Monday, April 13, 2020

UHAKIKI WA RIWAYA YA TAKADINI

8UHAKIKI WA RIWAYA RIWAYA YA TAKADINI MWANDISHI: BEN HANSON MCHAPISHAJI: Mathews Bookstore
UTANGULIZI
TAKADINI ni riwaya inayoeleza maisha ya jamii za kiafrika na tamaduni zake.Riwaya hii inaeleza namna jamii nyingi za kiafrika zinavyowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye ulemavu kutokana na mila potofu.Katika riwaya hii mwandishi amemtumia kijana Takadini aliyezaliwa sope alivyowakilisha waathirika wa mila hizo potofu.
 MAUDHUI DHAMIRA KUU; UKOMBOZI
Mwandishi ameeleza kuwa ili tuweze kupata ukombozi wa kweli na kujenga jamii mpya tunapaswa kuachana na mila potofu na kukomboka kifikra na kiutamaduni.Miongoni mwa mila hizo ni mauaji kwa watu wenye ulemavu.Takadini alizaliwa sope aliamriwa auawe siku ya pili tu toka atoke tumboni mwa mamaye Sekai. Aidha makwati anasikitika baada ya kuletewa taarifa kuwa mtoto aliyezaliwa ni sope anasema…..hilositalielewa……itakuwaje….aliuliza maswali mengi (uk 12).Bila ngozi?,Sope?ni nini ulichokileta hapa kwetu?maswali haya yanaonyesha namna walemavu wasivyothamini
wa.Suala hili lilimsononesha sana Sekai inaonyesha dhahiri mtoto sope katika jamii ya Makwati hakustahili kuishi.
 DHAMIRA NDOGO NDOGO MAPENZI Mwandishi anaonyesha mapenzi katika sura mbili tofauti yale ya dhati na ya uongo.Mapenzi ya dhati hayachagui hali wala mali pia kabila dini wala rangi.Kila mtu ana haki ya kupendwa na kupenda Mapenzi ya dhati kati ya Sekai na mwanae, Sekai alikuwa radhi auawe ilimradi furaha yake itimie ya kubaki na mwanawe sope, hakuogopa kufa alimlinda takadini na kuamua atoroke baada ya makwati kuruhusu wazee wamwangamize Mapenzi ya dhati kati ya Sekai na Tendai hawa ni marafiki wa kweli walifarijiana baada ya kuelezana matatizo yao,Tendai mke mdogo wa mtemi masasa aliyelazimishwa kuolewa na mzee wa rika la baba yake. Mapenzi ya dhati kati yaMzee Chivero na Sekai, mzee Chivero alimpokea Sekai na mwanawe Takadini na kuwachukulia kama wanawe (familia yake)licha ya wanakijiji wengine kuwatenga Mapenzi ya dhati baina ya Takadini na Shingai ,Shingai alimpenda Takadini licha ya kuwa na ulemavu wa ngozi (sope)pia mlemavu wa mguu (alitembea kwa msaada wa gongo)kama anavyokiri mwenyewe “huyu ndiye mwanaume ninayetaka anioe” Mapenzi ya uongo ni baina ya Makwati na Takadini, Nhamo na Shangai, Sekai na wake w
enza isipokuwa Pindai
NDOA ZA MITARA
 Mwandishi ameeleza athari za ndoa za mitara kuwa ni pamoja na chuki baina ya wanawake na hivyo kusababisha migogoro ndani ya familia.Mfano Sekai anasengenywa na wake wenza wake Dedirai,na Rumbidzai na kudai ni mchawi. Aidha wake wa Mtemi Masasa wanamdharau Tendai na kuchukulia kama mtoto wao na si mke mwenzao kwa sababu ya umri wake mdogo
 MILA POTOFU
Dhamira hii imetazamwa katika sura tofauti kama vile:- Wazazi kuwachagulia watoto wao wenza (wake/waume)Tendai na Shingai wanalazimishwa kuolewa na watu wasiowataka,hii ni mila potofu zilizopitwa na wakati. Pia Mauaji kwa walemavu, mwandishi anaonyesha kuwa watu wenye ulemavu hawakustahili kuishi katika himaya ya akina Makwati na mtemi Masasa na ndiyo maana kuzaliwa na kuishi kwa Takadini kulileta mzozo. NAFASI YA MWANAMKE Jamii nyingi za kiafrika zinamkandamiza mwanamke na kumfanya mtu duni katika Nyanja mbalimbali za maisha,kama ifuatavyo; Mwanamke hana maamuzi yake binafsi,watoto wa kike hawapati haki sawa na watoto wa kiume.mfano Tendai anaonekana kutofurahishwa na tendo la kuolewa na mume mwenye umri mkubwa (mzee Masasa)alisema “ni heshima kuwa mke wa mtemi mwenye nguvu kama Masasa lakini namchukulia kama baba yangu kuliko mumewangu”…….’’(uk 47)hapa inaonyesha mwanamke hana nafasi ya kuongea kama mtu mwingine. Mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe,hili linaonyeshwa kwa mzee Makwati na Mtemi Masasa kuwa na wanawake wengi kwa ajili ya kujifurahisha na hili linajitokeza bayana pale(uk 40) aliletwa mtoto kumpa joto mzee angehisi msisimko wowote ule wa mapenzi. Mwanamke anachorwa kama mwanamapinduzi, haya yanajionyesha wazi kwa Sekai na Shingai ni wanawake walioleta mabadiliko katika jamii.mfano Sekai alikuwa wa kwanza kuvunja mila na desturi kwa kukataa Takadini asiuawe na kuamua kutorokea kijiji cha jirani pia alileta mabdiliko akiwa uhamishoni Shingai naye mwanamapinduzi kwani alipingana na suala kuchaguliwa mchumba aliamini kuwa ndoa ya kweli inahusisha watu wawili waliopendana na waliochaguana alisema “ Si kwamba ninamchukia Nhamo ,la hasha isipokuwa sidhani kama nitakuwa furaha ya kuishi naye”(UK 110)mwisho mwandishi anaonyesha Shingai ameolewa na Takadini na wamezaa mtoto asiye sope. UMOJA NA MSHIKAMANO Umoja na mshikamano ni moja kati ya nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko na ukombozi wa kiutamaduni,mshikamano mzuri ulionyeshwa na mzee Chivero,Tendai,mtemi Masasa ulisaidia kumlinda Takadini dhidi ya unyanyapaa na hatari ya kupoteza maisha katika mapambano yoyote yenye umoja na nguvu utengano ni udhaifu UJASIRI Mwandishi ameonyesha kuwa Sekai ni mwanamke jasiri aliepambana kufa na kupona kumlinda mwanae Takadini dhidi ya mila na desturi za kikatili hatima yake kuleta ukombozi katika jamii. Shingai naye ni mwanamke aliyepambana na matatizo ya kuchaguliwa mchumba,mila zinazokandamiza wanawake. SUALA LA MALEZI Malezi ya watoto yanapaswa kusimamiwa kwa pamoja yaani baba na mama.Katika kitabu hiki malezi yanaonekana ya upande mmoja mfano Sekai ndio mlezi mkuu wa familia hususani malezi ya Takadini.Shingai naye anapata malezi kwa mama,shangazi na bibi hata anapokata shauri la kutorokea kwa Takadini ,anaulizwa kuwa ndivyo ulivyolelewa?mzee Nhariswa anampiga mkewe na kusema “umefanya nini wewe mwanamke tangu mwanao alivyopeleka maji kwa Sekai umefuatilia kujua anachokifanya …uliona dalili kwanini hukutafuta dawa? UJUMBE Walemavu wana haki sawa ya kuishi kama watu wengine hivyo wathaminiwe. Malezi yanahusisha pande zote mbili yaani baba na mama hivyo kila mmoja awajibike. Wanawake wawe na maamuzi katika jamii hiyo ili wasinyanyaswe Ndoa nibaina ya watu wawili wapendanao hivyo haipaswi kuingiliwa na mtu yoyote Umoja na mshikamano ni jambo muhimu katika ukombozi wa jamii yeyote ile. MTAZAMO WA MWANDISHI Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu,anaona kuwa matatizo yanayotokana na mila na desturi yanaweza kukataliwa na watu wengine kwa kuchukua hatua za kujikomboa kama alivyofanya Sekai na wenzake. MSIMAMO WA MWANDISHI Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameeleza udhaifu wa baadhi ya mila na desturi zinazokandamiza watu hivyo anataka jamii ijikomboe dhidi ya mila desturi hizo. FALSAFA Mwandishi anaamini kuwa binadamu wote ni sawa hata kama kuna tofauti za kimaumbile lakini kila mtu ana haki ya kuishi . MIGOGORO Migogoro imejitokeza sehemu mbalimbali katika riwaya hii ya TAKADINI kama ifuatavyo; Mgogoro kati ya Makwati na Sekai,chanzo cha mgogoro huu ni (mila na imani potofu) baada ya Sekai kuzaa mtoto sope,mtoto huyo alipaswa auawe ,mwandishi anasema suala hili halikuungwa mkono na Sekai,suluhisho sekai aliamua kutoroka kijijini ili kunusuru maisha ya mtoto Takadini. Mgogoro wa Shingai na wazazi wake,Chanzo cha mgogoro huu ni mila potofu wa kuchaguliwa mchumba ambaye ni Nhamo ambapo wazazi walikasirika hata kumtolea maneno mabaya,suluhisho ni Shingai anaamua kutorokea kwa Takadini. Mgogoro kati ya Sekai na wake wenzake,chanzo cha mgogoro huu ni Makwati kuzidisha upendo kwa Sekai hivyo waliamini kuwa Sekai ni mchawi Mgogoro wa nafsi huu unajitokezakwa Tendai ambaye aliozwa kwa mzee Masasa ambaye alikuwa na umri mkubwa Mgogoro wa kijamii,chanzo cha mgogoro ni kuzaliwa mtoto mlemavu(sope)kulizuka mgogoro baina ya wanajamii ,wao walitaka Sekai na mtoto wake wafukuzwe. MUUNDO Mwandishi ametumia muundo wa msago (moja kwa moja).Mwandishi ameanza mwanzo kuonyesha mimba ya Sekai ambayo inazua chuki kwa wake wenza pia anapozaa mtoto wa kiume (sope). Sekai anaamua kutoroka ili kuokoa maisha ya mtoto,anaishi ugenini siku nyingi hata sope anakuwa mkubwa na kupata mke na mwisho kabisa mwandishi anaonyesha Sekai akipanga kurudi kwao. MTINDO Mwandishi anatumia mtindo wa masimulizi vilevile kuna matumizi ya dayalojia (UK 4) Dadirai na Rumbidzai wanajibizana Je na yule mbuzi wako uliepewa na baba mzee Makwati amekupa watoto wangapi? Tangu nimepata ni miaka miwili sasa na tayari ana watoto wawili nabado anatarajia mwingine. Pia mwandishi ametumia nyimbo (UK 2) Mashamba yote yamelimwa mbegu zote zimepandwa zimechipua na kumea,sisi watatu tumepata mavuno yetu.,Mheshimiwa wetu amemiliki mavuno kwa mikono yake halisi kutoka mashamba yetu yote lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi ile isiyomea kitu?……….. MATUMIZI YA LUGHA Mwandishi ametumia lugha rahisi inayotumika kwa watu wengi,pia ametumia tamathali za semi,nahau,misemo na mbinu nyingi za kisanaa. MISEMO NA NAHAU Misemo na nahau imetumika katika riwaya hii ili kuipamba kazi yake “Habari njema kuchechemea kwa mguu mmoja lakini mbaya kukimbia kama sungura.Msemo huu unamaanisha kwamba habari njema hazienei haraka ila mbaya huenea haraka sana Pia kuna misemo mingi Kama Pokea upewacho Maosha ni matamu Kanga hawezi kutua kwenye bua la mtama Mume ni kiungo kwa mwanamke TAMATHALI ZA SEMI Tashibiha Matumizi ya tashibiha yamejitokeza sehemu mbalimbali Giza jepesi lilibakia ukutani kama mgeni asiyekaribishwa na asiyetaka kuondoka Muda huenda polepole sana mithili ya mwendo wa kakakuona (UK 6) Tashihisi Mwandishi wa riwaya ya Takadini ametumia tashihisi sehemu mbalimbal; kama vile’ Ubongo wake uliathiriwa kwa mawazo yaliofukuza usingizi wake Fikra zilizopingana zilijichomeka katika nafsi yake Mwanga wa jua ungaavu za novemba uliingia ndani na kulifukuza giza totoro. Dhihaka Mwandishi ametumia tamathali iliyoonyesha dharau na yenye lengo la kumweka mtu katika hali duni kupita kiasi lakini kwa mbinu ya mafumbo (uk 2) “Naamini ulichobeba sasa ni mtoto na si dubwasha” Haya maneno yalimlenga Sekai kwakuwa siku zote waliamini hazai Tafsida Mwandishi ametumia tamathali hii kufichaukali wa maneno (uk 83) Akashambulia hata sehemu za siri (UK 17)walifanya tendo la ndoa Takriri Wewe ni sope,sope,sope Najua ,najua (UK 79) Mdokezo Siku moja sijui lini ….lakini hivi (UK 75) Sukuma mara moja tena ….(UK 125) WAHUSIKA Takadini Huyu ndiye mhusika mkuu wa riwaya hii. Ni mtoto wa Sekai. Ni mlemavu wa mguu na ngozi (zeruzeru ). Kijana wa kiume. Ni mchapakazi na anayependa kujituma.Ni mtiifu.Ni jasiri.Ni mwathirika wa mila na desturi mbaya au zilizopitwa na wakati.Anafaa kuigwa na jamii. Sekai Ni mhusika mkuu. Ni mama yake Takadini. Ni mke wa kwanza wa Makwati. Mwana mapinduzi. Mwathirika wa mila na desturi zilizopitwa na wakati. Ni Jasiri. Ni mwenye huruma.Ni mwenye upendo Makwati Mume wa Sekai.Baba wa Takadini. Ni mkali. Anapendana na mke wake, Anashiriki mila za kale Chivero Ni mzee wa makamo. Ni mganga wa kienyeji. Mwenye upendo. Mwenye huruma.. Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa.Mpenda mabadiliko. Alimpokea Sekai na Takadini Mtemi masasa Mzee wa makamo. Ni Mtemi wa kijiji. Mwenye heshima. Ni mpole na Mwenye huruma.Mwenye wake wanne. Shingai Ni binti wa mzee Nhasriswa.Mke wa takadini.Ni jasiri. Mwanamapinduzi. Ni msichana mwenye msimamo na mapenzi ya kweli na takadini. Mpenda mabadiliko. Ana huruma .Anafaa kuigwa Tendai Mke mdogo wa mzee Masasa. Ni mke mkarimu. Mwanamapinduzi. Ni mpole .Rafiki kipenzi wa Sekai Dadirai Mke wa tatu wa Makwati.Ni mwenye roho mbaya Mpenda majanga .Ana wivu .Ana mawazo potofu MANDHARI Mwandishi ametumia mandhari ya kijijini.Mandhari hii inawakilisha vijiji mbalimbali hapa Tanzania na Bara la Afrika.Kwa ujumla mahala ambapo hakuna elimu kuhusu ulemavu wa ngozi haijaeleweka vema au hakuna kabisa.Pia vijiji ambavyo huduma kama shule hakuna JINA LA KITABU TAKADINI linasanifu yaliyomo kuwa kuna neno TAKADINI lina maana ya sisi tumefanya nini?Swali ambalo wahusika wengi wanajiuliza mfana Sekai na wanawake wasiozaa na hata vijana au watu wenye ulemavu UCHAMBUZI WA RIWAYA WATOTO WA MAMA NTILIE MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS MWAKA: 2002 WASIFU WA MWANDISHI Emmanuel Mbogo ni Profesa wa drama na fasihi na amehudumu katika vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo, Chuo Kikuu cha Kenyatta Kenya na Chuo Kikuu Huria. Mbogo ni mwanafasihi mahiri sana katika Afrika ya Mashariki. MUHTASARI WA RIWAYA Maman’tilie, mama mwenye watoto wawili lakini wote wamefukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Anajitahidi hapa na pale ili apate, lakini wapi? Pesa imegeuka nyoka inateleza kwenye nyasi. Mumewe Mzee Lomolomo hana muda, yeye kila kukuchapo huelekea bunge la walevi kunywa pombe tani yake. Akiwa huko hunywa na kurudi nyumbani akiwa mbwii! Mwisho mwandishi anauliza swali gumu, ‘Nani anajali?’ MAUDHUI Maudhui hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama mwandishi wa kazi ya fasihi akaandika kazi yake. DHAMIRA Dhamira ni lile wazo linalomfanya mwandishi wa kazi ya fasihi aandike kazi yake. Katika riwaya hii, dhamira nyingi zimejadiliwa kama: UMASIKINI Dhamira hii imetawala katika riwaya. Asilimia kubwa ya wahusika ni watu wenye maisha ya dhiki na kazi za kijungujiko. Umasikini wao unadhihirishwa na mitaa wanayoishi kama: Manzese, Msufini, Tabata, Kisutu na Temeke. Maeneo haya ndiyo yaitwayo uswahilini leo hii. Zita na Pita wanafukuzwa shule kwa sababu ya kukosa ada na sare (uk 1). Mamant’ilie naye anatumia maji ya mwarobaini kutibu homa yake kwa sababu hana pesa ya kununulia dawa za hospitali. ULEVI Unywaji wa pombe kupitiliza huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji. Mzee Lomolomo ni mlevi mzoefu, kutokana na ulevi wake, anashindwa hata kuwalipia ada wanae ili waendelee na shule. Ni ulevi huohuo unamfanya aishi maisha ya dhiki huku akishindwa kutoa mchango kwa familia yake na taifa linalomtegemea. Mwisho Lomolomo anakufa kwa sababu ya pombe. Mwandishi anasema, “… Lomolomo alikuwa lofa, mtu wa kazi za kijungujiko na vipesa vyake viliishia kwenye pombe…” (uk 7). MALEZI YA WATOTO Watoto wasipopata malezi yanayostahili kutoka kwa wazazi wote wawili huwa ni rahisi kwao kujiingiza katika mambo yasiyofaa. Mwandishi anaonyesha aina tatu za watoto. Kwanza kuna Zita na Pita. Hawa wana wazazi wote wawili lakini baba hajishughulishi na malezi yao. Pia mama naye ametingwa na shughuli nyingi katika genge lake la uuzaji wa chakula. Zita na Pita hawana malezi ya kueleweka. Hali hii inamfanya Pita ajiingize katika biashara ya madawa ya kulevya. Pili, kuna Dan na Musa hawa hawana baba, wanaishi na mama zao tu. Mama zao hawawajali wala kuwakemea kwa chochote kibaya wanachofanya. Dan anajiingiza katika ujambazi na kupoteza maisha. Musa anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya na kuishia jela. Tatu kuna Kurwa na Doto. Hawa hawana wazazi kabisa. mwandishi anasema, “… walikuwa chokoraa namba moja, kupigana kulala na njaa, kukamatwa na polisi… yalikuwa sehemu ya maisha yao…” Doto anajiingiza katika ujambazi, huko anauawa na mlinzi Simango. RUSHWA Rushwa imeota mizizi katika jamii. Kila uendako, kila upitako na kila utokako utaambiwa toa rushwa ili upate kitu fulani. Mamant’ilie alishindwa kuyamudu maisha ya mjini kwa sababu ya rushwa aliyokuwa akiwapa askari wa jiji. Kwa kalamu yake isiyoisha wino, Mbogo anaandika, “KSodi na hongo kwa askari wa jiji, ziliikamua faida yake.” (uk 32). MMOMONYOKO WA MAADILI Maadili ya siku hizi si yale ya zamani. Miaka inabadilika na vizazi navyo vinabadilika. Watu ni watu tu lakini hawana utu. Watoto wadogo sasa wanavuta sigara na kutafuna mirungi kama tumuonavyo Dan na Musa. Watu hawana moyo wa kusaidiana tena, wao wanaamini kuwa kila mwenye janga atalila peke yake. Zita anazidiwa na maradhi yaliyosababishwa na kuumwa na mbwa mwenye kichaa. Watu hawakumsaidia, badala yake walivishangilia vioja alivyovifanya. Mwandishi anatuonesha Zenabu akiwaomba msaada na kuwakalipia, “Nisaidieni, mnacheka nini? Wendawazimu wakubwa.” (uk 82). NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII Nafasi ya mwanamke ni jumla ya matendo yote yafanywayo na mwanamke katika jamii yake. Mara nyingi huwa mabaya na yenye mtazamo hasi, lakini mara chache huwa mazuri yenye mtazamo chanya. Mwandishi wa riwaya hii, amemchora na kumjadili mwanamke kwa mawanda mapana kama inavyoelezwa: Mama mlezi na mwangalizi mkuu wa familia. Maman’tilie ndiye aliyejua familia yake ile nini, ifanye nini na iishi vipi. Mumewe mzee Lomolomo hakuwa na mchango wowote. Yeye kila kukuchapo alikwenda kilingeni kufakamia mataputapu na pombe haramu. Mwenye huruma na moyo wa kutoa msaada. Zenabu anawakilisha tabia hii. Alimsaidia Pita alipokuwa na njaa. Ni yeye akishirikiana na Mama sara walimpeleka Zita hospitali. Mwenye mapenzi na kazi. Kurwa anapenda kazi, alifuatana na Maman’tilie kwenda gengeni, huko alimsaidia kuuza chakula. Hata siku moja kurwa hakuchoka kufanya kazi. Aliyenyimwa elimu. Zita ni mwanamke aliyenyimwa elimu. Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Mzembe na asiyejali malezi ya watoto. Mama Musa ni mzembe na hajali malezi ya mwanae. Yeye ameshika themanini zake na Musa kashika hamsini zake. UJUMBE Ujumbe ni funzo litolewalo na kazi ya fasihi. Mafunzo mengi yametolewa katika riwaya hii: Watoto wasifukuzwe shule kwa sababu ya kukosa ada, kwani kufanya hivyo kunawanyima haki yao ya kupata elimu. Majalala ya kuchoma takataka yajengwe mbali na makazi ya watu. Mwandishi anasema, “Mapafu ya wakazi yaliendelea kuteketea kwa moshi siku hadi siku… watu wale walikuwa wanakufa taratibu.” (uk 27). Pombe si suluhisho la matatizo. Mzaha mzaha hutumbua usaha. Zita alikwaruzwa na mbwa mwenye kichaa, lakini wakapuuzia, mwishi ni kifo cha Zita. MIGOGORO Migogoro ni kukosekana kwa maelewano baina ya watu binafsi, jamii, taifa au mataifa. Migogoro iliyojitokeza ni: Migogoro ya wahusika Mwalimu Chikoya na wanafunzi wasiokuwa na ada wala sare za shule. Huu unasababishwa na wanafunzi wasiokuwa na ada wala sare. Suluhisho lake ni wanafunzi hao kufukuzwa shule. Maman’tilie na mzee Lomolomo. Huu unasababishwa na ulevi wa Lomolomo. Suluhisho ni kifo cha mzee Lomolomo. Peter na Doto. Huu unasababishwa na Doto kumfukuza Pita jaani. Suluhisho la mgogoro huu ni Kurwa kumsaidia Peter. Mgogoro wa nafsi, Huu unampata Peter, yeye anamawazo ya kurudi shule lakini hajui ni kipi afanye ili apate pesa za kumrudisha. Migogoro mingine ni: migogoro ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. FALSAFA Falsafa ni imani ya mwandishi. Emmanuel Mbogo anaamini kuwasaidia watoto kupata elimu yao kutaondoa matatizo yanayozuia ujenzi wa jamii mpya. MTAZAMO/MSIMAMO Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Anaamini kuwapatia watoto elimu na kusimamia malezi yao kutaliokoa taifa. UCHAMBUZI WA FANI NA VIPENGELE VYAKE Fani ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake. Fani ndiyo hutupatia kile kiitwacho maudhui. Katia riwaya hii, fani imechambuliwa Kama ifuatavyo: WAHUSIKA Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa uwakilisha tabia za watu katika kazi ya fasihi. Wahusika waliopo katika riwaya hii ni: Maman’tilie. Ni mke wa mzee Lomolomo. Ni mchapakazi. Ni mama yao Zita na Peter na anafaa kuigwa na jamii. Lomolomo. Ni mume wa Maman’tilie. Ni mlevi wa pombe haramu. Hawajibiki katika malezi ya watoto wake na hafai kuigwa na jamii. Zita. Mtoto wa Maman’tilie na mzee Lomolomo. Alifukuzwa shule kwa kukosa ada na sare akiwa darasa la sita. Pia, alikwaruzwa na mbwa mwenye kichaa. Mwisho anakufa kwa kupuuzia ule mkwaruzo wa mbwa. Peter. Mtoto wa Mzee Lomolomo na Maman’tilie. Anafukuzwa shule akiwa darasa la tano. Anatafuta ridhiki dampo. Baadaye anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya. Chikoya. Ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Makurumla. Anawafukuza wanafunzi wasiokuwa na sare wala ada. Musa. Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Hamheshimu mama yake. Anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya. Sara. Mwanafunzi wa Makurumla na ni jirani yao Zita. Mama Sara. Mama yake Sara. Alimsaidia Zita alipopatwa na kichaa. Zenabu. Anafanya kazi Kikale Bar. Ana huruma. Anafaa kuigwa. Kurwa. Ni yatima. Anaishi vichochoroni. Anategemea chakula cha dampo. Anasingiziwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Doto. Ni yatima. Anauawa kwa kujihusisha na ujambazi. Rhemtulah. Ni mfanyabiashara wa kihindi. Simango. Ni mlinzi wa Rhemtulah. Anawaua Doto na Dan. Dani. Ni mtoto ambaye hamjui baba yake. Anauawa kwa kujihusisha na ujambazi. Jane. Aliwalea Doto na Kurwa baada ya kufiwa na mama yao. Naye pia anakufa. Master Baroni. Anawatumia watoto katika biashara yake ya madawa ya kulevya. Si mfano wa kuigwa na jamii. MATUMIZI YA LUGHA Fasihi ni sanaa itoayo maudhui kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa au kuandiwa. Kipengele cha lugha ni muhimu kwani ndicho kinachotofautisha fasihi na sanaa zingine. Lugha iliyotumika katika riwaya hii ni nyepesi na yenye kueleweka. Mwandishi ametumia vipengele vingi vipatikanavyo katika matumizi ya lugha kama: ucheshi na lugha ya picha, misemo na tamathali za semi. TAMATHALI ZA SEMI Tamathali za semi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Wakati mwingine hutumiwa ili kupamba na kuongeza utamu wa kazi za fasihi. Mwandishi ametumia tamathali nyingi za semi kama: Tanakali sauti (onomatopoeia). Tanakali sauti ni maneno au nomino ziundwazo katika sentensi kutokana na sauti zinazofanana. “Bwee!” “Paah!” (uk. 5) Tashibiha. Katika tamathali hii, watu ama vitu viwili au zaidi hulinganishwa na watu au vitu vingine kwa kutumia maneno, ‘kama’, ‘mithili’… “Masikio yamesimama wima kama anasisitiza kitu.” (uk. 2) “Mdomo wake uliokaa kama bakuli la pombe.” (uk. 10) Tafsida. Hii hutumika kupunguza ukali wa maneno. “Akaenda haja ndogo.” (uk. 2) “Akakitibu kidonda chake kwa maji ya chumvichumvi.” (uk 55) Takriri. tamathali hii, maneno hurudiwarudiwa ili kuonyesha msisitizo. “Yalaa! Yalaa!” (uk 2) “Mjomba! Mjomba!” Mdokezo. Hapa msemaji husema kitu bila kukimalizia kukitaja. “Shikamoo mama…” (uk 6) “Una… una…” (uk 11) Tashihisi. Hapa vitu hupewa sifa alizonazo binadamu. “Maman’tilie alimtupia jicho bintie.” “Mabega yameangalia juu.” (uk 10). Mjalizo. Katika tamathali hii maneno hufuatana pasipo kiunganishi. “Walikaa, wakala, wakanywa maji, wakamshukuru Mungu.” Kejeli. Hii ni tamathali ya semi ambayo maneno yake huwa kinyume na maana yanayotoa. “Naye pita aliitikia salamu hizo za ukarimu kwa kupiga chafya mbili au tatu.” (uk 19). “Lomolomo uso wake uliopendeza kwa chang’aa…” (uk 70). Sitiari. Tamathali hii hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi. “Wakatembea mwendo wa farasi.” (uk 86). Ritifaa. Katika tamathali hii, mtu huongea na kitu ambacho husikika kwa fikra tu. “Kumbe wewe na mwanao mna hila kiasi hiki? Mmepatana kuondoka na kusafiri katika dau moja.” (uk 94). Misemo. “Ukienda Tabata utapata.” “Waswahili hawana dogo.” Matumizi ya lugha za kigeni. “Nikukonekti.” (uk 78). Methali. “Kamba hukatikia pembamba.” Ucheshi na lugha ya picha. “Alikunywa funda moja, akajisikilizia kabla ya kulimeza. Alisikia pombe ikisafiri kufuata barabara ya lami hadi tumboni.” (uk 87). MTINDO Mtindo ni ule upekee wa mtunzi wakazi ya fasihi na mtunzi mwingine. Mfano, mwandishi anaweza kutumia, nyimbo, mashairi, nafsi zote, dayolojia, monolojia n.k. mwandishi amefanikisha mtindo wake kwa kutumia, Matumizi ya nyimbo. Mfano katika ukurasa wa 10 Lomolomo aliimba, “Kuleni nae, Hata bangi vuteni nae, Lakini ni bure, Mwenzenu nimezaa naye…” Mwandishi katumia monolojia (masimulizi) na dayolojia (majibishano). Mwandishi katumia nafsi zote tatu. MUUNDO Riwaya hii imetumia muundo wa kurukia. Mwandishi amemuonyesha Lomolomo akiwa katika hali ya ulevi, baadaye anatukumbusha alipokuwa anafanya kazi bandarini. Vilevile anawaonyesha Kurwa na Doto wakiishi peke yao. Lakini baadaye anatukumbusha kipindi walipokuwa wanalelewa na mama yao ambaye hata hivyo alifariki kisha wakalelewa na Jane ambaye naye anafariki. MANDHARI Mandhari ni sehemu ambayo kazi ya fasihi hutendeka. Riwaya hii imetumia mandhari ya jiji la Dar es Salaam na mitaa yake kama, Manzese, Msufini, Tabata, Kisutu, Urafiki na mtaa wa Ajentina. JINA LA KITABU Jina la kitabu, Watoto wa Maman’tilie, linasadifu yaliyomo, kwani ndani ya riwaya hii kuna mhusika mkuu ambaye ndiye Maman’tilie. Riwaya hii inamwonesha mama huyu akijaribu kujinasua yeye na watoto wake katika wimbi la umasikini, lakini wapi? Jitihada zote anazofanya zinagonga mwamba na matatizo yake yanazidi kuongezeka. KUFAULU KIMAUDHUI Mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuonyesha shida wazipatazo watoto wa mitaani. Mwandishi amefanikiwa kuonyesha madhara ya umasikini. Mwandishi ameonyesha madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi na ulevi. KUFAULU KIFANI Amekitendea haki kipengele cha mtindo, kwani humo ametumia vipengele vingi kama nyimbo n.k. Kazi yake imeshibishwa kwa tamathali nyingi za semi. Ametumia lugha ya picha inayomwelewesha zaidi msomaji. KUTOFAULU KWA MWANDISHI 1. Kimaudhui. Mtazamo wa mwandishi katika suala la umasikini hauko sawa. Yeye anaamini hata ukifanya kazi kwa bidii kama ni masikini utaendelea kuwa masikini kama tumuonavyo Maman’tilie. 2. Kifani wahusika wa mwandishi hawana uwiano. Wengi wao ni watu masikini. Pia, mandhari yote yaliyotumiwa na mwandishi ni ya mjini. Mwandishi ameutenga upande wa kijijini ambao nao kama ungetazamwa, jamii ingejifunza mengi. MASWALI YA MAZOEZI Maadili mema na maonyo yamejadiliwa na washairi wa diwani. Onesha mjadala huo kwa kutumia diwani mbili. Ni kwa vipi muundo na mtindo wa ushairi hutofautiana na muundo wa riwaya na tamthilya? Tetea jibu lako kwa kuonesha jinsi muundo na mtindo wa ushairi ulivyo. Ujenzi wa taswira katika kazi za kifasihi hutufanya tuhisi au kuona kabisa uhalisia wa mambo ulivyo. Jadili kwa kutumia diwani mbili ulizosoma. Waandishi wa kazi za fasihi ni walimu? Jadili. Mtazamo, msimamo na falsafa ya mwandishi hututhibitishia ukweli wa mawazo yake katika kazi yake. Fafanua. “Fasihi hubeba yote anayoibusha binadamu katika maisha yake ya kila siku”. Jadili kauli hii kwa kutoa mifano. Fafanua tofauti ya Fasihi simulizi na Fasihi andishi katika vipengele vya fani vifuatavyo: (a) Muundo (b) Mtindo (c) Hadhira (d) Kitanzu Fani na maudhui katika Fasihi ni tunda la marakuja na ganda lake. Jadili kauli hiyo kwa uthibitisho kutoka kwa wataalamu mbalimbali. “Mhakiki ni kivuko kati ya msanii na jamii aliyoiandikia”. Jadili hoja hiyo ukithibitisha kwa mifano madhubuti toka katika kazi za Fasihi andishi za Kitanzania. Fasihi simulizi inaweza kuelimisha au kutoelimisha jamii kutegemea na jinsi ilivyotumika. Thibitisha kauli hii kwa kutumia methali na vitendawili mbalimbali. “Msanii wa Fasihi andishi hutumia vipengele mbalimbali vya Fasihi simulizi ili kuipa kazi yake ubora na mvuto kwa wasomaji wake”. Ukitumia vipengele vitano, fafanua hoja hiyo. Jadili jinsi dhima mbalimbali katika hadithi za Fasihi simulizi zinavyoodhihirishwa na wahusika mbalimbali. “Fasihi inashughulikia utu”. Fafanua usemi huu na thibitisha jibu lako kwa mifano mahususi. “Kila mwanafasihi anatetea tabaka lake”. Jadili kauli hii kwa kutumia mifano ya Tanzania. “Mhakiki wa kazi ya Fasihi ni mnyonyaji wa kazi ya msanii asilia”. Jadili hoja hii kwa mifano. Jadili jukumu la Fasihi simulizi kwa jamii ya Tanzania. Fafanua ni jinsi gani fani na maudhui visivyoweza kutenganishwa katika kazi ya Fasihi. Eleza maana na dhima ya mwandishi wa kazi ya Fasihi kwa wananchi wa Tanzania. Fasihi simulizi inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na utandawazi. Jadili kauli hii kwa kutoa mifano halisi.

No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...