UHAKIKI WA TAMTHILIYA
TAMTHILIYA: KILIO CHETU
WAANDISHI: MEDICAL AID FOUNDATION
MCHAPISHAJI: TANZANIA PUBLISHING HOUSE (TPH) MWAKA 1995
UTANGULIZI
Kilio Chetu ni tamthiliya inayojikita kuzungumzia umuhimu wa elimu ya jinsia na ukimwi kwa vijana, Tamthiliya hii inaonesha namna ukosefu wa elimu ya jinsia na ukimwi kwa jamii hususani vijana inavyochangia mimba za utotoni au mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana.
Katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna ambavyo jamii ikiangaika kujielimisha kuhusu elimu hii ya jinsia na ukimwa na kuwaacha vijana wakiangamia kwa kukosa elimu hiyo, hali hii inaifanya jamii kugawanyika, wapo wanaoona kuwa suluhisho la janga hili la Ukimwi, ni jamii nzima wakiwemo na vijana kupewa elimu hii lakini wapo wazazi wanaopinga wakiamini vijana umri wao wakupewa elimu hii haujafika bado. Je ni nini hatima ya vijana hawa? Basi tafuta kitabu hiki cha Kilio chetu kisome utajifunza mambo mengi sana ni kitabu kinachotakiwa kusomwa na watu wa rika lolote.
DHAMIRA
Hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Na katika tamthiliya hii kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo ambazo zimejitokeza, kwa kuanza tunaanza na;
(a) Dhamira Kuu
Dhamira kuu katika tamthiliya ni umuhimu wa elimu ya jinsia na ukimwi, mwandishi anaamini kuwa, ili jamii iweze kunusurika na matatizo yatokanayo na kujamiana kama vile mimba za utotoni (mimba zisizotarajiwa) magonjwa ya zinaa kama vile kasendwe, kisonono gono na ukimwi, sharti vijana wapewe elimu ya jinsia na ukimwi, mwandishi anathibitisha hili akimtumia muhusika Mjomba anaposema, “Upepo umebadilika sasa. Hawa vijana wetu wapewe elimu ya familia ikiwepo ya jinsia. Watoto waambiwe wazi juu ya mambo haya ya mapenzi na hatima yake.” Uk. 9
Vilevile, mwandishi anaonesha namna ambavyo vijana wanapukutika, wanaangamia na ukimwi kwa sababu ya kukosa elimu hii ya jinsia na ukimwi, hali hii inasababisha vijana kuwa gizani kabisa wanashindwa namna ya kujikinga na wengine hata kushindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu , rejea ukurasa wa 13, Mwandishi akimtumia muhusika Mtambaji anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani. Watoto ndio kabisa. Wapo katika giza nene. Wanashindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu.”
Si hivyo tu, mwandishi anaendelea kutuonesha kuwa, ukosefu wa elimu hii ya jinsia na ukimwi kwa vijana/watoto inawafanya watoto/vijana kujitenga na mapambano dhidi ya ukimwi kwakuwa wao wanaamini kuwa ugonjwa huu wa ukimwi ni wa wakubwa tu kwani watoto hawawezi kuambukizwa virusi vya UKIMWI kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mwarami anapomwabia Anna, “Ukimwi unawapata wakubwa, Anna.” Uk. 25
Si watoto tu, wapo hata wazazi, watu wazima ambao nao wanaamini kuwa watoto wadogo hawawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi, kama anavyoamini Mama Suzi, rejea ukurasa wa 4, muhusika Mama Suzi anaposema, “…Lakini shoga, watu wanatafuta laana ya marehemu. Kitoto kama kile; kife kwa ukimwi! Ungeingilia kona gani?” {Uk.4}
Mwandishi anaendelea kutuonesha kuwa, hata mimba za utotoni, mimba zisizotarajiwa kwa vijana husababishwa na ukosefu wa elimu hii ya jinsia, kwa mfano mwandishi anamtumia muhusika Suzi ambaye anaamini kuwa, kwa kufanya ngono mara moja hakuwezi kusababisha mtu akapata mimba, hili tunaliona ukurasa wa 28, Suzi anapomwambia Anna, “Wala sina mimba, kwanza mimi nimefanya mara moja tu na joti.” {Uk.28}
Vilevile, mwandishi anaonesha kuwa, wapo watoto/vijana ambao kutokana na kukosa elimu hii ya jinsia, wanaamini kuwa wao kama watoto hawawezi kupata mimba, mwandishi anamtumia muhusika Joti anapowaambia rafiki zake, “Mara moja tu, hakuna mimba sisi watoto.” {Uk. 16}
Mwandishi hakuishia tu kuonesha madhara ya kukosa elimu hii ya jinsia, kwa upande mwingine ameonesha faida za elimu hii ya jinsia na ukimwi kwa vijana, mwandishi anaonesha kuwa, vijana waliopata elimu hii, huwasaidia sana kupambana na kujizuia na vishawishi vya kingono kutokana na uelewa waliokuwa nao, kwa mfano mwandishi anamtumia muhusika Anna, ambaye kutokana na mafunzo aliyopewa na wazazi wake yanamsaidia sana kupambana na kujizuia na vishawishi hivyo kutokana na kufahamu madhara ya kushiriki ngono kabla ya wakati, hili mwandishi analithibitisha akimtumia muhusika Anna anaposema, “…Hujui kama kuna madhara mengine. Hujui magonjwa ya zinaa wewe: hujui kisonono, kaswende na mengine kedekede. Haya hata UKIMWI hujui?” {Uk. 25}
Hivyo mwandishi anashauri, elimu hii ya jinsia na UKIMWI, isitolewa kiubaguzi, itolewe kwa watu wote kwani kila mtu yuko katika hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI, mwandishi anaonesha namna ambavyo vijana wanateketea kwa kubaguliwa kwao kupewa elimu hii, rejea ukurasa wa 1-2, Mtambaji anaposimulia, “Wakubwa wakaandika mabuku kupeana habari. Wakabandika mabango kupeana tahadhari, lakini watoto wakateketea kwa kukosa habari zozote za kuwaokoa.”
Mwandishi anaonesha kuwa, kama vijana wangeelimishwa kuhusu madhara ya kufanya mapenzi kabla ya wakati, namna ya kujilinda, basi wasingetummbukia katika janga hili, mwandishi anathibitisha kwa kumtumia muhusika Suzi anaposema, “Naapa kwa Mungu wangu, mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa, tusingetumbu…tusi… (Anaanguka chini.)” {Uk. 36}
(B) DHAMIRA NDOGO NDOGO
1. Ukosefu wa elimu
Dhamira hii inajitokeza katika tamthiliya, mwandishi anaonesha kuwa ukosefu wa elimu ya namna ya kupambana na Ukimwi unaifanya jamii kushindwa kulikabili gonjwa hili, ukosefu wa elimu unawafanya wengine kuamini ugonjwa huu ni wa kurogwa, wengine wanaamini ni ugonjwa unaletwa na mizimu na hata wengine kudhani ni majini.
2. Mapenzi na ndoa
Suala la mapenzi na ndoa pia limepewa nafasi katika tamthiliya hii, tukianza na suala la mapenzi, mwandishi anajadili mapenzi ya namna mbili, mapenzi ya dhati na mapenzi ya ulaghai.
(a) Mapenzi ya dhati
Baba Anna kwa familia yake. Mjomba kwa Suzi.Anna kwa wazazi wake.Anna kwa Suzi.Suzi kwa Joti
(b) Mapenzi ya ulaghai
Joti kwa Suzi. Joti kwa Chausiku.Chausiku kwa Joti
3. Malezi kwa vijana
Mwandishi pia amegusia suala la malezi kwa watoto, mwandishi anaonesha kuwa, malezi bora kwa mtoto ni malezi ya wazazi wote wawili, yaani baba na mama, na anapokosekana mzazi mmoja huweza kumuathiri mtoto, katika tamthiliya hii tunamuona Suzi akilelewa na mama peke yake bila baba hali hii inachangia mtoto kuingia katika matatizo, hili linathibitishwa na mwandishi akimtumia muhusika Mama Suzi anaposema, “Kila siku ninasema mwanangu mdogo, mwanangu ni mtoto mzuri, leo Suzi unanifanyia hivi? Hivi baba yako angekuwepo ungefanya hivi? Ah Suzi, ungefanya?” {Uk.31}
Katika suala hili la malezi, mwandishi anatuambia kuwa kuwa, mzazi ndiyo mwalimu bora kwa malezi mema ya mtoto,rejea ukurasa wa 11, Mjomba na Baba ANNA wanaposema, “Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza…Na ndiye bora.” {Uk. 11} hivyo wazazi wawafundishe vema watoto wao, lakini wazazi wasipofanya hivyo, walimwengu watawafundisha na kwa kawaida walimwengu hufundisha katika upotofu, rejea ukurasa wa 10-11, Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.” {Uk.10-11}
4. USALITI
Usaliti ni dhamira nyingine inayojitokeza katika tamthiliya hii, kwa mfano mwandishi anaonesha usaliti unaofanywa na Baba Joti kwa mke wake, Baba Joti anaisaliti ndoa yake kwa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, hili linathibitishwa na Mama Anna anaposema, “Lakini leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu nguru anayeichimba ndoa yangu.” {Uk. 7}
Usaliti mwingine, tunaona kwa Joti, pamoja na kwamba Joti anakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Suzi anaamua kumsaliti na kuanzisha mahusiano na wanawake wengine, mwandishi analithibitisha hili akimtumia muhusika Suzi anaposema, “Ndiyo maana mie nilikuwa nakataa Joti. Nishaambiwa kwamba unawasichana wengi shuleni na mtaani kwetu.” {Uk. 21}
Usaliti mwingine unajitokeza kwa Joti na Chausiku, mwandishi anaonesha kuwa Joti pamoja na kuwa na mahusiano na Chausiku anamsaliti Chausiku kwa kuwa na mahusiano na wasichana wengine, Joti anapewa vitu na Chausiku naye anawapa wanawake wengine, rejea ukurasa wa 22, Chausiku anaposema, “Toka hapa. Nimesikia habari zako. Kila msichana unamtaka tu. Mie nakununulia fulana ya mazoezi wewe unahonga kinyago chako kile. Bisha…Nikikupa hela ya kununua peni we unanunulia bazooka visichana vyako.” {Uk. 22} lakini si Joti tu ndiye anamsaliti mwenzake, mwanandishi anatuonesha kuwa, hata Chausiku pia, anamsaliti Joti kwa kuwa na mahusiano na wanaume wengine, rejea ukurasa wa 22-23, Mwarami anapomwambia Joti, “Sasa ndiyo kuparamia mpaka wasichana wakubwa wa mtaani? Fikiri juu ya Chausiku, Yule msichana mjuvi wa mji ambaye pia anachukuliwa na Yule mpemba muuza duka.” {Uk. 22-23}
5. ATHARI ZA UTANDAWAZI
Mwandishi pia amejadili suala la utandawazi na athari zake, mwandishi anaonesha namna utandawazi unavyochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu tabia na maadili ya watoto na vijana, kwa mfano tunawaona akina Joti, Jumbe, Choggo na Mwarami wanajiingiza katika mahusiano ya kingono wakiwa watoto wadogo kutokana na kuathiriwa na video za ngono (sinema za X) wanazozitazama mtaani, mikanda hii ya ngono imekuwa rahisi sana kupatikana kutokana na utandawazi.
6. ATHALI ZA UKOLONI NA UKOLONI MAMBO LEO
Suala la ukoloni na ukoloni mambo leo pia limepewa nafasi katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna wakoloni walivyoharibu utamaduni wetu kwa kuuita ushenzi na hata tulivyopata uhuru, viongoni wetu wakaendelea kushikilia mawazo hayo potofu ya kikoloni ambayo kwa kiasi kikubwa tunaangamia wenyewe, hili mwandishi analithibisha akimtumia Mtambaji anaposema, “Mila zetu hazikukataza kutoa mafunzo ya elimu ya jinsia…Wakoloni na vibaraka wao ndio wanaostahili kulaumiwa wakoloni walipiga vita jando na unyago wakidai eti ni ushenzi.” Mtambaji anaendelea kutuambia tena, “Viongozi wetu nao wakaendeleza mawazo hayo hata baada uhuru bila kutambua kuwa wanajiua wenyewe.” {Uk. 13-14}
7. NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Mwanamke amechorwa kama mlezi wa familia, mwandishi anatuonesha namna ambavyo mwanamke anakuwa mlezi mzuri wa familia, anaangaika hapa na pale kuhakikisha mtoto au watoto wake wanapata mahitaji yote muhimu kama vile chakula, mavazi na hata elimu, rejea ukurasa 30, Mama Suzi anaposema, “Mimi ninahangaika kukusomesha, wewe unanifanya hivi…Mama yako nimeungua viganja kwa kupika vitumbu ili mwanangu usome.” {Uk. 30}
Mwanamke amechorwa Kama mtu mwenyemsimamo, mwandishi anamtumia muhusika Anna kumuonesha mwanamke kama mtu mwenye msimamo katika maamuzi yake, tunamuona Anna pamoja na kusumbuliwa mara kwa mara na Mwarami kumtaka kimapenzi bado anashikilia msimamo wake ule ule wa kumkatalia, hata watu wazima wenye uwezo kipesa wanapomtaka Anna bado Anna anaonesha kutoyumba kimimamo kwa kuwakatalia. Rejea wimbo anaoimba Anna ukurasa wa 27,
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni x2”
Mwanamke amechorwa kama mtu anayepinga mabadiliko katika jamii, mwandishi anatuonesha kuwa mwanamke ni mtu asiyependa mabadiliko katika jamii, asiyependa kwenda na wakati, dunia inabadilika jamii inatakiwa kuwaelimisha vijana wao kuhusu elimu ya jinsia na mahusiano ,Mama Suzi anapinga, rejea Mama Suzi anaposema, “Tena ishia hapo hapo kaka! Huko si kunifundishia mwanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono ilitoka wapi hiyo? {Uk. 9}
Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na msimamo, mwandishi anatuonesha kuwa, mwanamke ni mtu asiye na msimamo katika maamuzi yake, mwandishi anamtumia Suzi, kuijadili nafasi hii, richa ya Suzi kuamua kuachana na Joti na hata anapogundua kuwa Joti anamahusiano na wanawake wengine bado anakubali kuendelea naye. (Rejea uk. 17 na 21)
Vile vile, mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe,Anamtumia mhusika Joti ambaye anawatumia wanawake ili kujistarehesha kingono, lakini pia tunaona namna watu wanavyotumia pesa na vitu vya thamani ili kuwarubuni wasichana wapate kukidhi mahitaji yao ya kingono. {rejea ukurasa 27}
Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na elimu juu ya mambo ya jinsia na ukimwi, katika kuilezea nafasi hii, mwandishi anamtumia mhusika Mama Suzi, ambaye anaoneka kutokuwa na ufahamu mzuri juu ya masuala ya UKIMWI, kwa mawazo yake anaamini kuwa ugonjwa wa UKIMWI ni ugonjwa unaowahusu watu wakubwa tu, na watoto hawawezi kuambukizwa jambo ambalo si sahihi. Hata katika jamii yetu, wapo watu wanaoamini kuwa ugonjwa huu wa UKIMWI huwakumba watu wazima watoto na watu walio katika ndoa hawawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi jambo ambalo si kweli. Hivyo jamii inatakiwa kuelimishwa sana kuhusu ugonjwa huu.
WAHUSIKA
Katika kazi ya fasihi wahusika wanaweza kuwa watu, wanyama au vitu, na wahusika ndiyo wanaobeba dhamira za msanii, na katika kazi ya fasihi wahusika tunawagawa katika makundi mawili, wahusika wakuu na wahusika wasaidizi/ wahusika wadogowdogo
(a) Wahusika Wakuu
Katika tamthiliya hii, ina wahusika wakuu wawili, ambao ni Suzi na Joti.
1. SUZI
Ni binti anayesoma shule ya msingi
Ni binti asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, Mama yake anashindwa kumpa elimu hiyo akiamini kuwa umri wa Suzi haujafikia kupewa elimu hiyo.
Anajiingiza katika mapenzi akiwa mdogo.
Anakuwa na mahusiano ya kingono na mwanafunzi mwenzake anayeitwa Joti.
Ni binti wa pekee wa Mama Suzi.
Anapata mimba akiwa mwanafunzi na anafikiria kuiotoa mimba hiyo.
2. JOTI
Ni kijana wa kiume anayesoma shule ya msingi.
Ni kijana asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, baba yake anashindwa kumpa elimu hiyo akiamini kuwa umri wa joti haujafikia kupewa elimu hiyo.
Anajiingiza katika mahusiano ya kingono akiwa mdogo huku akiwa mwanafunzi.
Anajihusisha na mahusiano ya kingono na wasichana wengi, akiwemo Suzi, Chausiku, Gelda n.k.
Ni mvulana mlaghai, anawalaghai wasichana ili tu kutimiza haja zake za kingono.
Anaambukizwa virusi vya ukimwi
Anafariki kwa ugonjwa wa ukimwi.
(b) Wahusika wadogo wadogo
1. MAMA SUZI
Huyu ni mama yake Suzi. Anamlea Suzi bila baba. Anajishughulisha na biashara ndogondogo kama vile kuuza vitumbua ili kujipatia kipato. Anaamini kuwa mtoto mdogo hawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi. Anakumbatia mila na desturi zililozipitwa na wakati zinazokataza watoto/vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi.Anakataa katakata mtoto wake, Suzi kupewa elimu ya jinsia na ukimwi akiamini kuwa umri wake ni mdogo, na kufanya hivyo ni sawa na kumfundisha umalaya.Anamwadhibu mtoto wake (Suzi) baada ya kukuta vidonge vya kuzuia mimba katika mfuko wa sketi yake.
2. BABA JOTI
Ni baba yake na Joti.Anaamini kuwa ukali wa mzazi na viboko ndiyo suluhisho la kuwazuia watoto kujiingiza katika mambo mabaya. Anakataa katakata elimu ya jinsia na ukimwi kutolewa kwa watoto/vijana.Anaangaika kuokoa uhai wa mtoto wake, Joti, kwa kutafuta tiba yake kila mahali. Anampoteza mtoto wake (joti) baada ya kufariki kutokana na ukimwi.
3. MAMA JOTI
Huyu ni mama yake Joti.Mke wa Baba Joti. Rafiki yake Mama Suzi. Anahisi mume wake ana uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine, hali inayomlazimu kuwanunulia kanga zenye maandishi ya mafumbo ili kuwapasha wezi wake.Yeye na mumu wake (Baba Joti) wanashindwa kumpa Joti elimu ya jinsia na ukimwi.
4. BABA ANNA
Huyu ni baba yake Anna.Anaamini kuwa elimu ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru na janga la ukimwi.Kwa kushirikiana na mke wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya jinsia na ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
5. MAMA ANNA
Huyu ni mama yake Anna. Ni mke wa Baba Anna.Kwa kushirikiana na mume wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya jinsia na ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
6. ANNA
Mtoto wa kike wa Baba Anna na Mama Anna.Ni mwanafunzi wa Shule ya msingi.Amepewa elimu ya jinsia na ukimwi, elimu inayomsaidia kupambana na vishawishi vya kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mdogo.Ana mkatalia Mwarami kuwa naye kimapenzi.
Wahusika wengine katika tamthiliya ya kilio chetu ni jirani, mwarami, chogo, mjomba, jumbe, fausta, chausiku na mpemba.
MIGOGORO
Migogoro ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili, unaweza kuwa mgogoro kati ya mtu na mtu, mtu na kikundi cha watu, kikundi kimoja na kikundi kingine cha watu au unaweza kuwa mgogoro wa mtu na nafsi yake. Katika tamthiliya hii, mwandishi ameweza kuibua na kuonesha migogoro mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo imeweza kusaidia katika ujenzi wa dhamira mbalimbali zilizoweza kujitokeza katika kazi hii, migogoro iliyojitokeza katika tamthiliya hii ni:
Mgogoro kati ya Mama suzi na mwanaye,(Suzi) chanzo cha mgogoro ni Mama Suzi kukuta kasha la vidonge vya kuzuia mimba kwenye mfuko wa sketi ya Suzi, mgogoro unakua zaidi Mama Suzi kuamua kumuadhibu kwa kumchapa Suzi hadi anapotokea Mjomba na Baba Anna, kuamulia mgogoro huo na kushauri jambo la msingi ni kumpa elimu ya jinsia na si kutumia ukali na viboko, kama ambavyo Baba Anna anasema, “Watoto wajazwe elimu, waone uchafu na hatari ya kufanya haya. Siyo kuwatia hofu tu. Je leo ukifa ama kulazimika kuwa mbali nawe? Si atafanya tu maana mtia hofu hayupo?” {Uk. 13}
Mgogoro kati ya Mjomba na Mama Suzi, chanzo cha mgogoro ni kitendo cha Mjomba kumshauri Mama Suzi kuacha kumuadhibu Suzi na badala yake apewe elimu ya jinsia na mahusiano ya kimapenzi jambo linalopingwa na Mama Suzi na hivyo kuibua mgogoro. {Rejea ukurasa wa 8-14}
Mgogoro kati ya Suzi na Joti, mgogoro huu unaibuka baada ya Suzi kupigwa na mama yake sababu ya vidonge vya kuzuia mimba alivyopewa na Joti, mgogoro huu unafikia hatua ya Suzi kuamua kuachana na Joti, suluhisho la mgogoro huu, wanaamua kurudiana na kuendelea na uhusiano wao. (Rejea uk. 17 na 21)
Mgogoro kati ya Mwarami na rafiki zake yaani Jumbe, Joti na Choggo. Chanzo cha mgogoro ni kitendo cha Mwarami kutokuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana, hatua inayosababisha kumtishia kumfukuza katika kundi lao, rejea ukurasa wa 24, Jumbe anapomwambia Mwarami, “Sasa bwana hapa kwenye grupu letu hatutaki tabia hiyo ya ushamba. La sivyotutakutoa umemba.” Suluhisho la mgogoro huu ni Mwarami kuamua kumshawishi Anna kimapenzi hata hivyo juhudi zake zinagonga mwamba.
Mgogoro kati ya Mama Joti na Mwanamke anayedhani anaingilia ndoa yake,Mama Joti anaona suluhisho la mgogoro huu ni kununua kanga zenye maneno ya vijembe ili kumpasha na kumuumiza roho, Rejea Mama Joti anaposema, “Lakini leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu nguru anayeichimba ndoa yangu…Ngoja kwanza nimpashe najua litamuuma tu.” {Uk. 7}
Mgogoro mwingine ni kati ya Chausiku na Joti, chanzo cha mgogoro huu ni baada ya kugundua kuwa Joti anamahusiano ya kimapenzi na wasichana wengine, mgogoro unafikia hatua ya Chausiku kumtishia kumdhuru Joti, kama anavyosema, “We usinifanye mie bwege mwenzio…wewe ndiyo unajigonga gonga. Wewe na visichana vyako hivyo nitawachoma moto mie! Nyie hamnijui, ohoooo!” {Uk. 22}
Mgogoro wa Suzi na nafsi yake, chanzo cha mgogoro huu ni kitendo cha kuambiwa na mama yake kuwa shangazi yake ataenda kumpima mimba, Suzi anaona suluhisho la mgogoro huu ni kutokubali kwenda kupimwa mimba na shangazi yake na badala yake kumtafuta mwanaume anayehusika na mimba hiyo (Joti) kuzungumza naye, rejea Suzi anaposema, “Oh Mungu wangu! Nifanye nini sasa? Siwezi kumruhusu shangazi akanipime…oh, nifanye nini mie! Nimtafute Joti, lazima niongee naye.” {Uk. 31}
UJUMBE
Ujumbe ni funzo analolipata fanani anaposoma ama kusikiliza kazi za fasihi, pamoja na ujumbe pia kuna maadili mbalimbali hupatikana, katika tamthiliya hii kuna mafunzo mbalimbali ambayo msomaji wa kazi hii anaweza kuyapata, mafunzo hayo ni kama:
Elimu ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru vijana na mimba za utotoni(mimba zisizotarajiwa) na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Ukimwi hauchagui rika, mwandishi anatupa ujumbe kuwa gonjwa hili la UKIMWI hauchagui mtu, kila mtu anaweza kuupata, kama tunavyoona kwa Fausta na Joti, ni watoto wadogo lakini wanaathirika na virusi vya ukimwi na kusababisha vifo vyao.
Asiyefunzwa na mama yake, hufunzwa na ulimwengu, hili ni funzo linguine tunalilipata katika tamthiliya, mwandishi anatufundisha umuhimu wa wazazi kuwafundishi watoto wao maadili mema na si kuwaacha watoto wakajifunza wenyewe mtaani, wakiwaacha hivyo, huko hujifunza mambo yasiyofaa, tunaona kwa Suzi, Joti, Mwarami, Choggo, Jumbe, wazazi wao hawakuwafundisha elimu ya jinsia na mahusiano watoto wakajifunza wenyewe mambo machafu na hataimaye yakawaletea madhara.
Wazazi ndiyo walimu bora kwa malezi bora na maadili mema kwa watoto wao. Mwandishi anaendelea kutufundisha kuwa, ili vijana wetu wawe na tabia njema, mzazi ni mwalimu bora kabisa anayeweza kumfundisha mtoto wake vema, rejea mwandishi akimtumia muhusika Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.”
Kinga ni bora kuliko tiba. Ni vizuri jamii ikajikinga na magonjwa mbalimbali, kuliko kutojikinga na baadaye kuanza kutafuta tiba, tiba huwa gharama sana kuliko kujikinga, tunamuona Baba Joti akitumia gharama kubwa kutafuta tiba ya mtoto wake, kama ambavyo mwandisha anasema, “Mtani ushauza rasilimali zako kuuguza mtoto. Ushajitia umskini kwa kuhangaika…” {Uk. 34} Hivyo basi ni vema jamii ikaamua kujikinga dhidi ya matatizo mbalimbali kwani matatizo hayo pindi yanapokukumba huwa ni gharama sana kuyatatua na wakati mwingine matatizo mengine huwa hayana tiba kama tunavyoona katika ugonjwa wa UKIMWI.
Ngono zembe ni chanzo cha maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa, Tunamuona Joti akiambukizwa virusi vya ukimwi kutokana na kushiriki ngono zemba, vilevile tunamuona Suzi akipata mimba na hata kuwa katika wasiwasi wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI kutokana na kushiriki ngono zemba. (Rejea ukurasa wa 4 na 34)
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha ya kawaida, sentensi fupifupi na inayoeleweka kwa urahisi, pamoja na hayo mwandishi pia ametumia lugha ya kisanaa yenye mbinu mbalimbali za kisanaa kama vile nahau na tamathari za semi.
Matumizi ya methali
“Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha.” Uk.
“Shukrani ya punda mateke.” {Uk. 19}
Matumizi ya misemo na nahau
Shoga, mtakatifu wa kwenye mwanga si lazima awe mtakatifu gizani. {Uk. 4}
“Kakanyaga nyaya.” {Uk. 4}
“Potelea kwao…” uk. 9
“Makapera kibao, mume wangu wa nini. Uk. 7
“Wembamba wa reli treni inapita, uk 6
Kifua simkingii, maana siwi naye. Uk 6
“Kwa mashairi nimekuvulia kofia siku nyingi.” Uk.6
“We pita juu mie nipite chini…”uk 19
Mbona umetuanika juani. Uk 16
“Hakikisha ndege mjanja ananasa katika tundu bovu.” Uk. 24
(c) Matumizi ya taswira/lugha ya picha
Dubwana, Manaa yake ni kitu au mtu mwenye umbo kubwa lisilo la kawaida au la hovyo hovyo, mwandishi ametumia neno dubwana kitaswira kuufananisha ugonjwa wa Ukimwi sawa na jambo linalotisha, kuogopesha. (Rejea ukurasa wa 1-2)
Gizani, gizani ni mahali pasipokuwa na mwanga, hivyo mwandishi ametumia neno giza, akimaanisha kukosa maarifa au kutokuwa na ufahamu ya jambo fulani, kwa kifupi kukosa elimu, Rejea mtambaji anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani…watoto ndio kabisa. Wapo katika giza nene.” {Uk. 13}
(d) Matumizi ya tamathali za semi.
Tashibiha,
Hizi ni tamathari ambazo hulinganisha vitu kwa kutumia viunganishi kama, mfano wa, sawa na, mithili ya, kama vile. N.k. baadhi ya tashibiha zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
“Wewe nawe unakuwa nyuma nyuma Kama koti.” Uk. 4
“Shoga mbona unakuwa mgumu kama mpingo?” uk. 5
“Watu walipukutika, wakapukutika Kama majani ya kiangazi.” Uk.1
“Lile Dubwana limetanda Kama utando wa buibui.” {Uk.13}
“Miti inayoungua Kama mabua.” Uk. 6
Sitiari
Hizi ni tamathari za semi ambazo hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi, mfano wa tamathali zilizotumika ni pamoja na:
“We mbwa mweusi.” Uk. 8
“Nyoka wee.” Uk.9
Mjalizo
Hii ni aina ya tamathali za semi ambazo msanii/mwandishi huitumia kutaja vitu au mambo yaliyo katika orodha bila kutumia viunganishi. Mfano:
“…Lakini soma maneno yake. Yamejaa kejeli, ushari, uchimvi, kusengenyana na kufumbiana mafumbo ya kila aina.” Uk. 6
Nidaa
Hizi ni tamathali za semi, zinazoonesha hali ya kushangaa au kushangazwa na jambo Fulani, mfano wa tamathali hizi ni:
“Ai, ai, lahaula lakwata…weye, hiki kitoto?” {uk. 9}
“Oi, oi, oi, toba! Kile si kitoto kama cha kwangu…” {uk.10}
Takriri
Hii ni hali ya kurudiarudia maneno, neno, silabi au sauti zinazolingana katika kazi ya fasihi ili kusisitiza au kutia mkazo jambo fulani. Mfano wa takriri zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
“Watu walipukutika, wakapukutika Kama majani ya kiangazi. Wakapukutika.” Uk. 1
“Waongo! Waongo wakubwa.” Uk. 3
“Vifo vikawazoa, vikawazoa…vikawazoa.” uk. 2
“Piga domo, piga doma, nikashinda.” UK. 16
Tanakali sauti
Hii ni aina ya tamathali ambayo sauti ya kitu fulani huigwa ili kwa lengo la kuburudisha au kuipa dhamira uzito falani. Mfano wa tanakali sauti zilizotumika katika tamthiliya hii ni
“Wacha moyo unipwite pwi,pwi,pwi…” uk.16
Tashititi
Hii ni aina ya tamathari ya semi ambayo mtu huuliza swali huku jibu lake akilifahamu, mfano wa tashititi zinazojitokea katika tamthiliya hii ni:
“Huyu ni Suzi kweli au nani?” uk.15
MTINDO
Mtindo ni jinsi msanii anavyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza jambo fulani katika kazi ya fasihi, na mtindo ndiyo huweza kumtofautisha msanii/mwandishi mmoja na mwandishi mwingine. Mtindo hutumika kuipamba kazi ya fasihi, baadhi ya mitindo nayotumika katika kazi hii ni pamoja na:
Matumizi ya hadithi ndani ya tamthiliya
Mwandishi ametumia mtindo wa hadithi ambao ni utanzu wa fasihi simulizi ndani ya tamthiliya, mtindo huu unajidhihirisha ukurasa wa kwanza, Mtambaji anapoanza kusimulia hadithi anaposema, “Paukwa” na hadhira inaitikia “Pakawaaaaaaa” na Mtambaji anaendelea, “Hapo zamani za kale paliondokea kisiwa kimoja…” {Uk. 1} Ni utanzu wa hadithi pekee ndiyo huwa na mwanzo wa namna hiyo.
Matumizi ya wimbo/shairi ndani ya tamthiliya
Mwandishi pia ametumia wimbo kuipamba kazi yake, wimbo unajitokeza ukurasa wa 27 Anna anaimba wimbo unaowataka wanaume wanaomtaka kimapenzi kuacha kumfuatafuata, muda wake wa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi haujafika bado mwanafunzi.
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni x2”
Matumizi ya lugha ya majibizano/dialojia na masilmulizi
Kama ilivyo ada, mtindo wa lugha unaotumika katika tamthiliya, kwa asilimia huwa ni mtindo wa majibizano, yaani dialojia. Hivyo basi hata katika tamthiliya hii, mwandishi kwa kiasi kikubwa ametumia mtindo wa majibizano na kidogo ametumia masimulizi, (Rejea masimulizi ya Mtambaji ukurasa wa 1-2, 3-4, na 36)
Matumizi ya nafsi zote tatu
Pia nafsi zote tatu zinajitokeza katika tamthiliya hii,
Nafsi ya kwanza, mfano, Mimi nawashangaa… {Uk. 6} Najua litamuuma tu (uk.7), Tumebomoa ghala imara…” {Uk. 6}
Nafsi ya pili, mfano, “Utamaliza kanga zilizoandikwa kila aina ya maneno…” Wewe unamwona Fausta alikuwa mdogo?
Nafsi ya tatu, mfano …alikufa kwa ukimwi” uk. 9, atakutafuta tu mwenyewe.” (uk 17), “Wanashindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu.” (Uk. 13)
MUUNDO
Muundo ni mfuatano wa masimulizi au visa katika kazi ya sanaa ya fasihi, hivyo basi.muundo wa tamthiliya hii ni wa moja kwa moja, yaani visa vyake vimepangwa kuanzia kisa cha kwanza, kati hadi mwisho, katika kuvipanga visa vyake, mwandishi ameigawa kazi yake katika sehemu sita, ambazo amezipa majina, Sehemu ya kwanza, Sehemu ya Pili, ya Tatu, ya Nne, Tano na Sehemu ya Sita.
Sehemu ya kwanza.
Mtambaji anasimulia habari za Dubwana (Ukimwi), anasimulia namna wakubwa wanavyoelimishana namna ya kujilinda na ugonjwa huo, huku wakiwaacha watoto wakiangamia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi.
Sehemu ya Pili
Hapa mwandishi anatuonesha nyumbani kwa Mama Suzi, Mama Suzi na Mama Joti wanapeana habari za kifo cha Fausta kilichosababishwa na ukimwi, Mama Suzi anakuta kasha la vidonge kwenye mfuko wa sketi ya Suzi wakati akifua jambo linalozua mgogoro kati ya Suzi na mama yake, Mjomba na Baba Anna wanamshauri Mama Suzi kuacha kutumia ukali na badala yake anatakiwa kumpa elimu ya jinsia binti yake ili ajitambue jambo linalopingwa vikali na Mama Suzi.
Sehemu ya Tatu
Hapa mwandishi anatuonesha mtaani, Joti anakutana na Suzi, Suzi anaamua kuachana na Joti kwa sababu ya vidonge vya kuzia mimba alivyopewa na Joti kumsababishia kupigwa na mama yake. Joti anawasimulia wenzake namna alivyofanikiwa kumpata Suzi, Joti, Jumbe, Choggo na Mwarami wanaenda mtaani kuangalia sinema za X.
Sehemu ya Nne
Tukio linatendeka njiani, Joti na Suzi wanakutana, Suzi anamlaumu Joti kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wasichana wengine, wanaamua kurudisha uhusiano wao, Joti anaanza kujisikia vibaya, Jumbe anaamua kumpeleka nyumbani, Mwarami anaonekana akimshawishi Anna amkubalie ombi lake la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi, Anna anaonesha msimamo anamkatalia, mwandishi pia anatuonesha namna Anna anavyoshinda vishawishi vya kingono.
Sehemu ya Tano
Tukio linatendeka chumbani kwa Suzi akiwa na Anna, Suzi anajisikia vibaya, anahisi huenda ana mimba, anataka kuitoa, rafiki yake Anna anamshauri kuachana na mpango huo kwani ni hatari, anaamua kwenda kwa Joti kuzungumza naye suala hilo.
Sehemu ya Sita
Hii ni sehemu ya mwisho, mwandishi anatuonesha nyumbani kwa Baba Joti, tunaona namna Baba Joti alivyoangaika kwa waganga mbalimbali kutafuta tiba ya Joti bila mafanikio, mwisho wanaamua kumpeleka hospitali, huko wanapata wajibu kuwa Joti amethirika na virusi vya ukimwi, Jirani anamshauri Baba Joti kumpeleka Joti kwa mganga mwingine, Mjomba anamshauri Baba Joti kuachana na mpango huo kwani ugonjwa alionao Joti hauna tiba wala dawa. Suzi anawasili kwa akina Joti anagundua Joti ana ukimwi, Joti anafariki dunia, Suzi anakuwa na wasiwasi kama naye atakuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi, anabaki akijutia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi. Na mchezo unaishia hapo.
MANDHARI
Mandhari ni sehemu au eneo ambalo visa na matukio hutendeka katika kazi ya fasihi, katika kazi ya fasihi mandhari huweza kuwa mandhari halisi au ya kubuni, katika tamthiliya mwandishi ametumia mandhari ya kubuni, hivyo basi, mandhari ya tamthiliya hii yanaweza kuwa sehemu yoyote ile katika nchi za Kiafrika. Pia mwandishi anatuonesha visa na matukio yakitendeka mandhari ya nyumbani, mtaani, njiani n.k.
Mandhari ya nyumba
Katika mandhari ya nyumbani, tunaona nyumbani kwa Mama Suzi na Nyumbani kwa Baba Joti, kwa Mama Suzi tunaona ukuta uliowekwa kati ya mzazi na mtoto kuhusu elimu ya jinsia kwa mtoto, Mama Suzi anamuadhibu Suzi kwa kukuta vidonge vya kuzuia mimba kwenye mfuko wa sketi ya Suzi, Suzi anaanza kujisikia vibaya, anafikiria kuitoa mimba. Nyumbani kwa Baba Joti, tunaona kuumwa kwa Joti, kugundulika kuwa ana ukimwi na kufariki kwake.
Hivyo mwandishi ametumia mandhari hii, ili kufikisha dhamira ya umuhimu wa elimu ya jinsia kwa watoto, malezi bora ya mtoto, tatizo la ugonjwa wa ukimwi na athari zake katika familia, n.k.
Mandhari ya Mtaani
Katika mandhari haya, mwandishi, anatuonesha Joti na Suzi wakiwa katika mazungumzo ya uhusiano wao wa kimapenzi, pia tunaoneshwa kuwa ni mahali ambapo Joti na wenzake hukutana na kupanga mambo yao ya mapenzi. Mwandishi anatumia mandhari haya, kuonesha namna watoto wanavyoharibikiwa kitabia mtaani, mandhari ya njiani inatuonesha namna watoto wakike wanavyosumbuliwa na wanaume wasiokuwa waadilifu ambao huwataka kimapenzi.
FALSAFA YA MWANDISHI
Falsafa ni mchujo wa mawazo ya mwandishi kuhusu maisha na jamii yake. Falsafa ya mwandishi wa tamthilia hii anaamini kuwa, ili jamii yoyote ile iweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii husika, elimu ni nyenzo muhimu sana ya kupambana na changamoto hizo. Na elimu hiyo isitolewe kimatabaka.
MTAZAMO WA MWANDISHI
Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu, ana mtazamo kuwa, matatizo yote yanayotokea katika jamii chanzo ni jamii yenyewe na jamii yenyewe ndiyo inayotakiwa kukabiliana na matatizo hayo, na ndiyo maana anaitaka jamii yake ibadilike.
MSIMAMO WA MWANDISHI
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anaitaka jamii yake ibadilike ili kuendana na wakati, na anaitaka jamii kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu au tamthiliya hii ni Kilio Chetu,kilio chetu ina maana ya tatizo, balaa au janga linapoingia katika jamii ni letu sisi sote. Hivyo basi, jina la kitabu Kilio Chetu linasadifu sana yaliyomo katika tamthiliya hii. Tukianza na:
Tatizo la ukimwi
Mwandishi anajadili ukimwi kuwa ni ugonjwa hatari sana, ni ugonjwa usiobagua mkubwa wala mtoto, kama mwandishi anavyosema, “Ukimwi hauchagui mkuwa wala mdogo.” {Uk. 25} hii inathibitisha kuwa tatizo hili la ukimwi ni letu sote tunatakiwa wote kupambana nalo, na hapa ndipo linapokuja suala la Kilio Chetu.
Elimu ya jinsia
Mwandishi pia anaonesha kuwa suala la watoto/vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi ni kilio cha jamii, jamii inasisitiza na kupigia kelele suala la vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi, kwa mfano, mwandishi anamtumia muhusika Baba Anna anaposema, “Mimi bwana nitaendelea kusisitiza juu ya elimu hii.” Mwandishi anaendelea kwa kusema akimtumia muhusika Mjomba, “Tutaendelea kuwaelimisha wazazi umuhimu wa elimu hii.” {Uk.12} Hivyo tunaona kuwa Baba Anna na Mjomba wanatoa kilio chao cha kutaka watoto kuelimishwa elimu ya jinsia.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
(A) KUFAULU KWA MWANDISHI.
Hapa tunaangalia kufanikiwa kwa mwandishi katika vipengele vya fani na maudhui, Kifani mwandishi amefanikiwa sana, tukianza na:
Mwandishi amefanikiwa kuwajenga wahusika wake vizuri, amewajenga wahusika katika rika tofauti tofauti na kila rika amefanikiwa kuwavisha uhusika unaendana na rika husika, na amafanikiwa kuonesha namna kila rika linavyoweza kuathiliwa na UKIMWI na kuitaka jamii kutoa elimu ya jinsia kwa kila rika.
Mwandishi amefanikiwa kuifanyanga lugha yake kiufundi, amefanikiwa kutumia lugha nyepesi inayoeleweka na kila mtu inayoambatana na matumizi ya methali, misemo/nahau na tamathali za semi, matumizi yote haya ya lugha yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha ujumbe uliokusudiwa na kuipamba kazi husika. (Rejea kipengele cha Matumizi ya lugha)
Katika suala la mtindo, mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, kwani amefanikiwa kutumia utanzu wa hadithi na wimbo kuipamba kazi yake na ikawa kazi ya kuvutia na inayovuta hisia za msomaji kupenda kuendelea kukisoma kitabu hiki zaidi na zaidi. (Rejea kipengele cha Mtindo)
Mwandishi ametumia muundo rahisi, muundo unaeleweka kwa urahisi na hivyo kumsaidia mwandishi kufikisha ujumbe alioukusudia kwa jamii husika, visa vyake amevipangalia vizuri hali inayomfanya msomaji apende kuendelea kukisoma kitabu hiki ukurasa mmoja hadi mwingine hadi anakimaliza kitabu hiki.
Kwa upande wa maudhui, mwandishi amefanikiwa kuonesha dhamira mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zina uhalisia katika jamii yetu. (Rejea dhamira)
Vilevile, kwa upande wa ujumbe, mwandishi amefanikiwa kutupa ujumbe au mafunzo muhimu sana ambayo kama jamii itayazingatia basi mafunzo haya yanaweza kuwasaidia sana. (Rejea Kipengele cha ujumbe)
Migogoro, mwandishi amefanikiwa kuibua migogoro, kuonesha chanzo, upeo na hata baadhi ya migogoro amefanikiwa kuitolea suluhisho. (rejea kipengele cha Migogoro)
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Mwandishi ameshindwa kutuonesha mwanamke aliyemuambukiza Joti virusi vya UKIMWI.
Mwandishi pia ameshindwa kutuonesha hatima ya akina Jumbe na Choggo kama nao waliathirika na UKIMWI au la, maana hawa wote matendo yao alikuwa yanafanana tu na Joti.
Mwandishi ameshindwa kutuambia alipo baba yake, kama amesafiri au amefariki.