Monday, April 13, 2020

FASIHI KWA UJUMLA

Fasihi; ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayomhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake. (Wamitila, 2004).
Fasili hii imejaribu kufafanua vizuri kile ambacho fasihi inajihusisha nacho, kimsingi fasihi inajihusisha na wanadamu. Vitu vya msingi tunavyoviona katika fasili hii ni kwamba fasihi ni sanaa, na fasihi inatumia lugha lakini zaidi fasihi inajihusisha na wanadamu.
Dhima za Fasihi katika Jamii
Fafanua dhima za fasihi katika jamii
Dhima za fasihi katika jamii ni pamoja na hizi zifuatazo:
  • Kuburudisha jamii:Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.
  • Kuelimisha. Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mabalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.
  • Kuonya jamii. Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
  • Kuunganisha jamii. Fasihi huleta watu katika jamii. Watu huunganishwa kupitia kazi mbalimbali za kifasihi, kwa mfano, kupitia nyimbo, miviga, vichekesho na kadhalika.
  • Kukuza lugha.Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.
  • Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.
  • Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.

No comments:

Post a Comment

Maswali ya vitabu na majibu yake

 NECTA 2012 “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwa...