaojinufaisha na kuendeleza matabaka katika jamii. Katika shairi la “Mjamzito” mwandishi anaonesha jinsi watu wanavyoogopa harakati za mapinduzi katika jamii zetu. Katika mashairi ya “Ni vita si Lelemama” na “Maendeleo ya Umma” mwandishi anaonesha jinsi suala la mageuzi lilivyo gumu, ingawa ana matumaini kuwa umoja na ushirikiano wetu utatufanya tushinde. Pia anaamini kuwa unyonyaji na uonevu hautadumu milele, kwani kuna siku, saa, dakika na nukta itafika uovu wote utaondolewa kwa nguvu.

Katika shairi la “Joka La Mdimu” mwandishi anatoa mfano wa tawala dhalimu zilizoondolewa kwa nguvu kwa ushirikiano wa tabaka la chini. Katika shairi hili mwandishi anaonesha jinsi wananchi walivyoshirikiana katika kuutokomeza ukoloni hapa nchini. Hivyo ili nasi tufanikiwe kujenga jamii mpya hatuna budi kufanya mapinduzi (mageuzi).
KUWA NA UZALENDO KATIKA NCHI
Uzalendo ni ile hali ya kuipenda nchi kwa dhati na hata kuifia. Msimamo wa mwandishi ni kuwa hataihama nchi yake hata kwa kutishiwa njaa, maafa au umaskini. Pia ataipigania nchi yake ili iwe salama. Hivyo hata sisi hatuna budi kuipigania nchi yetu kwa hali na mali ili kuondoa udhalimu uliopo. Katika shairi la  “Nchi Yangu”  mwandishi anasema;
Naipenda nchi yangu,
Naipenda, naipenda nitakufa naipenda.
Tailinda nguvu zangu,tailinda,
Tailinda kwa maafa tailinda,
Sitakwenda kwa wenzangu,
Sitakwenda,sitakwenda hata sifa sitakwenda,
Nitakwenda hku kwangu,nitaganda,
Nitaganda kwa ulofa nitaganda.
Mwandishi anaona kuwa, tukiwa na uzalendo na nchi yetu tutafanikiwa kujenga jamii mpya, kwani usaliti wa viongozi wetu utaanguka na kila mmoja ataipenda nchi yake kwa  dhati.
KUPIGA VITA UKOLONI MAMBOLEO
Ukoloni mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bandia (kisiasa) lakini njia zote za uchumi hutawaliwa au hubaki mikononi mwa mabepari au watu wa nchi nyingine.Katika shairila “Ruya” mwandishi anasema;
Ruya,menitoa shamba,mji kuuramba niwe utumwani?
chini umwinyini,
nimo kifungoni!
Ni ‘’huru’’ machoni!
Ruya,hivyo wanitimba,kunifunga kamba,za ukoloni,
Njozi niondokee!
Mwandishi anaona kuwa wazungu ndio walioondoka katika ardhi ya Afrika lakini unyonyaji bado upon a unaendelea. Viongozi waliochukua madaraka baada ya uhuru bado wanaendeleza zile taratibu zilizoachwa na wakoloni.
Katika shairi la “Kunguru” mwandishi anaonyesha pia athari za ukoloni mamboleo hapa nchini. Katika shairi hili mwandishi anazungumzia juu ya kuondoka kwa ukoloni mamboleo. Hivyo mwandishi anaonesha kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita ukoloni mamboleo ili tuwe na uhuru wa kuamua mambo y etu wenyewe.



KUPIGA VITA WIZI WA MALIYA UMMA
Mwandihi wa diwani hii ameshindwa kuficha hasira yake dhidi ya wizi. Ameutaja wazi kuwa umo kanisani, msikitini, ikuluni na bomani. Waandishi wengi kukwepa kutaja ukweli kama huu. Asemacho mwandishi ni kwamba, sehemu zote za jamii zimeoza. Zamani watu wengi waliamini kuwa viongozi wa dini wana maadili wasiyoweza kuyakiuka. Kwa hiyo, maovu hayo yasingetokea huko. Lakini sasa viongozi hao na wale wa Ikulu wamejiunga na wahalifu. Lililo baya zaidi ni kuwapo kwa “Walinzi” wanaolinda hao wezi.. Shairi hili la “wizi” mwandishi anasema;
Wizi umo;
Kanisani,Msikitini,
Hekaluni,Wanyang’anywao ni waumini.
Kwa kifupi wizi umehalalishwa na kubarikiwa .
Mwandishi  hasemi tufanyeje  Lakini kwa mtiririko na mantiki ya mashairi yake mengine, mwandishi anashauri ufumuaji na usafishaji wa jamii nzima.Katika  shairi la“Kunguru”  mwandishi pia anajadili Suala la wizi . Japo amefumba lakini anawaelimisha wasomaji kuhusu wezi waliotimuliwa na kutawanywa. Baada ya muda wezi wakajitayarisha kwa mbinu tofauti na kuendeleza wizi wao. Mwandishi anatanabaisha raia kuhusu kuwapo kwa wezi hawa na marafiki zao. Katika shairi la “Joka la Mdimuni” mwandishi anatanabaisha watu kuhusu uwezekano wa wakoloni kurudi kwa umbo tofauti lakini kwa athari zile zile. Katika shairi la “Naona “Mwandishi anaonesha taabu wanazopata wakulima na malipo duni wanayopewa kwa mzao yao. Anamaliza Kwa msimamo huu;

”Naona Ni fukara wakulima
Wamepigwa alitima
Kwa wengine ni neema
Kwao wao ni nakama
Wamekosa haki!
KUPIGA VITA UKASUKU WA VIONGOZI WETU
Mwandishi amekemea tabia za viongozi na watendaji wengine kukubali kila lisemwalo bila kufikiri au kwa hofu tu, si nzuri. Tabia hii ya ukasuku anauita ugonjwa unaohitaji tiba (tiba yenyewe hakuitaja). Ugonjwa huu hudunisha akili. Mwandishi anaonyesha chanzo na athari zake.Katika shairi la “Ukasuku” mwandishi anasema;
“Kupea kwa ukasuku
Rais huhubiri
Wabunge hukariri
Wasomi huhariri
Na taifa husimama”  .
Mwandishi anawachunguza viongozi wa bara la Afrik na kuwaona kuwa ni mabepari, madikteta, wenye ukabila, wabadhirifu wasiojali raia wao wapenda hongo. Wote amewakemea na kuwakanya wasitende hivyo. Amewapa majina yanayowafaa- wahaini, wasaliti, majasusi n.k. Mwandishi anastahili pongezi kwa kuweza kuwakemea, badhi ya waandishi huwasifu.


UJUMBE
Uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na kukosekana kwa haki, ukasuku na matumizi mabaya ya mali ya umma ni vikwazo  ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Umoja na ushirikiano ni njia moja wapo ya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
 Mfumo wa ujamaa ni mfumo pekee utakaomkomboa mtu mnyonge, yaani ndiyo utakaoleta hali nzuri kwa wakulima au wafanyakazi.
Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na ujasiri wa kujitoa mhanga, tuwe wazalendo na nchi yetu na tufanye mapinduzi (mageuzi ya kweli) katika jamii.
Mapenzi ya kweli ni yale yasiyojali fedha au hali ya mtu.
FALSAFA
Mwandishi anatetea itikadi ya ujamaa yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Analaani wizi, dhuluma na majivuno ya kirasimu. Mwandishi angependa nchi iongozwe kwa haki na usawa. Vile vile anatetea mapenzi ya kweli katika maisha.
MSIMAMO
Mwandisi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani ameonesha matatizo mbali mbali yanayozikumba jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na dhuluma, n.k.

FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo changamano. Kuna muundo wa tathnia (mistari 2) mfano shairi la “Mjamzito” (uk 5-6), Muundo wa tathlitha (mistari mitatu) mfano shairi la “Fungate” (uk 1), “Nataka Kusema” (uk 14), Muundo wa tarbia (mistari minne) mfano shairi la “Nahodha Mtwesi” (uk 5), “Gorila” (uk 11), “Afrika” (uk 17) , “Kunguru” (uk 19), n.k.
 Vile vile ametumia muundo wa sabilia au takhimisa (mistari mitano na kuendelea) mfano mshairi ya “Utawala” (uk 21), “Ladha ya Maji Katani”(uk 27), “Joka la Mdimuni” (uk 31), “Mkata “ (uk 15) n.k.
MTINDO
Diwani hii ina mashairi yanayofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na yale yanayofuata kanuni za mashairi ya kisasa. Hii ina maana kwamba, mwandishi anayakubali mashairi ya aina mbili (kimapokeo na kisasa)
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha sanifu yenye lahaja ya Kiunguja. Lugha hii imejaa misemo mbali mbali, tamathali za semi na taswira.
MISEMO
Imetumika kwawingi.Mfano:
Nahodha mtwesi chombo chenda joshi (uk 5)
Waja wa Mungu (uk 20)
Paka shume (uk 34)
Utakiona cha mtema kuni (uk 24)
Joka la mdimuni (uk 31) n.k.
Tamathali za semi
TASHIBIHA
Mfano shairi la “Mkata” (uk 15):-
Kitandani nilalapo kama dema la samaki…
Mbu ndani kama ndege wa vitani…
Matopeni hujazika mithili nimo karoni…
Nimekoni kama ndizi natokota na kufoka
SITIARI
Mfano shairi la “Uwapi Uzuri Wako” (uk 35)
Sasa ni chano cha maji, watu wajichanyatia
Baola mkahawani, kila mtu akaliya
Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokeya.
KEJELI
Shairi la “Fungate” (uk 1) linakejeli tabia za baadhi ya viongozi wetu wanaoendelea kuifaidi Fungate ya Uhuru.
Shairi la “Kantu Sauti ya Kiza”  mwandishi anatumia nyuki kukejeli baadhi ya tabia chafu za watu.

TAFSIDA
Mwandishi ametumia Tafsida kuyasema maneno makali, machafu, matusi. Mfano shairi la “Paka Shume” linajadili suala la kumendea vitu vya watu kwa njia isiyo halali. Hata neno lenyewe fungate ni tafsida.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
TAKRIRI
Katika shairi la “Mkata” (uk 15), “Dafina” pamoja na shairi la “Nchi Yangu”
MJALIZO
Katika shairi la “Mkata” (uk 15).
MDOKEZO
Katika shairi la “Mwinyi Mpe Ndiyo”
UJENZI WA TASWIRA
Neno Fungate linaleta taswira ya ulimbwende wa maharusi au viongozi. Shairi la “Mjamzito” (uk 5) linajenga taswira ya viongozi waoga katika jamii. Viongozi wasioweza kutatua matatizo ya wananchi. Shairi la “Paka Shume”(uk 34) linajenga taswira ya udokozi. Shairi la “Viongozi wa Afrika” (uk 15) linajenga taswira ya viongozi wanaotumia madaraka vibaya.
JINA LA KITABU
Kwa ujumla jina la kitabu Fungate ya Uhuru linasadifu  yale yaliyomo ndani ya kitabu. Mwandishi ameonesha jinsi viongozi wetu walivyo kwenye fungate ya Uhuru. Hali kadhalika wananchi bado wanaendelea kugharamia sherehe mbali mbali za viongozi kwa njia ya michango kama vile kodi, mchango wa mwenge, n.k.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu Kuonesha matatizo mbali mbali ya jamii zetu na mbinu za kuyaondoa.
Kutofaulu kwa Mwandishi
Mashairi mengi kyanahusu  siasa na hivyo kuwa kama mahubiri ya kisiasa.
Kusisitiza mfumo wa chama kimoja badala ya mfumo wa mageuzi  na kitabu kiliandikwa  wakati mfumo wa mageuzi umepamba moto dunia nzima.
Kumfanyia Mwinyi kampeni ni udhaifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa Rais Mwinyi hakuweza kuondoa matatizo aliyoyajadili na ndiyo maana hadi sasa yapo.
Amekemea uongozi mbaya, lakini hakuonesha chanzo cha uongozi mbaya na mbinu mbali mbali za kuwapata viongozi bora hapa nchini.
Kutumia lahaja ya Kiunguja ni udhaifu mwingine wa mwandishi, kwani anakinyima Kiswahili sanifu uwanja wa kukua na kuenea.


UHAKIKI WA UTENZI WA MAPENZI BORA
UTANGULIZI
Mapenzi bora ni utenzi ulioandikwa na Shaaban Robert mwaka 1958.Utenzi huu una beti 700, ambazo lengo lake ni kuiadilia jamii juu ya maana, sifa, faida na hasara za kukosa mapenzi bora. Mwandishi wa kitabu hiki anasema,kusudi ni kuandalia mahitaji ya watu waliofikia fahamu ya kuwaza na kuhoji neno au kitu au tendo kwa akili ingawa haitakuwa vibaya kikisomwa na watu wowote ambao hawajafikia upeo kama huo wa kupenda, kujiweka tayari kwa zamu yao.Pia ni kwa watu ambao wana dhana kwamba,mapenzi si kitu cha maana, wanaonywa kuwa wanapata hasara kubwa kwa kupitwa bila kujua uzuri na fahari, heshima na utukufu ambao hustahili wao wenyewe. Ni kwamba wanamiliki majohari wasiyojua thamani yake. Pia anawaandikia watu wanaodai kuwa,mapenzi karaha  kuzungumzwa. Anadai wanachekesha si kidogo. Mwisho  anasisitiza kuwa mapenzi ni jambo moja katika mambo yaliyo muhimu katika wajibu wa mwanadamu.
DHAMIRA KUU
MAPENZI YALIYO BORA
Katika kuifafanua dhana ya mapenzi bora mwandishi S. Robert amefafanua,maana ya mapenzi bora, faida za kuwa na mapenzi bora pamoja na hasara za kukosa mapenzi bora.
Kwanza kabisa mtunzi ametuonesha maana ya mapenzi bora ni ipi;
Kwa mujibu wa mtunzi,mapenzi bora ni mapenzi ya kumcha Mungu,kwani ndiye Muumba wa ulimwengu na ndiye anayeamua jaala za wanadamu. Hivyo ni vyema kumpenda Mwenyezi Mungu.
Mfano katika ubeti wa 122 anaposema;
“ Tusihini walimwengu,Mapenzi tumpe Mungu,
Naye atatupa fungu, Katika wake wenezi.”
Pia mtunzi anasema kuwa mapenzi yaliyo bora ni yale ya kupendana wenyewe kwa wenyewe bila kubaguana au kwa kuangalia tofauti zetu za mambo kama vile rangi, jinsia, kabila na hali za kiuchumi.
Mfano katika ubeti wa 123 anaposema;
“Tupendane na wenyewe
Tofauti tuondoe,
Amani itushukie,
Mapenzi tufanye ngazi.”
Pia hili limedhirika katika beti za 116,117 na 118.
Katika kuelezea swala la mapenzi bora mwandishi amebainisha sifa mbalimbali za mapenzi bora kama ifuatavyo; Anasema mapenzi ni kama pambo la moyo,kwamba mapenzi bora ni jambo linaloupendeza moyo na kamwe haliishi uzuri wake. Mfano katika ubeti wa 467
“Mapenzi pambo la moyo,
Ni furaha kuwa nayo,
Mapenzi hushinda cheo,
Hata pato la ghawazi.
Mapenzi ni kitu cha thamani kubwa na endapo tukiyapoteza tutaingiwa na gharama kubwa sana kuyarudisha,Mfano katika ubeti wa 103-104 kama anavyosema;
“Wote wapige mayowe,
Mapenzi wayalilie,
Kwa kutaka yarejee,
Na kurudi hayawezi.”
“Watayataka kwa pesa,
Yawape tena fursa,
Kitu walichokifyosa,
Huwaje tena kipenzi!”
Mapenzi bora hayaambatani na aina yoyote ya chuki,na pia yenyewe ni kama dawa iondoayo chuki. Mfano katika ubeti wa 471
“Kitu hiki ni mithaki,
Kwa waelewa haki,
Mapenzi dawa ya chuki,
Kwa watu wavumilizi.”
Mapenzi bora ni kitu kisicho na kipimo,huwezi kuyapima wala kuyalinganisha na kitu chochote hata dhahabu. Mfano ubeti wa 473;
“Hushinda hata dhahabu,
Yapimwapo kwa hesabu,
Mapenzi yana ajabu,
Hayapimiki kwa wazi.”
Lakini pia katika utenzi huu ameonesha faida jamii izipatazo endapo itashikilia na kuwa na mapenzi bora;
Watu wakiwa katika mapenzi bora wote hujiona wa aina moja na hawazioni tofauti zao za mambo kama vile rangi wala hawajihisi kubaguliwa.Mfano katika ubeti wa 147
“Mapenzi wanayo mengi,
Wanadamu kila rangi,
Lakini hayawaungi,
Kwa sera ya ubaguzi.”
Kukiwa na mapenzi bora haki itatawala katika jamii na hapatakuwa na dhuluma na watu wataheshimiana.Mfano katika ubeti wa 627-631
628. “Wanadamu kwa wanyama,
Na wadudu wa kuuma,
Walisafiri salama,
Kwa imani na mapenzi.”
Mapenzi ya kweli humfanya mtu ajione kuwa hana haja ya mali wala utajiri. Anasisitiza kuwa penye dhiki na msiba marafiki huwa haba na pia mfiwa huweza hata kukosa wa kumshauri,kinachoweza kuondoa shida hii basi ni mapenzi bora tu. Mfano katika ubeti wa 271-274 Katika ubeti wa 271 anasema
“Kama mapenzi ya kweli,
Hayana haja ya mali,
Na wala hayendi mbali
Siku ya kuja majonzi.”
Mapenzi bora huondoa matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii,kama vile chuki,choyo,uchokozi,ghasia,wivu na utovu mwingine wa nidhamu. Kwamba katika ulimwengu huu uliojaa ghasia mapenzi bora ndiyo kimbilio. Mfano katika ubeti wa 66
“Ulimwengu kama huu,
Wenye mashaka makuu,
Kimbilio na nafuu,
Ni palipo na mapenzi.”
Mapenzi bora huleta amani na utulivu. Mapenzi bora huleta mwafaka na kuondoa mshaka na hivyo furaha kutawala katika jamii. Mfano katika ubeti wa 552-557 katika 552.
“Ni kitu chenye Baraka,
Na mambo huwa mwafaka,
Halizuki la mashaka,
Wala neno la tatizi.”
Aidha mwandishi ameonesha hasara jamii inazoweza kuzipata kwa kukosa mapenzi bora kama ifuatavyo;
Mapenzi yakimezwa na chuki huleta kutokuelewana na kupotea kwa amani katika jamii,tena anasisitiza kuwa chuki ni kitu hatari kama moto katika jamii. Mfano katika ubeti wa 333-35
“Chuki inashinda moto,
Ikisadifu mateto,
Chuki ni kitu kizito,
Kueka hatukiwezi.”
Kukosekana kwa mapenzi bora ni chanzo cha masikitiko,masumbuko,maudhi na ghasia/fujo katika jamii. Mfano katika ubeti wa 195-198
“Kitu chenye maudhiko,
Na fujo na masumbuko,
Dhiki na masikitiko,
Kuwapo ni pingamizi.”
Kukosekana kwa mapenzi bor akatika jamii huleta ubaguzi,hufanya watu wadhulumiane. Mfano katika ubeti wa 126.
“Ubaguzi ni husuda,
Wala hauna faida,
Unadhuru kila muda,
Katika kila kizazi.”
DHAMIRA NDOGO NDOGO
SUALA LA CHUKI
Mtunzi ametuonesha kwamba chuki sio jambo la kukumbatiwa na ina madhara makubwa kama ikiendekezwa na pia ameifananisha na laana, huleta maudhi na huweza kuharibu mambo kwa muda mfupi. Mfano katika ubeti wa 335,336 na 345
“Chuki madhara ya dhati,
Afadhali ya mauti,
Ni faradhi kwa umati,
Chuki inanyong’onyezi.”
SUALA LA CHOYO
Mwandishi ametuonesha kwamba choyo ni tatizo kubwa,humfanya mtu asione na asiwe na mapenzi kwa wenzake na pia huleta uadui, choyo humfanya mtu akawa mpumbavu. Mfano katika ubeti wa 364-378
“Akiwa katika choyo,
Mtu fahamu hinayo,
Kadiri hali iwayo,
La mapenzi haliwezi.”
MATABAKA
Mtunzi ameweka wazi namna jamii yetu ilivyo na matabaka na hasa tabaka la wenye nacho yaani matajiri na wasio nacho yaani masikini. Haya yamebainishwa katika ubeti wa 95 na 289. Mfano katika ubeti wa 95
“Maskini na tajiri,
Watu wa kila umri,
Kulia watakithiri,
Kama hili hubarizi.”
SUALA LA KULEWA SIFA
Mtunzi amezungumzia suala la mtu kulewa sifa na jinsi jambo hili lilivyo na madhara makubwa. Anasema mtu akilewa sifa humfanya ahadaike,alaghaike na huweza kumletea matatizo mengi. Mfano katika ubeti wa 211,212 na 215.

“Mimi sifa za dunia,
Sina haja kusikia,
Sababu zinahadaa,
Na wingi wa mapinduzi”.
SUALA LA ULEVI
Mtunzi amezungumzia suala la ulevi wa pombe na mihadarati,ameonesha kwamba ulevi wa vitu hivi humfanya mtu asiwe na mawazo mema,fikira zake zigure,awe bwege,akili zisimtoshe na kupungua kwa fikra. Mfano katika ubeti wa 49-58 Ubeti wa 52.
“Nahisi kalewa mbege,
Ni sawa na mtu bwege,
Mapenzi tunda za ndege,
Wanayama na sisimizi.”
UJUMBE
Mwandishi S. Robert ameibua ujumbe wa aina tofauti katika utenzi wake huu kama ifuatavyo;
Kila mwanajamii bila kujali ni masikini au tajiri anahitaji mapenzi ya dhati yaliyo bora,kwani mapenzi ni muhimu kwa matabaka yote. Mfano katika ubeti wa 95
Mapenzi ya kweli ni tiba,uguzo kwa wagonjwa na ni faraja kwa yatima. Kwa kuwa mapenzi ni muhimu kwa kila mzunguko wa maisha. Mfano ubeti wa 251-252
Mapenzi ya dhati yaliyo bora kwa mwanadamu yeyote ni muhimu kwani pakikosekana mapenzi kwa muda mfupi,kwa mfano hata kwa muda wa saa moja tu wanadamu watakufa kwa majonzi. Mfano ubeti wa 323
Mapenzi ya kweli huondoa uhasama,tuhuma na fitina. Palipo na mapenzi ya kweli panakuwa hakuna migongano. Mfano kama inavyooneshwa katika ubeti wa 137.
Chuki haifai hivyo sharti itokomezwe kabisa,na hakika ina madhara makubwa. Chuki huleta hila na ukabila na huleta aibu.Mfano katika ubeti wa 127 na 132.

FALSAFA
Mwandishi Shaaban Robert  anaamini kuwa mapenzi bora,yaani mapenzi ya kupendana wanajamii wote bila kujali tofauti zetu za rangi,dini,kabila na tofauti nyingine pamoja na kumpenda Mwenyezi Mungu yataifanya dunia iwe mahala pazuri sana pa kuishi na pia Mwenyezi Mungu atatupatia thawabu.
MSIMAMO
Katika utenzi wa Mapenzi bora mwandishi ametumia mitazamo yote miwili yaani wa kidhanifu na kiyakinifu.
Kiyakinifu mwandishi ameonesha kwamba mapenzi ya kweli ni muhimu kwa maendeleo ya nyanja zote za maisha ya binadamu. Hii ni kutokana na jinsi alivyolizungumzia suala la mapenzi ya kweli na nafasi yake katika kuleta maendeleo,amani,kuondoa matabaka,ubaguzi na kupambana na tuhuma na fitina kwa wanajamii.
Kidhanifu,washairi wa kale walisisitiza sana umuhimu wa kupendana. Mapendo waliyosisitiza yalikuwa mbinu mojawapo ya kuwapofusha wanyonge ili wasipambane kitabaka bali wapendane na matajiri.  Maskini, yaani wanyonge, wasiwaonee wivu matajiri kwani Mungu ndiye kawapa,kwa hiyo kila mmoja aridhike na alichopewa.
Katika utenzi wa Mapenzi Bora, Shaaban Robert anasisitiza watu wapendane, waridhike na hali zao, kwani asiyeridhika na hali yake hupata tamaa “mbaya”. Kwahiyo mapenzi bora aliyokuwa anayasisitiza S. Robert yalikuwa mapenzi “duni”, kwani katu hayangewasaidia wanyonge kujikomboa.

FANI
MUUNDO
Mtunzi  S. Robert  ametumia muundo ambao beti zake zimeundwa kwa mishororo minneminne yaani tarbia,ambapo kila mshororo una mizani nane,vina vya mwisho vilivyojitokeza katika utenzi huu ni ‘zi’ na ‘nzi’.
MTINDO
Katika diwani hii mtunzi ametumia mtindo wa usahiri wa monolojia,  kwani utenzi huwa ni simulio juu ya jambo fulani lakini kwa lengo la kuiadilisha jamii, aidha mtunzi ameandika beti 700 akifafanua kiundani suala la mapenzi bora.
Kila ubeti una mishororo minne yenye mizani nane na vina vinavyofanana katika mistari mitatu ya mwanzo ya kila ubeti.

MATUMIZI YA LUGHA
Tamathali za semi
Sitiari
Mapenzi ua la moyo mfano ubeti wa 161Hapa mtunzi alikuwa na maana kwamba mapenzi huufurahisha na kuupendeza moyo wa aliye nayo.
Kupendana ni ungwana mfano katika ubeti wa 206 Hapa mtunzi alikuwa na maana kuwa kupendana ni jambo la busara kwa kila mmoja.
Chuki mwanawe ni kondo mfano katika ubeti 280.Hapa mtunzi alikuwa na maana kwamba chuki haina maana na inarudisha nyuma juhudi za kusonga mbele.
Maisha ni utelezi mfano katika ubeti wa 641, Hapa pia mwandishi alikuwa na maana kwamba maisha ni kama jambo linaloweza kukatika muda wowote.
Tashihisi
Tunachekwa na wadudu,wajinga wa kuabudu mfano katika ubeti wa 201, Mtunzi amewapa wadudu uwezo wa kucheka kama binadamu, kwamba tusipoyazingatia mapenzi yaliyo bora hata wadudu watatucheka.
Chuki ilie kwa wivu mfano katika ubeti wa 583, Mwandishi ameipa chuki uwezo wa kulia na kuwa na wivu kama binadamu.
Kondoo na mbwamwitu, hawakuteta kwa kitu mfano katika ubeti wa 630, Aidha, mwandishi amewapa uwezo kondoo na mbwa mwitu uwezo wa kuteta. Kuteta ni jambo aliwezalo binadamu peke yake.
Tashibiha
Katika utenzi wa Mapenzi Bora tashbiha zifuatazo zimejitokeza;
Mapenzi kwa mwanadamu,kama mshipa na damu, mfano katika ubeti wa 86, Mtunzi amelinganisha mapenzi kwa wanadamu kama damu na mishipa vinavyotegemeana,kwamba kimoja hakiwezi kuwepo na kikafanya kazi bila mwenzake.
Yawambe kama mimea katika ubeti wa 242, Hapa mtunzi anahamasisha kwamba mapenzi sharti yakuwe na kuimarika kama mimea, 
Chozi litatiririka,mfano kama gharika katika ubeti wa 278, Mtunzi analinganisha utiririkaji wa machozi ya kukosa mapenzi na gharika. Anaonesha jinsi machozi yatakavyokuwa mengi.
Twanuka kama kutuzi katika ubeti wa 298, Mwandishi anaonesha namna wanajamii wasio na mapenzi wanavyoweza kuonekana kwamba wananuka kama kutuzi.
Mubalagha
Katika utenzi mifano kadhaa imeonekana kama vile;
Nyuso zote zitatota,kwa bahari ya machozi katika ubeti wa 93, Mwandishi ametia chumvi katika hili kwani hata mtu alie kwa kiasi gani hawezi kupata bahari ya machozi.
Nyuso zikifanya Mito, ya bahari ya machozi katika ubeti wa 94, Aidha hapa mwandishi pia ametia chumvi, kwani uso hauwezi kufanya mto na kuwa na bahari ya machozi.
MBINU NYINGINE ZA KISANII
Takriri
Tuna “tata na tatizi”katika ubeti wa 296 na 297
“Choyo” katika beti za 364 hadi 385
“Chuki” katika beti za 330 hadi 336
Inkisari
Ni mbinu ambayo kwayo maneno hufupishwa kwa malengo ya kuleta urari au idadi ya mizani zitakiwazo. Mfano katika utenzi wa Mapenzi Bora
Neno “dumu” katika mstari huo lilitakiwa kuwa neno “kudumu” katika ubeti wa 92
Neno “upuzi” hapa neno hili lilipaswa kusomeka “upuuzi” katika ubeti wa 240
Mazida
Ni mbinu ya kisanaa ambayo kwayo mtunzi hurefusha neno kwa madhumuni ya kupata vina au idadi ya mizani azitakazo. Mfano katika utenzi huu ni;
Neno ”zamani” katika mstari usemao “watu wa zamani hizi ikiwa na maana ya “zama hizi” katika ubeti wa 98
“Wataalamizi” katika ubeti wa 648 likiwa na maana ya “wataalamu”
Mbinu hizi za kifani zimepelekea kuibuliwa kwa maudhui mbalimbali pamoja na kuifanya kazi hii iwe na mvuto wa kipekee.
 JINA LA KITABU
Jina la kitabu linasadifu/linaendana kabisa na yaliyomo katika kitabu kitabu hiki kwani toka mwanzo hadi mwisho wa kitabu mwandishi anajadili na kuonesha maana ya mapenzi bora, sifa za mapenzi bora, faida na hasara za kukosekana kwa mapenzi bora katika jamii yoyote.
KUFAULU KWA MWANDISHI
KIFANI
Mwandishi aefaulu sana kutumia lugha rahisi na Kiswahili sanifu,na maneno aliyoona yatawawia magumu wasomaji wake ameamua kuyaorodhesha nyuma yaani mwishoni mwa utenzi wake na kuyatolea maana.
Pia, mwandishi amefaulu kwani ametumia tamathali za semi kwa wingi kama vile tashibiha, tashihisi, sitiari na mubalagha pamoja na mbinu nyingine za kisanaa.
Pia, ameweza kuoanisha vipengele vya fani kiasi kwamba vikawiana na maudhui yaliyomo kwenye utenzi wake.
KIMAUDHUI
Mwandishi amefaulu pia katika upande wa maudhui hasa ukizingatia kwamba utenzi huu unaitwa “MAPENZI BORA” ameweza kuonesha umuhimu hasa wa kudumisha mapenzi bora, lakini pia akaweka wazi kwamba mapenzi yenyewe yaliyo bora ni yapi hasa, na pia akaeleza wazi yale yanayoweza kuwakumba wanadamu wasipozingatia na kuwa na mapenzi ya kweli yaliyo bora.
KUTOFAULU
KIMAUDHUI
Katika kipengele hiki kwa kiasi kidogo hajafaulu kwa sababu anasisitiza watu wapendane, waridhike na hali zao, kwani asiyeridhika na hali yake hupata tamaa “mbaya”. Kwahiyo mapenzi bora aliyokuwa anayasisitiza S. Robert yalikuwa mapenzi “duni”, kwani katu hayangeswasaidia wanyonge kujikomboa. 



















No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...